Wednesday, August 22, 2012

ADEBAYOR ATUA TOTTENHAM

Emmanuel Adebayor
Emmanuel Adebayor

Emmanuel Adebayor amekamilisha mipango ya kuhamia Tottenham Hotspur kutoka Manchester City kwa kitita cha pauni milioni 5.
Mshambulizi huyo kutoka Togo alionyesha umahiri wake msimu uliopita, akiichezea Tottenham kwa mkopo, kwa kufunga jumla ya magoli 17 katika ligi kuu ya Premier.

Adebayor atakuwa ni kati ya wachezaji wenye mishahara mikubwa katika klabu hiyo ya uwanja wa White Hart Lane.

Adebayor, mwenye umri wa miaka 28, alikuwa akilipwa na Manchester City pauni milioni 175,000 kwa wiki.

Mshambulizi huyo, ambaye zamani alikuwa akiichezea Arsenal, alifichua habari za kujiunga na Tottenham kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter: “Tottenham niko njiani! Natamani magoli. Kaeni chonjo.”

Mkataba wa Adebayor ulikuwa uendelee kwa miaka miwili zaidi na klabu ya Man City, na kwa kipindi kirefu katika misimu miwili iliyopita alikuwa akiichezea Real Madrid ya Uhispania, na kisha Tottenham.

“Ninafurahi kujiunga kabisa na Spurs baada ya klabu kuelewana na Manchester City,” aliongezea Adebayor.

“Pengine ilichukua muda mrefu kinyume na ilivyotazamiwa, lakini nimefurahi sana kurudi Tottenham Hotspur. Nilifurahi sana nilipokuwa hapa msimu uliopita, na ni matumaini yangu tutaweza kwa pamoja kufanikiwa hata zaidi.”

Inafahamika kwamba Spurs walikataa kubadilisha mipango yao ya mishahara ili kufanikisha mipango ya kumpata Adebayor.

Lakini kutokana na Adebayor kukataa kupunguziwa mshahara, mabingwa wa ligi kuu Manchester City walikubali kuongezea zaidi tofauti ya senti atakazopokea Adebayor katika klabu ya Tottenham, na kiwango alichozoea Man City cha pauni 175,000.

Tottenham watamlipa pauni 80,000 kwa wiki, na Man City ilibidi kukubali kuongezea tofauti ya elfu 95,000 kwa wiki, ili kuyafanikisha makubaliano kati ya vilabu hivyo viwili.

Makubaliano hayo yanahitimisha ubishi ulioendelea kwa muda mrefu, kuhusu ikiwa Adebayor alistahili kulipwa bakshishi na marupurupu mengineyo iwapo angelisisitiza kuondoka Man City pasipo makubaliano kamili kati yake na klabu hiyo.
Mavituz ya Adebayor