Monday, January 30, 2012

Djokovic bingwa Australia open amchabanga Nadal, Azarenka bingwa kwa wanawake

Novak Djokovic
Djokovic bingwa wa Tennis kwa wanaume

Novak Djokovic kutoka Serbia, Jumapili alimshinda Rafael Nadal kutoka Uhispania, katika fainalil ya mashindano ya tennis ya Australian Open, iliyofanyika mjini Melbourne.
Djokovic alipata ushindi wa 5-7, 6-4, 2-6, 6-7, 7-5.
DJOKOVIC VS NADAL

Pambano hilo sasa limeandikishwa katika historia kama shindano ambalo limechukua muda mrefu zaidi katika historia ya mashindano ya tennis ya Open.
Ushindi huo wa tatu mfululizo katika mashindano ya Grand Slam, umemchukua Djokovic muda wa saa tano, na dakika 53.
Limeandikisha historia pia kwa kuwa pambano la muda mrefu zaidi kwa mchezaji mmoja kwa mmoja katika mashindano ya Australian Open.
Akimpongeza mpinzani wake, Djokovic alimsifu Rafael Nadal, akisema ni kati ya wachezaji bora zaidi katika historia ya tennis.
Alimpongeza pia kwa pamoja wote kuandikisha historia ya fainali ya muda mrefu zaidi, na akitumaini kwamba watakutana katika mapambano mengine siku zijazo, ila Jumapili ilikuwa haiwezekani kuwapata washindi wawili kwa pamoja.
Fainali ya kitambo ya Grand Slam iliyochukua muda mrefu zaidi ilikuwa ni mwaka 1988, mashindano ya US Open, wakati Mats Wilander, raia wa Sweden, alipomshinda Ivan Lendl, mchezaji wa Czechoslovakia, na ambaye baadaye alibadilisha uraia na kuwa Mmarekani.
Pambano hilo lilichukua muda wa saa 4, dakika 54.

Azarenka

Azarenka vs Sharapova

Kwa upande wa fainali ya kina dada, siku ya Jumamosi, Victoria Azarenka alimshinda Maria Sharapova na kupata ushindi wake wa kwanza wa mashindano ya Grand Slam.
Ushindi huo umemfanya kuwa ni nambari moja sasa katika tennis ya kina dada ulimwenguni.
Azarenka, mwenye umri wa miaka 22, na ambaye ni raia wa Belarus, alimshinda Sharapova kutoka Urusi 6-3 6-0, baada ya muda wa saa nzima, na dakika 22.

Ghana yailiza Mali

Andre Dede Ayew
Ayew akishangilia goli la pli la Ghana

Ghana inaelekea kufuzu kwa robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika, baada ya Jumamosi kuishinda Mali magoli 2-0.
Asamoah Gyan ndiye aliyefunga bao la kwanza la Black Stars.
Ghana vs Mali

Andre 'Dede' Ayew kisha aliwachanganya walinzi wa Mali na kupitia nafasi iliyojitokeza, aliandikisha bao la pili la Ghana.
Awali Cheick Diabate mara mbili ilikuwa nusra aifungie Mali magoli, lakini kweli bahati haikuwa yake, kwani mipira yote iligonga goli, lakini kamwe mpira ulikataa kugusa nyavu katika mechi hiyo iliyochezewa mjini Franceville.
Ghana inaongoza kundi D kwa pointi sita, lakini kimahesabu, mataifa ya Guinea na Mali bado yana nafasi ya kufuzu kuingia robo fainali.
Guinea kwa hakika ilithibitisha uwezo wake katika mashindano hayo kwa kuiangamiza bila huruma Botswana, magoli 6-1, katika mechi ambayo pia ilichezewa mjini Franceville.
Guinea inatazamia wingi huo wa mabao huenda ikawa jambo zuri, na inasubiri kwa hamu kusikia matokeo ya mechi kati ya Mali na Botswana Jumatano ijayo mambo yatakuwa vipi, na wakati ambao wao watacheza na Ghana.

Zambia yawaliza wenyeji kombe la mataifa ya Afrika

Wachezaji wa Zambia
Wachezaji wa Zambia wakishangilia bao

Zambia ilijitengea nafasi katika robo fainali za michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa kuwashinda wenyeji Equatorial Guinea bao 1-0 katika mechi ya kundi A, na kuongoza kundi hilo, ikiwa na pointi 7.
Nahodha Chris Katongo aliifungia Zambia bao hilo katika dakika ya 67.
Zambia 1-0 Guinea

Ushindi huo unamaanisha kwamba Zambia huenda wakaepuka kucheza na Ivory Coast katika robo fainali, nchi ambayo inatazamiwa kuongoza kundi B.
Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Equatorial Guinea kushindwa, na ambao wanashirikiana na Gabon kama wenyeji wa mashindano hayo.
Ilikuwa pia ni mara ya kwanza kwa kocha mpya Gilson Paulo akiitizama timu yake ikifungwa.
Equatorial Guinea imo katika nafasi ya pili katika kundi A, ikiwa na pointi 6, Libya ina nne, na Senegal ni ya mwisho ikiwa haina pointi zozote.
Wenyeji Equatorial Guinea tayari walikuwa wamefuzu, na Zambia walihitaji tu kuondoka sare kuingia robo fainali.
Ushindi wa Chipolopolo unamaanisha kwamba sasa watasafiri kuelekea hadi uwanja wa Bata, katika kujiandaa kwa mechi yao ya robo fainali siku ya Jumamosi, tarehe 4 Februari.
Kinyume na Senegal ambao wanarudi nyumbani bila hata pointi moja, Libya inaondoka mashindano hayo baada ya kupata ushindi wa magoli 2-1 katika mechi yake ya Jumapili dhidi ya Senegal.
Ihab Albusaifi alifunga katika kipindi cha kwanza, na vile vile katika kipindi cha pili.
Deme Ndiaye aliifungia Senegal, na kinyume cha matazamio ya wengi, timu hiyo sasa inarudi nyumbani baada ya kushindwa katika mechi tatu.
Hata hivyo bado ni fahari kwa timu ya Libya ya Mediterranean Knights kuondoka mashindano hayo kwa kupata ushindi katika mechi, ikiwa ni ushindi wao wa kwanza tangu mwaka 1982, wakati nchi yao ilikuwa mwenyeji wa mashindano hayo
Huu ni ushindi wao wa kwanza kwa mechi ya Kombe la Mataifa ya Afrika, nje ya nchi yao.
Watajipongeza kwa kufikia hatua hiyo, hasa wakikumbuka kwamba ni hivi majuzi tu nchi yao imeanza kupata kutulia baada ya matatizo mengi.

Arsenal yailipua Aston Villa kombe la F.A

Robin Van Persie na Theo Walcott
Van Persie na Walcott

Robin van Persie ilibidia afanye kazi ya ziada Jumapili, na hatimaye akifunga magoli mawili ya penalti, na kuiwezesha Arsenal kuponea chupuchupu kuondolewa katika raundi ya nne ya Kombe la FA, baada ya kupambana na Aston Villa, hatimaye ikishinda 3-2.
Kufikia mwisho wa nusu ya kwanza ya mchezo, Arsenal ikichezea uwanja wa nyumbani wa Imarati, tayari ilikuwa imeachwa nyuma kwa magoli 2-0.
Arsenal vs Aston Villa

Mabao hayo yalikuwa yamefungwa na Richard Dunne (kwa kichwa) na goli la mkwaju wa kupinda kupitia mchezaji Darren Bent.
Lakini magoli matatu katika muda wa dakika saba yaliubadilisha mchezo kabisa, na Van Persie akibadilisha mambo kwa mkwaju wa penalti, baada ya Dunne kumchezea vibaya Aaron Ramsey.
Theo Walcott alisawazisha kabla ya Van Persie kuandikisha ushindi, kwa kupata bao la pili la penalti, kufuatia Bent kucheza mchezo usio halali dhidi ya Laurent Koscielny.
Arsenal, mabingwa mara 10 wa Kombe la FA, sasa watacheza na mshindi atakayepatikana katika mchezo wa raundi ya nne utakaorudiwa kati ya Middlesbrough na Sunderland.
Sunderland na Middlesbrough walipocheza katika mechi ya awali Jumapili mchezo ulikwisha kwa sare ya 1-1.
The Gunners watacheza mechi hiyo wakifahamu sasa wana uwezo wa hatimaye kuendelea na mashindano hayo, na kuwaletea mashabiki wao kombe ambalo wamelisubiri kwa muda mrefu.
Katika droo ya raundi ya tano, ambayo imefanyika Jumapili, klabu ya daraja ya kwanza, Stevenage, kwa mara ya kwanza katika historia yake imekuwa miongoni mwa timu 16 zilizosalia katika mashindano hayo, na sasa itacheza na Tottenham.
Brighton itasafiri hadi uwanja wa Anfield kucheza na Liverpool, Chelsea nao ni wenyeji wa Birmingham, na Crawley Town, katika daraja ya pili, itacheza na Stoke.
Sunderland ikifuzu baada ya mechi ya marudiano, itapambana na Arsenal.
Norwich itacheza na Leicester, na Everton itaikaribisha Blackpool.
Bolton itacheza aidha na Millwall, au Southampton.