Thursday, September 29, 2011

Yanga yafanya maangamizi yaisambaratisha Coastal Union 5-0


Davis Mwape akichanja mbuga

Kenneth Asamoah alitia kambani mabao mawili na kuiongoza Yanga kuwasambaratisha wagosi wa kaya ambao ni vibonde wa ligi Coastal Union kwa mabao 5-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mabingwa hao waliopoteza mvuto kwa mashabiki wao kutokana na kuanza ligi kwa kusuasua jana walionekana tofauti kabisa kwani katika dakika ya nne mshambuliaji wao wa kimataifa wa Ghana, Asamoah alifunga bao la kwanza kabla ya Shamte Ally, Davies Mwape, Nurdin Bakari na Mghana huyo kufunga kalamu hiyo ya kishindo.

Kiungo Idrisa Rajabu alitoa mchango mkubwa kwenye mauaji hayo kwa kutengeneza mabao matatu kati ya matano ikiwa ni mechi yake ya tatu kuanza kuitumikia Yanga.

Umakini huo wa safu ya ushambuliaji ya Yanga unamfanya kocha Sam Timbe kutomfikiria kabisa mshambuliaji wake Jerryson Tegete aliyefunguliwa na uongozi wake hivi karibuni.

Timbe aliwapumzisha Mwape, Shamte na Asamoah na kuwaingiza Rashid Gumbo, Julius Mrope na Hamis Kiiza.

Mabingwa hao sasa wamefikisha pointi 12, huku Coastal wakibaki mkiani na pointi zao nne katika ligi hiyo inayoongozwa na Simba yenye pointi 18.

Mshambuliaji Davies Mwape alijaribu kufunga bao la mapema katika dakika ya 2, lakini mpira wake wa kichwa ulidakwa na kipa wa Coastal Union, Omar Hamis na dakika mbili baadaye Asamoah alifungia Yanga bao la kuongoza akimalizia kwa kichwa krosi nzuri ya Idrisa Rajabu.

Mshambuliaji wa kimataifa wa zamani wa Kenya, Ben Mwalala alikaribia kuipatia timu yake bao katika dakika 11 baada ya kuunganisha vizuri krosi kutoka upande wa kulia iliyopigwa na Daniel Lianga, lakini kipa wa Yanga, Yaw Berko aliupangua mpira huo.

Winga Shamte Ally aliipatia Yanga bao la pili katika dakika ya 21 akiunganisha kwa umakini krosi ya Asamoah kutoka upande wa kushoto, wakati Wagosi hao wakishaanga uwanja wa Taifa, Mwape aliendeleza kalamu ya mabao kwa kufunga bao la tatu kwa Yanga katika dakika ya 30 kwa kuunganisha kwa shuti kali pasi ya Rashid kutoka winga ya kushoto.

Mshambuliaji Mwalala alijaribu kuwaongoza vijana wake bila ya mafanikio kwa sababu katika dakika ya 35 alipiga shuti kali lililopanguliwa na Berko na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Nurdin Bakari aliipatia Yanga bao la nne katika dakika ya 41, akimalizia pasi nzuri ya Asamoah.

Yanga ambayo safu yake ya ushambuliaji ilikuwa ikilaumiwa kwa ubutu ilionekana kuwa bora mbele ya mabeki dhaifu wa Coastal Union ambao wameruhusu timu hiyo kufungwa mechi sita kati ya nane ilizocheza msimu huu.

Coastal mabingwa wa mwaka 1988 wanaofundishwa na Hafidh Bardu walishindwa kucheza kabisa na kumtegemea Mwalala wakati wapinzani wao Yanga wakitawala asilimia 80 ya ya mchezo huo katika nafasi ya kiungo na ushambuliaji.

Asamoah alipachika bao la tano katika dakika ya 46 akipokea krosi ya Rajabu na kuifanya Yanga kushinda kwa mabao 5-0. Asamoah amefunga mabao manne tangu msimu huu wa Ligi Kuu uanze.

Kocha wa Coastal Union, Badru alimpumzisha kipa wake Hamis aliyeruhusu mabao manne na kumwingiza Godson Mmasa, pia Coastal ilimtoa Mwinyi Abdulrahman na kumuingiza Said Swed

Arsenal,Barcelona zafanya kweli ligi ya mabingwa ulaya

Arsenal 2-1 Olympiakos


Bate borisov 0-5 Barcelona


Valencia 1-1 Chelsea


AC Milan 2-0 Victoria Pulzen