Monday, April 16, 2012

MAZISHI YA MUTHARIKA KUIGHARIMU MALAWI MILIONI 600 KUAGWA SIKU 10


Aliyekuwa Rais wa Malawi marehemu Bingu wa Mutharika

Serikali ya Malawi imetenga siku kumi kwa ajili ya wananchi wa Taifa hilo kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Bingu wa Mutharika.

Mwili wa kiongozi huyo unatarajiwa kuwasili leo jijini Lilongwe ukitokea katika hosipitali ya jeshi mjini Pretoria, Afrika Kusini na baadaye utapelekwa Ikulu ambako waombolezaji watapata fursa ya kuanza kutoa heshima za mwisho.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi ya Mutharika, Henry Mussa alisema kesho Jumapili mwili wa kiongozi huyo utaendelea kuwapo Ikulu na milango itakuwa wazi kwa wanafamilia na marafiki wa karibu kutoa heshima zao za mwisho na Jumatatu utawekwa katika jengo jipya la Bunge mjini Lilongwe ambako wananchi watapata fursa ya kutoa heshima hizo kwa siku mbili.

Mussa ambaye pia ni Waziri wa Serikali za Mitaa, alisema Jumatano mwili wa Mutharika utapelekwa katika mji wa Mzuzu ambako wananchi wa Kanda ya Kaskazini mwa Malawi pia watamuaga kiongozi wao, na Alhamisi mwili huo utasafirishwa kwenda Blantyre ambako utahifadhiwa Ikulu ya ndogo ya Sanjika.


Marehemu Mutharika kulia akiteta jambo na Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe enzi za uhai wake

Katika Ikulu hiyo wananchi watatoa heshima zao za mwisho kwa siku tatu hadi Jumamosi, April 21 kisha mwili huo kupelekwa katika eneo la maziko, shamba la Ndata, ambako wakazi wa eneo hilo pia watatoa heshima zao za mwisho, Jumapili Aprili 22.

Mussa alisema siku ya mazishi ambayo ni Jumatatu Aprili 23, 2012 watakaoruhusiwa kutoa heshima zao za mwisho ni wakuu wa nchi, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa na wale wa Jumuiya za Kikanda kabla ya Ibada itakayoongozwa na Kanisa Katoliki ambalo Mutharika alikuwa muumini wake.

Juzi, Ikulu ya Lilongwe ilithibitisha kwamba Rais Jakaya Kikwete ni miongoni mwa wakuu wa nchi na Serikali ambao wamealikwa kushiriki mazishi ya kiongozi huyo ambaye alifariki Aprili 5, mwaka huu kutokana na ugonjwa wa moyo.

Mutharika atazikwa katika shamba la Ndata katika Wilaya ya Thyolo iliyoko umbali wa Kilometa 45 Kusini mwa Blantyre, uamuzi ambao Mussa alisema ulitokana na maelekezo yake aliyoyatoa kabla hajafariki dunia.

“Kwa wale ambao tumewahi kufika Ndata alipozikwa mke wake Ether, aliweka sehemu ambayo pia angependa azikwe yeye, kwahiyo sisi ni akina nani hadi tupinge uamuzi wake?” alisema Mussa.

Mazishi kugharimu Sh600 milioni
Katika hatua nyingine Mussa alisema Serikali ya Malawi imechukua hatua za kuhakikisha kwamba hakutakuwa na uhaba wa mafuta wakati wote wa taratibu za mazishi ya Mutharika, ambayo yataigharimu nchi hiyo Kwacha150 milioni (zaidi ya Sh600 milioni).

Waziri wa Fedha wa Malawi juzi aliwasilisha bajeti ya Kwacha400 milioni (zaidi ya Sh1.6 bilioni) mbele ya kikao cha Baraza la Mawaziri lakini kikao hicho kilichokutana na chini ya Uenyekiti wa Rais Joyce Banda kikaipunguza hadi kufikia kwacha150 milioni.

Mussa alisema mbali na msaada wa lita milioni tano za mafuta ambazo Malawi imepokea kutoka Serikali ya Zambia, kiasi kingine cha lita milioni 20 kinatarajiwa kuingia mapema iwezekanavyo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba shughuli za Serikali hazikwami.


Mwenyekiti wa kamati ya mazishi Henry Mussa ambaye pia ni Waziri wa serikali za mitaa

“Shehena ya mafuta inaingia sasa kupitia sehemu mbalimbali, katika Bandari ya Dar es Salaam (Tanzania) na Beira, pia kule Nakala na tunataraji kwamba mafuta haya yatatumika kuhakikisha shughuli za mazishi ya Rais wetu hazikwami,” alisema Mussa.

Jana Malawi ilipokea rasmi mafuta ya msaada yaliyotolewa na Zambia kupitia kwa Rais wa nchi hiyo Michael Satan yalikabidhiwa na Waziri mwenye dhamana ya Nishati nchi hiyo, Christopher Yalima kwa Rais Banda.

Uhaba wa mafuta nchini Malawi ulianza kujitokeza miaka mitatu iliyopita lakini hali inaelezwa kuwa mbaya zaidi yapata miezi miwili iliyopita, kiasi cha kusababisha bei za bidhaa kupanda hivyo kuongeza ugumu wa maisha kwa Wamalawi.
Maombolezo Ikulu
Wananchi wa Malawi wameendelea kuingia Ikulu ya Malawi kwa ajili ya maombolezo ya Mutharika pia kuwafariji wafiwa katika msiba huo.

Habari kutoka Blantyre pia zinasema maombolezo kama hayo yanaendelea katika shamba la Mutharika la Ndata ambalo pia lilifunguliwa kwa ajili ya kuwaruhusu wananchi kuhani msiba wa kiongozi wao.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais wa Malawi, Khumbo Kachali aliapishwa jana na Jaji Mkuu wa nchi hiyo, Lovemore Munlo katika hafla iliyohudhuriwa na Rais Banda na mamia ya wafuasi wa chama kipya cha Peoples Party (PP).

ZUMA KUOA MKE WA SITA WIKI HII


Rais wa Afrika ya Kusini Jacob Zuma

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini ametangaza kwamba atafunga ndoa ya sita wiki hii.
Rais huyo mwenye umri wa miaka 70, atamuoa mchumba ake kwenye harusi ya kijadi huko Kwa Zulu Natal.
Gloria Bongekile Ngema, mfanya biashara kutoka Durban, ameshaonekana mara nyingi akifuatana na rais lakini kutoka juma lijalo, wawili hao watakuwa wameowana rasmi kijadi.
Harusi inatarajiwa kuwa ya fahari lakini ya faragha katika kijiji cha Nkandla, katika jimbo la Kwa Zulu Natal, nyumbani kwao Rais Zuma.

Zuma na mkewe wake mtarajiwa, Bi Gloria Bongekile Ngema

Rais Zuma ni mtu anayefuata mila za kabila lake la Zulu.
Mwenyewe amezaliwa na baba aliyekuwa na wake kadha.
Na ndoa yake kwa Bi Ngema ni ya sita, ingawa kutoka juma lijalo atakuwa na wake wane tu.
Mmoja, ambaye ni waziri wa serikali, alimuacha.
Na mwengine alijiiuwa.
Nyumba ya Rais Zuma imetengenezwa sana ili kuweza kuweka familia yake.
Inafikiriwa ana watoto 20.
Lakini hivi karibuni alisema ndoa ya juma lijalo ndio itakuwa ya mwisho.

MAN U YAIFUMUA ASTON VILLA 4-0, CHELSEA YAIZABUA SPURS 5-1

Chelsea thrash Spurs to reach FA Cup final
Drogba na wachezaji wenzake wakishangilia goli

Chelsea iliwachapa Tottenham mabao 5-1 nakuingia katika fainali za kombe la FA ambapo watakutana na Liverpool.
Hata hivyo ushindi huyo haukukosa manung'uniko baada ya refa kuipa Chelsea goli ambalo ilidaiwa kuwa mpira ulikuwa haujavuja mstari wa goli.
Utata huo sasa umeibua mjada kwamba kuna haja ya kuanzishwa mara moja kwa utaalam wa kuangalia kama mpira umevuka mstari wa goli au la.

Goooooooooooooooal!!!

Ushindi huo mnono umempa raha mkufunzi wa Chelsea Roberto di Matteo kwani umeiweka katika hali nzuri ya kupambana na Barcelona watakapowatembelea siku ya Jumatano.
Wakati Chelsea wakifurahia ushindi wao Spurs walikua na malalamiko chungu nzima kwani walidai kuwa walikuwa wanaonewa pale mpuliza kipenga ,Martin Atkinson alipowapa Chelsea bao la utata.

MAN UNITED YAUA

Manchester United imeongeza wigo wa pointi hadi tano dhidi ya Manchester City kileleni mwa Ligi Kuu ya Kandanda ya England lakin i ushindi wao dhidi ya Aston Villa uligubikwa kwa mara nyingine na penalti iliyoonekana ni ya utata.

Wayne Rooney - Manchester United v Aston Villa - Premier League
Rooney akitupia kambani kwa mkwaju wa penati

Ashley Young, ambaye alifanikiwa kupata penalti wakati Manchester United walipocheza na QPR, kwa mara nyingine alifanikiwa kupata penalti baada ya kutegewa na Ciaran Clark.
Kuguswa huko kwa Young kulikuwa kudogo sana lakini Wayne Rooney alifanikiwa kufunga mkwaju huo wa penalti kabla Danny Welbeck kuipatia Manchester United bao la pili.
Villa iliimarika kidogo baada ya kipindi cha pili lakini walikuwa Rooney na Nani walioandika mabao mengine mawili yaliyohitimisha karamu ya mabao 4-0.
Wayne Rooney - Manchester United v Aston Villa - Premier League
Rooney katikati na Young mgongoni pamoja na Carrick wakishangilia goli la Rooney

Manchester United walionekana kikosi bora zaidi katika kipindi cha kwanza na ushindi huo umepunguza pia deni la mabao ya kufunga na Manchester City na sasa kuwa manne.
Lakini bado swali litaendelea kubakia kwa wapenzi wa kandanda juu ya Young anavyojiangusha na aliposhutumiwa alipofanya hivyo dhidi ya QPR, ambapo Shaun Derry aliadhibiwa kwa kumsukuma mshambuliaji huyo wa pembeni na alioneshwa kadi nyekundu.
Rufaa iliyokatwa na Rangers ilitupiliwa mbali na Chama cha Kandanda cha England na shutuma zitaendelea kumuandama Young kutokana na alivyofanya kwa mara nyingine.
Na kubwa zaidi Young alifanya hivyo kwa timu aliyowahi kuichezea na itaongeza zaidi chumvi kwenye jeraha kwa timu ya Aston Villa.
Wayne Rooney - Manchester United v Aston Villa - Premier League
Rooney akishangilia bao

Villa walishindwa kuivunja rekodi dhidi yao wanapopambana na Manchester United, ambapo wamewahi kushinda mara moja tu katika mechi 31.
Jambo muhimu ni kwamba wapo pointi sita juu ya msatari wa kuteremka daraja na sasa wanajiandaa kwa pambano dhidi ya Sunderland, Bolton na West Brom ambapo lazima watafute pointi kujihakikishia hawateremki daraja.