Tuesday, April 24, 2012

HAKUNA SIMBA INOGILE KAMA INO, YAICHAPA MORO UNITED 3-0, MTIBWA YATIA MPIRA KWAPANI


Beki wa Moro United Eric Mawala akiwa makini kuzuia mashambulizi ya Okwi

Simba sports Club, imeendelea kutakata kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya jana kuigaragaza Moro United mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, huku mchezo mwingine wa ligi hiyo kati ya Azam na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Chamazi kuvunjika dakika 88 matokeo yakiwa sare ya 1-1.

Wawakilishi hao wa Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, sasa wamefikisha pointi 59 akiwa na mechi moja mkononi dhidi ya Yanga wenye ndoto ya kupata nafasi ya pili kama watashinda kesho dhidi ya JKT Olojro na kuomba Azam ipoteze michezo yake iliyosalia.

Vinara hao iliwachukua dakika 10 kupata bao kwanza lililotiwa kambani kwa mkwaju wa penalti na Mafisango, Haruna Moshi kutupia bao la pili dakika 33 na Felix Sunzu alipigilia msumari wa mwisho dakika ya 74.

Ushindi huo unaiweka Simba kwenye mazingira mazuri kabla ya mechi yake ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Al Alhy Shendi.

Chamazi, Mwamuzi Rashid Msangi alilazimika kumaliza mchezo dakika ya 88, baada ya wachezaji Mtibwa Sugar kugomea penalti katika mchezo ulioshuhudia ubabe mwingi.

Dakika tatu kabla ya filimbi ya mwisho mwamuzi Msangi alilazimika kumaliza pambano baada ya wachezaji wa Mtibwa Sugar kutoka uwanjani wakigomea penalti.

Beki wa Mtibwa Juma Abuu aliunawa mpira kwenye eneo la hatari wakati akijaribu kuokoa na mwamuzi kuamua adhabu hiyo, ndipo wachezaji wa Mtibwa walipomzonga kupiga uamuzi huo.

Wenyeji Azam walipata bao la mapema bao la dakika ya kwanza kupitia kwa mshambuliaji Mrisho Ngasa baada ya kuingia ndani ya 18 na kumlamba chenga kipa wa Mtibwa Sugar, Deogratius Mushi 'Dida'.

Vijana wa Manungu walisawazisha bao hilo dakika 18, kwa mpira wa adhabu uliopigwa na beki mkongwe Salum Swed na kwenda moja kwa moja wavuni.

Katika kipindi cha kwanza Mtibwa Sugar walionekana kucheza kibabe na kutembeza viatu kwa wachezaji wa Azam na kusababisha mwamuzi Msangi kutoa kadi za njano kwa Swed, Hassan Ramadhan na Hussen Javu waliomchezea vibaya John Boko na Ngasa dakika 27,30 na 35, huku Said Bahamuzi akipewa kadi ya njano kwa kupiga mpira nje wakati filimbi imeshapigwa.

Mwamuzi Msangi alitoa kadi ya pili ya njano na nyekundu kwa Bahamuzi aliyemchezea vibaya Salum Abubakari.

Awadhi Issa alifungia Mtibwa Sugar bao dakika 63, lakini mwamuzi alikataa kwa madai alishapulizi filimbi ya kuotea kabla ya mfungaji kupiga mpira huo.

Kwenye Uwanja wa Taifa, Furaha ya mashabiki wa Simba ilifutika ghafla baada ya kusikia mchezo kati ya Azam na Mtibwa Sugar umevunjika.

Simba ilifanya kile kilichosubiriwa na wengie kwa kuichakaza Moro United kwa kupata bao la kwanza dakika 10 kwa mkwaju wa penalti iliyopigwa na Mafisango baada ya beki wa Moro United, Omary Gae kunawa mpira ndani ya eneo la hatari.

Vinara hao walitawala zaidi sehemu ya kiungo na kufanya mashambulizi mengi langoni kwa Moro United iliyoingia uwanjani ikiwa na wachezaji wanne wanaolipwa mshahara na Simba waliowachukua kwa mkopo ni beki Meshack Abel, Salum Kanoni, Godfrey Wambura na Kelvin Charles.

Kiungo Haruna Moshi alifunga bao la pili kwa Simba katika dakika ya 33 akiunganisha vizuri krosi ya Uhuru Seleman.

Mshambuliaji Emmanuel Okwi alipoteza nafasi nzuri ya kuifungia Simba bao la tatu kwa kushindwa kumalizia kwa umakini krosi ya Uhuru katika dakika ya 36.

Moro walijibu mapigo dakika moja kabla ya mapumziko kwa shuti la beki Erick Mawala kugonga mwamba wa juu, lakini kipa Juma Kaseja alikuwa makini na kuwahi kudaka.

Kocha wa Simba, Milovan Cirkovic aliwapumisha Shomari Kapombe, Gervais Kago na kuwaingiza Nasoro Masoud na Felix Sunzu, wakati Moro Utd alitoka Benedict Ngasa na kuingia Simon Msava.

Mabadiliko hayo yalikuwa na faida kwa Moro waliorudi mchezoni na kufanya mashambulizi mengi, lakini wakajisahau na kutoa nafasi kwa Sunzu kufunga bao la tatu dakika 74 akiunganisha krosi ya Okwi.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda jana aliipongeza Simba kwa kufanikiwa kuingia raundi ya tatu ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Akiongea bungeni, Pinda alisema hatua waliyofika Simba kwenye michuano hiyo wanahitaji pongezi na ameomba wapenda michezo kuisapoti.

ROBIN VAN PERSIE "RVP" ANYAKUA TUZO YA MCHEZAJI BORA WA MWAKA

Robin van Persie mchezaji bora wa mwaka
Robin Van Persie

Robin van Persie amechaguliwa mchezaji bora wa mwaka katika tuzo inayotolewa na Chama cha Wacheza Kandanda ya Kulipwa- PFA.
Mshambuliaji huyo wa Arsenal mwenye umri wa miakan 28 ameshapachika mabao mara 38 msimu huu, yakiwemo mabao 34 aliyoifungia Arsenal katika mashindano yote.


Van Persie shughuli yake awapo uwanjani

Mchezaji huyo ambaye pia huchezea timu ya taifa ya Uholanzi, akiwa anaongoza kwa kufunga mabao msimu huu wa ligi ya England alisema: "Iwapo watu wanasema hivyo, ni jambo maalum sana, lakini linakuwa maalum zaidi iwapo hata wapinzani wako wanalizungumza.

"Iwapo wamekusanya mawazo yao na kukiri mimi ni mchezaji bora basi ni heshima kubwa hiyo."

Van Persie, ambaye amekuwa kichocheo cha ushindi kwa kikosi cha Arsene Wenger, haraka alielezea umuhimu wa wachezaji wenzake wa Arsenal.

"Bila ya wao nisingefikia mafanikio yote haya," alisema. "Mathalan, Theo Walcott, amenipatia zaidi ya pasi 12 na kwa kweli namshukuru sana.
Van Persie msimu huu mambo yake yamekuwa safi tangu alipojiunga na Arsenal mwaka 2004, akiwa ameisaidia kwa kiasi kikubwa safu ya ushambuliaji wa kati."Kusema haki, mara ya kwanza nilipojiunga na Arsenal sikuwa najiamini na sikuwa na hakika kama nitafanya mambo makubwa," aliongeza kusema.

"Ilinichukua muda kiasi lakini baada ya miezi michache polepole nikaanza kujiamini kwamba naweza kufanya kazi nzuri ndani ya Arsenal."

Van Persie ameshinda tuzo hiyo akiwatangulia Wayne Rooney wa Manchester United, Scott Parker wa Tottenham na wachezaji watatu wa Manchester City Sergio Aguero, Joe Hart na David Silva.

Mlinzi wa Tottenham na timu ya taifa ya England Kyle Walker ameshinda tuzo ya PFA ya mchezaji bora Kijana wa Mwaka.

Manchester City ndio ilikuwa na wachezaji wengi waliowania tuzo hiyo ya mwaka. Walifanikiwa kuwa na wachezaji wanne - Joe Hart, Vincent Kompany, David Silva na Yaya Toure

EVERTON YAIBANA MBAVU MAN UNITED


Nani akipigilia msumari huku kipa wa Everton akichumpachumpa bila mafanikio

Matumaini ya Manchester United kunyakua taji la ubingwa wa Ligi ya Kandanda ya England yalitiwa doa wakati Everton ilipopigana kiume wakiwa nyuma ya mabao 4-2 na kumaliza mchezo kwa sare ya mabao 4-4 katika mpambano wa kusisimua hasa dakika za mwisho kwenye uwanja wa Old Trafford.
Wayne Rooney aliisawazishia Manchester United baada ya kuunganisha kwa kichwa pasi kutoka kwa Nani baada ya bao la kuongoza la Everton lililofungwa kwa na Nikica Jelavi.


Rooney akitupia kambani katika mechi hiyo

Danny Welbeck na Nani waliipatia Manchester United mabao mawili kabla Marouane Fellaini kufunga bao moja jingine kwa Everton.

Rooney alionekana kuipatia ushindi Man United alipopachika bao la nne na muda mfupi baadae Everton wakacharuka na kupachika mabao mawili katika muda wa dakika tatu kupitia kwa Jelavic na Steven Pienaar.


Fellaini akipiga kichwa mbele ya Ferdinand na kuipatia bao la kusawazisha Everton

Katika dakika za mwisho, Patrice Evra alipiga mpira wa kichwa uliogonga mlingoti wa lango la Everton akiwa karibu kabisa na baadae mlinda mlango wa Everton Tim Howard aliokoa kwa ustadi mkubwa mkwaju wa Rio Ferdinand na kuinyima ushindi Manchester United.

Manchester United hata hivyo bado wanaongoza Ligi Kuu ya England wakiwa na pointi 83.

Dah hawa watoto vipi wametumwa?

MAWAKILI SITA WANAMTETEA LULU ,YUMO MSHINDI WA TUZO YA MWANAMKE JASIRI YA MARTIN LUTHER KING


LULU
Msanii  wa filamu za Bongo movies, Elizabeth Michael Kimemeta maarufu kama Lulu, jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu huku akibubujikwa machozi kiasi cha kumfanya Hakimu Ritha Tarimo ambembeleze ili kumnyamazisha. Lulu anashtakiwa mahakamani hapo kwa kutuhuma za kumuua msanii mwenzake, Steven Kanumba na alifikishwa jana kwa mara ya pili akiwa chini ya ulinzi mkali wa askari Magereza na Polisi.

Lulu alifikishwa mahakamani hapo saa 3:06 asubuhi akiwa katika basi dogo la Magereza pamoja na mahabusu wengine wanawake ambalo lilikuwa likisindikizwa na magari mengine mawili na alikuwa chini ya ulinzi wa askari sita wa kike wa Magereza na askari mmoja wa kike wa Polisi wakishirikiana na askari wa kiume wa Magereza zaidi ya sita.Lulu (mwenye kiremba) akisindikizwa na askari kuingia mahakamani huku machozi yakimmwagika

Mara baada kuingia katika chumba cha Mahakama, Lulu ambaye alikuwa amevalia dira jekundu alianza kulia kwa uchungu hali ambayo ilimlazimu Hakimu Tarimo pamoja na baadhi ya askari kumnyamazisha.
Kutokana na kujaa kwa watu mahakamani hapo, askari wa Kikosi Maalumu cha Magereza walilazimika kuufunga mlango wa Mahakama hiyo ili kesi hiyo isikilizwe.

Baada ya kesi hiyo kutajwa, Wakili Mwandamizi wa Serikali Elizabeth Kaganda aliiomba Mahakama iamuru watu wote watoke nje kwa sababu walikuwa wamefunga njia ili mtuhumiwa huyo aweze kupitishwa.

Hakimu Tarimo alikubaliana na ombi hilo na kuwaamuru askari kusafisha njia ili waweze kumpitisha msanii huyo kwa kile alichosema kuwa Lulu bado ni mtuhumiwa na anaweza kuumizwa.
“Askari safisheni njia ili mtuhumiwa aweze kupita kwa sababu yeye bado ni mtuhumiwa anaweza kuumizwa,"alisema Hakimu Tarimo.

Baada ya kutolewa kwa amri hiyo, askari walitimiza wajibu wao na muda mfupi njia ilipatikana na msanii huyo kutolewa mahakamani hapo.

Jopo la mawakili
Katika kesi hiyo, Lulu anatetewa na jopo hilo la mawakili akiwemo Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG), Joaquine De- Melo, Kenedy Fungamtama, Peter Kibatala na Fulgence Massawe.

De- Melo pia aliwahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS) na mshindi wa Tuzo ya Mwanamke Jasiri Tanzania ya Martin Luther King.

Fungamtama ambaye ndiye kiongozi wa jopo la mawakili hao wanaomtetea Lulu, anakumbukwa kwa kuitetea kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans, katika kesi dhidi ya Tanesco, ambayo alishinda na shirika hilo kuamriwa kuilipa kampuni hiyo zaidi ya Sh94 bilioni kwa kuvunja mkataba.
Kibatala ambaye pia anamtetea kada wa Chadema, Fred Mpendazoe katika kesi ya uchaguzi Jimbo la Segerea, pia ni Makamu wa Rais wa TLS, wakati Massawe anatoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Mawakili hao walijitokeza jana mbele ya Hakimu Tarimo tayari kumtetea Lulu na baada ya mawakili hao kujitambulisha, Wakili Kaganda alisema upelelezi wa kesi bado haujakamilika na kuiomba Mahakama iipangie tarehe nyingine.

Hakimu Tarimo aliiahirisha kesi hiyo hadi Mei 7, mwaka huu itakapofikishwa mbele ya Mahakama hiyo kwa ajili ya kutajwa.

Kwa mara ya kwanza Lulu alifikishwa mahakamani hapo Aprili 10, mwaka huu mbele ya Hakimu Mkazi, Augustina Mmbando akikabiliwa na la shtaka hilo la mauaji.

Wakili Kaganda alimsomea hati ya mashtaka alidai kuwa Aprili 7, mwaka huu katika maeneo ya Sinza Vatican, Wilaya ya Kinondoni, mtuhumiwa alimuua Kanumba. Kanumba alifariki dunia siku hiyo saa 9:00 usiku kwa kile kilichodaiwa kuwa ni baada ya ugomvi baina yake na Lulu