Tuesday, July 24, 2012

ROBO FAINALI KAGAME CUP,HATUMWI MTOTO SOKONI SIMBA Vs AZAM


'Mwali" wa Kagame ambapo imefikia hatua ya robo fainali

Mabingwa wa Soka nchini, Simba na mabingwa wa Kombe la Mapinduzi, Azam FC leo zina fursa kupalilia kampeni ya kuongeza mataji kwenye makabati yao zitakapokutana katika mchezo wa robo fainali ya michuano ya Kombe la Kagame kwenye Uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.
Mbali na mechi hiyo inayotarajia kuwa na ushindani mkubwa, pia kutakuwa na mchezo mwingine wa robo fainali utakaozikitanisha Atletico ya Burundi dhidi ya Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mchezowa Simba na Azam ni kama fainali kwani zimekuwa zikikamiana kila zinapokutana, ambapo mara ya mwisho zilikutana fainali ya Kombe la Urafiki na Simba kushindwa kwa mikwaju ya penalti baada ya sare ya 2-2.
Lakini kabla ya hapo, Simba ilinyukwa mabao 2-0 kwenye michuano ya Kombe la Mpinduzi, kabla ya Wekundu hao wa Msimbazi kulipa kisasi kwa ushindi wa mabao 2-0 katika mechi ya marudiano ya Ligi Kuu.
Mechi ya leo inazikutanisha kwa mara ya nne, ambapo zitakutana tena katika mchezo wa Ngao ya Jamii mwishoni mwa mwezi ujao kama ishara ya mwanzo wa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara.
Azam inashiriki michuano ya Kombe la Kagame kwa mara ya kwanza na imepania kutaka kuweka rekodi ya kutwaa taji lingine baada ya lile la Mapinduzi.
Kocha Stewart Hall anajivunia kikosi chake kilichokuwa Kundi C la michuano hiyo pamoja na Mafunzo na Tusker ya Kenya.
Atamtegemea zaidi kipa mpya, Deogratius Munishi 'Dida'  ndiye atakayesimama langoni, huku Waziri Salum akirejea uwanjani kucheza beki wa kushoto na mchezaji bora nchini, Aggrey Morris atasimama katikati akishirikiana na Joseph Owino na Erasto Nyoni akicheza beki wa kulia.
Viungo watatu watakuwa ni Kipre Bolou, Salum Abubakar na Ramadhan Chombo Redondo, wakati mfungaji bora wa klabu John Bocco atasimama katika ushambuliaji akishirikiana na Kipre Tchetche na Mrisho Ngasa.
Kwa upande wa Simba ambayo makali yake katika safu ya ushambuliaji bado hayajaonekana tangu kuondoka kwa Emmanuel Okwi, itaendelea kumtegemea Felix Sunzu kupachika mabao.
Kocha Circovic Milovan, amekiri wazi kukosekana Okwi na kufariki kwa Patrick Mafisango, kumeacha pengo kubwa kwenye kikosi chake.
Simba ilianza vibaya michuano hiyo kwa kunyukwa 2-0 na URA ya Uganda kalba ya kuichapa Ports ya Djibouti mabao 3-1 na kulazimishwa sare ya 1-1 na Vita Club ya Kongo.
Majeruhi Shomari Kapombe na Amir Maftah wanampa presha Milovan na itabidi atumie muungano wa Haruna Shamte na Kiggi Makasi na nafasi ya Okwi akiiziba Abdallah Juma ambaye ni kinda aliyemfunika Felix Sunzu kutokana na kutumia vema nafasi hiyo.
"Kukosekana kwa ubunifu baada ya Okwi kuondoka ni ngumu kwetu, lakini Juma Abdallah anajitahidi kucheza vizuri ingawa bado haijaimudu vizuri.
"Nahitaji harakati mshambuliaji mmoja muhimu, nina uhakika wa asilimia 75 Okwi hawezi kurudi tena Simba," alisema Milovan.
Mechi nyingine itanayotarajia kuwa kali itazikutanisha Atletico na Vita Club ambazo zimeonyesha uwezo na kucheza kwa ufundi tangu kuanza kwa michuano hii.
Atletico imetinga robo fainali bila ya nyavu zake kutikiswa baada ya kuinyuka Yanga mabao 2-0 na kisha kwenda sare ya bila kufungana na APR, kabla ya kuinyuka Wau Salaam ya Sudan ya Kusini mabao 5-0 huku Vita ambayo inashiriki michuano hii kama wageni waalikwa walianza harakati zao kwa kuinyuka Ports ya Djibouti mabao 7-0 na kujikuta ikinyukwa mabao 3-1 na URA ya Uganda na kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Simba mwishoni mwa  wiki.