Saturday, June 16, 2012

Photo of the DAY

EURO 2012 UINGEREZA YAITANDIKA SWEDEN


Mashabiki "viburudisho" wa Sweden

Danny Welbeck aliweza kutia kambani bao la ushindi la England dhidi ya Sweden, katika mechi ya kusisimua ya kundi D.

England iliweza kutangulia kwa bao la kwanza wakati Andy Caroll alipofunga kwa kichwa, baada ya kuletewa mpira wa juujuu na Steven Gerrard.

Lakini mlinzi Olof Mellberg aliweza kufunga bao la kusawazisha, na baadaye kupata la pili kwa kichwa na kuiwezesha Sweden kuongoza kwa mabao 2-1.

Andy Caroll akipiga ndosi iliyoelekea moja kwa moja kambani na kuandika bao la kwanza kwa Uingereza


Zlatan Ibrahimovic akijaribu kuonyesha cheche lakini yuko chini ya ulinzi wa Glen Johnson

Lescott akiwa chini ya Ulinzi

Theo Walcott "Handsomeboy" akishangilia bao

Mchezaji wa zamu Theo Walcott kupitia mkwaju kutoka yadi 25 aliiwezesha England kusawazisha, na kisha baadaye alipompigia mpira Welbeck, akafanikiwa kufunga bao la tatu na la ushindi, na kuhakikisha Sweden wanaelekea nyumbani baada ya kuwaondoa katika mashindano ya mwaka huu ya Euro 2012.

Huu ndio ushindi mkubwa zaidi wa England dhidi ya timu ya Sweden, na mara tu baada ya Carroll kuwawezesha kuongoza, England haikuona tena kitisho kikubwa mno cha kulemewa katika mechi hiyo ya Ijumaa.

Pengine onyo la nahodha Steven Gerrard kabla ya mechi katika kuhakikisha mshambulizi Zlatan Ibrahimovic asipate nafasi za kufunga labda ziliweza kuisaidia England kuepuka kushindwa.

Lakini kwa kumzuia Ibrahimovic, pengine ndio maana mchezaji mwenzake Melberg alipata bao la pili la Sweden kwa urahisi kwa kuwa England hawakumzuia kikamilifu.

Meneja wa England Roy Hodgson kisha aliamua kumtumia Walcott, na bila shaka mchezaji huyo alibadilisha mchezo.
SWEDEN  2-3  ENGLAND

UERO 2012 WENYEJI UKRAINE WALOA KWA UFARANSA MVUA KIDOGO IHARIBU SHUGHULI


Menez akishangilia baada ya kutupia goli la kwanza

Ufaransa ilipata ushindi wake wa kwanza katika kundi D katika mechi ya Ijumaa ya Euro 2012, baada ya kuwashinda wenyeji Ukraine katika uwanja ulioloa maji kufuatia mvua kubwa iliyotandika katika uwanja wa Donetsk.


Wingu limetanda

Mchezo ulisitishwa baada ya dakika nne tu, kufuatia uwanja kujaa maji, na timu zilirudi uwanjani baada ya saa nzima kupita.
Lakini waliporudi, kulikuwa hakuna njia nyingine ya kuiokoa Ukraine, kuanzia wakati Jeremy Menez, mchezaji wa St Germain ya Ufaransa, alipowaongoza Wafaransa katika kufunga mabao, akitupia mpira kambani kutoka yadi 12.

Yohan Cabaye alitupia kambani bao la pili na hilo lilikuwa ni bao la kwanza katika mechi ya kimataifa kwa mchezaji huyo wa klabu ya Newcastle inayocheza katika ligi kuu ya England.

Bao hilo lilipatikana kwa urahisi kufuatia kosa la wachezaji wa ulinzi wa Ukraine namna walivyocheza katika uwanja huo wa Donbass Arena.

Wachezaji wa timu zote walikuwa na kibarua kigumu katika kucheza katika hali ya joto kali na uwanja ulioloa, na ndio maana mwamuzi Bjorn Kuipers kutoka Uholanzi awali alikuwa ameamua kusitisha mechi hiyo.

Ilibidi juhudi za dharura kufanyika ili kuyafyonza maji hayo, na baadaye mwamuzi kuidhinisha mechi kuendelea.

Mvua imeanza kutandika goma linaendelea Nasri akimchachafya mlinzi wa Ukraine

Mvua inaendelea kutandika na mashabiki wabishi wamo

Hatoki mtu uwanjani mpaka kieleweke mtanange unaendelea


Oyoooo mpaka kielewekeeeee!!!

Radi inatandika kisawasawa

Asiekubali kushindwa si mshindani..hatimae mwamuzi alisimamisha mtanange baada ya mvua kuendelea kushuka na maji yakijaa dimbaniIsiwe taabu ngoja tukaisikilizie nje, mwamuzi na wachezaji wakitoka uwanjani kufuatia mvua kubwa kunyesha

Tukausheni maji jamani leo hapa hatoki mtu, wafanyakazi wa uwanja wakikausha maji baada ya mvua kukatika


Kocha wa Ukraine akitest je maji kweli yamekauka au!!?
Ukraine  0-2  Ufaransa

MWANAMAMA FATOU ARITHI MIKOBA YA OCAMPO MAHAKAMA YA KIMATAIFA YA UHALIFU WA KIVITA


Bi Fatou Bensouda

Luis Moreno Ocampo(kushoto) mwendesha mashtaka anaemaliza muda wake na Bi Fatou Bensouda (kulia)

Mwendesha Mashtaka Mkuu mpya wa Mahakama ya Kimataifa ya kukabiliana na Uhalifu wa Kivita ameapishwa mjini Hague hii leo.

Bi Fatou Bensouda, aliyekuwa Waziri wa Haki nchini Gambia,ndiye Mwafrika na pia mwanamke wa kwanza kushikilia wadhifa huo wa kuendesha mashtaka ya uhalifu wa kivita.
Mtihani wa kwanza kwa mwanamama Fatou ni kumleta Hague mtoto wa aliyekuwa kiongozi wa Libya, Kanali Muamar Gaddafi, Saif al-Islam Gadaffi, ambaye ameshtakiwa kwa makosa dhidi ya binadamu na wakati huohuo kuongoza mashtaka yanayomkabili aliyekuwa kiongozi wa Ivory Coast, Laurant Gbagbo.


Bi Bensouda akila kiapo kuitumikia mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita

Fatou Bensouda amechukua nafasi ya Luis Moreno Ocampo"Jembe", ambaye ameongoza mahakama hiyo kwa zaidi ya mwongo mmoja.

Kesi ya rais wa zamani wa Liberia, Charles Taylor, ilisikilizwa na mahakama ya Umoja wa mataifa inayosikiliza kesi za waliohusika na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini
Sierra Leone.


Bi Bensouda amekuwa akifanya kazi kama naibu wa Luis Moreno-Ocampo anayemaliza muda wake katika mahakama ya ICC huko The Hague.

Mwandishi wa BBC anasema kuwa licha ya kwamba Bi Bensouda sio mgeni kwa mambo ya Hague, uteuzi wake unakuja wakati mfumo wa sheria ya kimataifa unahojiwa sana.

Pia anachukua jukumu hilo wakati kuna mtafaruku katika mahakama hiyo huku maafisa wanne wa mahakama hiyo wakiwa wanazuiliwa nchini Libya.

Mwandishi wa BBC anasema kuwa Bi Bensouda anasifika kwa kuwa mtulivu kitu ambacho huenda kimemsaidia katika kazi yake.
Ikizingatiwa kuwa washukiwa wengi ambao kesi zao ziko katika mahakama ya ICC ni waafrika na hili limekosolewa huku ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu  ikisadikiwa kuwalenga zaidi waafrika.


Bi Bensouda akifuatilia jambo mahakamani huko The Hague

Bi Bensouda katika "swagga"

Inatarajiwa kwamba kwa kuwa Bi Bensouda mwenyewe ni Mwafrika tena wakili, huenda akasaidiwa na hili kunyamazisha wakosoaji wake, kulingana na wadadisi wa mambo.

Mwezi Machi mbabe wa kivita kutoka DRC, Thomas Lubanga alipokea hukumu ya kwanza ya kesi yake ikiwa hukumu ya kwanza kuwahi kutolewa na mahakama hiyo tangu kuundwa kwake miaka kumi iliyopita.

Kikosi cha viongozi wa mashtaka wanataka Lubanga atundikwe miaka 30 jela kwa makosa ya kutumia watoto kama wanajeshi wakati wa vita mashariki mwa DRC  kati ya mwaka 2002 na 2003.