Tuesday, November 29, 2011

SIMBA MABINGWA VIJANA
Vijana Simba wakishangilia ushindi

KILA mwaka hufanyika mashindano ya soka kwa timu za vijana chini ya miaka 20, lengo hasa likiwa kuibua vipaji na kuvikuza.
Programu hiyo ilibuniwa na Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, kwa nia nzuri kabisa ya kuwajengea misingi bora wachezaji tangu wakiwa na umri mdogo ili baadae taifa lipate wanandinga makini kuunda timu ya taifa.
Hata hivyo, programu hiyo imeonekana kuzaa matunda baada ya kuibua wacheza wengi ambao wamepandishwa kuzichezea timu za wakubwa.
Baadhi ya klabu za Ligi Kuu, zimetangaza kuwapandisha chipukizi hao kwenye timu za wakubwa ili waweze kupata uzoefu na kukomaa kimashindano.
Ni msimu wa nne michuano hiyo inafanyika, lakini bado ni klabu chache zimeonyesha utayari kupokea wito huo pasipo kuelewa faida yake.
Mwaka huu zilishiriki timu 15 kutokana na ile ya Taifa kwa vijana U-17, Serengeti Boys kuongezwa kwa ajili ya kupata uzoefu wa mashindano.
Simba ambayo imeonyesha umakini na programu hiyo ya kukuza na kulea vipaji, ilitwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa mara ya pili tangu mashindano hayo yaanzishwe mwaka 2007.
Iliifunga Azam FC kwa mikwaju ya penalti 6-5, katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Karume Jumamosi iliyopita.
Kutokana na ushindi huo, ilijinyakulia kitita cha Sh1.5mil na Kikombe na kuvalishwa Medali za Dhahabu kama zawadi za bingwa wa michuano hiyo. Wakati Azam FC ikitwaa nafasi ya pili nakupatia Sh.1mil na Medali za Shaba.
Timu ya soka, Taifa Vijana U-17, Serengeti Boys ilishika nafasi ya tatu na kujitalia Sh500,000 na medali za fedha kwa kila mchezaji.
Mchezaji bora wa mashindano hayo alikuwa ni Ramadhan Singano wa Simba aliyejinyakulia kitita cha Sh400,000. Kipa bora ni Faishi Manula wa Azam aliyepata Sh300,000.
Mfungaji bora wa michuano hiyo alikuwa Simon Msuva wa Azam aliyepachika mabao sita na kujipatia Sh300,000.
Timu ambazo zilizoshiriki michuano hiyo ni Simba, Yanga, Azam, Mtibwa, Kagera, African Lyon, Toto African, Moro United, Polisi Tanzania, JKT Ruvu, Villa Squad, JKT Oljoro, Coastal Union, timu ya Taifa ya vijana U-17, Serengeti Boys na bingwa wa mwaka jana Ruvu Shooting.
Hata hivyo, wachezaji wa timu zote walilalamikia ratiba ya michuano hiyo kwa kucheza mechi tatu kwa siku ikiwa asubuhi, mchana na jioni.
Kwamba ratiba ilikuwa ya mechi za mfululizo na hakukuwa na sababu ya kucheza kufanya hivyo kwa kuwa muda ungalipo wa kuendesha mashindano hayo.
Vilevile kasoro nyingine ni viwanja uzoefu wa kucheza kwenye jua kali la nyasi bandia, ambazo watoto wengi walikuwa wakipata shida. Ni vema mechi hizo kuchezwa asubuhi ama jioni.
Tatizo lingine lililojitokeza ni kukosekana kwa huduma ya kwanza iliyosahihi. Ilibidi daktari wa Simba, Cosmas Kapinga kufanya kazi ya kuuguza wachezaji walioumia badala ya TFF ama wahusika kuwapatia huduma ya kwanza. Hata gari la wagonjwa kwa mchezaji ambaye angepata dharura halikuwepo.
Spoti Mikiki ilifanya mahojiano na makamu mwenyekiti wa Simba, Godfrey Nyange kutoa tadhmini ya michuano hiyo. Anasema hakika mashindano hayo yamepoteza uelekeo kutokana na klabu kuleta wachezaji ambao wamezidi umri ambao unatakiwa.
Ukweli ni kwamba michuano hayo imepoteza uhalisia wake, klabu zimekiuka taratibu na kuleta wachezaji ambao wamepita umri ambao unatakiwa. Nafikiri kufanya hivyo si kuikomoi TFF bali tunaiweka timu yetu ya Taifa kwenye mazingira magumu,
Naye kocha wa Small Kids ya Rukwa, John Willium Del Piero alisema mashindano hayo yameonyesha mafanikio makubwa kutengeneza wachezaji isipokuwa anashauri kuendeshwa sawa na Ligi Kuu.
Timu 15 kucheza ligi kwa majuma mawili ni sawa na bonanza, nafikiri haitoi fursa nzuri kwa vijana hao kuonyesha vipaji vyao,
Nafikiri TFF wakitafuta wadhamini zaidi kwa mashindano haya, ni wazi mambo yatakuwa mazuri, kwani ushindani utaongezeka.