Theo Walcott
Kocha wa Arsenal Arsene Wenger , amekariri kuwa klabu hiyo
haina nia yoyote ya kumuuza mchezaji wake Theo Walcott, msimu wa usajili Januari
mwakani.
Kufuatia uamuzi huo, Arsenal, sasa huenda ikampoteza Walcott, mwenye umri wa miaka 23, ila kupokea chochote, kwa kuwa kandarasi ya mchezaji huyo inakamilika mwisho wa msimu huu.
Ikiwa Walcott na wasimamizi wa klabu hiyo hawataafikiana lolote, kabla ya wakati huo, Walcott atakuwa huru kuanzisha mazungumzo na klabu yoyote na kama vipi akasepa Emirates.
Mazungumzo kuhusu kandarasi mpya yamekwama, na alipoulizwa ikiwa klabu hiyo itamuuza mchezaji huyo ikiwa mazungumzo hayo yataendelea hadi mwaka ujao, Wenger, alikariri kuwa hana nia yoyote ya kumpoteza mmoja wa wachezaji wake wa kutegemewa.
Mwezi Agosti mwaka huu, Walcott alikataa kusaini mkataba mpya ambao angelipwa £75,000 kwa wiki na kusisitiza kuwa, hatma yake katika klabu hiyo itategemea ikiwa atapewa nafasi ya kucheza kama mmoja wa washambulizi.