Monday, March 30, 2015

WANYAMA KUTUA ARSENAL


Wanyama akimtoka Kisly wa Swasea katika mchezo wa Ligi kuu Uingereza

Kocha wa Arsenal Arsene Wenger anapanga kumnunua kiungo wa kati wa Southampton Mkenya Victor Wanyama na mshambuliaji wa Anderlecht Aleksandr Mitrovic kulingana na gazeti la the Sun nchini Uingereza.
Wenger amejiandaa kutoa kitita cha pauni millioni 30 kwa wachezaji hao wawili,huku Wanyama akigharimu kitita cha pauni millioni 20 naye mshambuliaji huyo wa Anderlecht Mitrovic akigharimu pauni millioni 10.
Inaaminika kuwa Wanyama ataondoka katika kilabu ya Southampton iwapo atachukuliwa na kilabu kikubwa huku naye Mitrovic akiwa amekuwa akifuatiliwa na waajiri wa Arsenal katika kipindi cha wiki chache zilizopotea.
Mitrovic amekuwa akifananishwa na Didier Drogba kutokana na mchezo wake.


Victor Wanyama

WASAMBAZA PICHA ZA NGONO KUCHEZEA NYUNDO SABA JELA

 Leo, Serikali itawasilisha bungeni muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao wa mwaka 2015 kwa hati ya dharura unaoorodhesha adhabu mbalimbali, ikiwamo ya faini ya Sh50 milioni au kifungo kisichopungua miaka saba kwa mtu atakayebainika kusambaza picha za ngono mtandaoni.


Baadhi ya makosa yaliyoanishwa katika sheria hiyo  ni kutuma taarifa bila ridhaa ya mtu, kusambaza picha za ngono na za utupu, udanganyifu unaohusiana na kompyuta, makosa yanayohusiana na utambuzi, kughushi kunakohusiana na masuala ya kompyuta na kusambaza picha za utupu za watoto.
Mengine ni unyanyasaji kwa kutumia mtandao, kuchapisha taarifa yoyote ambayo itasababisha mauaji ya kimbari, uongo na matusi ya kibaguzi.
Sheria hiyo katika Kifungu cha 48 inaipa Mahakama mamlaka ya kutaifisha mali iliyopatikana kutokana na kosa lililofanywa na mhusika. Sheria hiyo pia itawataka wote watakaobainika kufanya makosa hayo kuwasilisha hati zao za kusafiria kwa mamlaka husika hadi hapo watakapolipa faini au watakapokuwa wamemaliza kutumikia vifungo.


Muswada huo ambao ukipitishwa utakuwa sheria, unawasilishwa bungeni katika kipindi ambacho kina matukio mengi ya watu kusambaza picha za ngono na utupu mitandaoni, kuingilia mawasiliano ya kompyuta ya watu wengine bila ridhaa yao.
Pia, kifungu hicho kinaeleza kuwa mtu atakayebainika kusambaza picha za ngono, uasherati na matusi, atatozwa faini isiyopungua Sh30 milioni au kwenda jela miaka 10, mtu atakayesambaza picha za utupu atalipa faini isiyopungua Sh20 milioni au kwenda jela miaka saba.
Inawabana pia watoa taarifa za uongo. Katika Kifungu cha 16, inasema mtu atakayetoa taarifa, takwimu au maelezo kwa njia ya picha au maandishi au aina nyingine yoyote zikiwa ni za uongo, akipatikana na hatia atalipa faini isiyopungua Sh3 milioni au kifungo kisichopungua miezi sita.
Kuhusu mauaji ya kimbari, inakataza mtu kuchapisha au kusababisha kuchapisha vitu vinavyochochea au kuhalalisha matendo yanayosababisha mauaji ya kimbari na adhabu yake ni faini ya Sh10 milioni au miaka mitatu jela .