Monday, November 14, 2011

Bunge Sports kushiriki mashindano ya mabunge ya Afrika mashariki Bujumbura

TIMU ya soka ya Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeingia kambini mjini Dodoma kujiandaa na michuano ya wabunge wa mabunge ya Afrika Mashariki, michuano itakayofanyika, Bujumbura, Burundi kuanzia Novemba 20.

Kocha wa timu hiyo, Kassim Majaliwa alisema kuwa kikosi chake kitaondoka Dodoma Novemba 19 kikiwa na wachezaji 25.Aliwataja wachezaji watakaoandamana na timu hiyo kuwa ni Amos Makala, William Ngeleja, Kighoma Malima, Sadifa Juma, Masauni Masauni, Erasto Zambi, Juma Nkamia na Steven Ngonyani.

Wachezaji wengine wanaounda timu hiyo ni; Haeshi Khalfan, Muiguru Mchemba, Ali Kingwangwala, Abdul Mteketa, Ngwali Juma, Victor Kawawa, Fakhi Haji Fakhi, Mahamoud Mgimwa, Chris Kimnyonyele na Job Lusinde.

Majaliwa ambaye ni Naibu Waziri wa Tamisemi aliwataja wengine kuwa ni Mambi Mumbala, Mark Kilumbi, Kassim Fundi na Michael Kadebe wakati daktari ni Kassim Ramadhani na Cesilia Sanya.

Mashindano hayo yatashirikisha nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Tanzania na wenyeji Burundi. Mwaka jana yalifanyika Arusha na Tanzania ilitwaa ubingwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Prof. Maji Marefu alisema maandalizi yanakwenda vizuri na timu yake iko vizuri kutetea ubingwa.

Stars yaifunga Chad 2-1

Mbinu ya kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Jan Poulsen ya kushambulia mwanzo mwisho katika mechi dhidi ya Chad, ilizaa matunda jana baada ya kuibuka na ushindi wa kwanza ugenini wa mabao 2-1 mechi ya kuwania nafasi ya kucheza hatua ya makundi fainali za Kombe la Dunia, shukrani kwa Nurdin Bakari aliyefunga bao la ushindi kwenye mechi hiyo.
Nurdin aliyeingia toka benchi, alifunga bao hilo katika dakika ya 85 akimaliza pasi nzuri ya Thomas Ulimwengu na kuwanyamazisha mashabiki wa Chad waliojazana kwenye Uwanja wa Idriss Mahamat.Huu ni ushindi wa kwanza ugenini wa kocha Poulsen tangu aanze kuifundisha Stars akichukua nafasi ya kocha Marcio Maximo.
Matokeo haya ni mazuri kwa Stars na angalau yametuliza kiu ya mashabiki wa soka nchini ambao kwa muda mrefu wamekuwa wanyonge kila timu yao inapocheza.Ili iweze kuingia hatua ya makundi, sambamba na Morocco, Ivory Coast na Gambia, Stars itahitaji sare tu katika mechi ya marudiano itakayofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wiki ijayo.
Mara baada ya mchezo kumalizika, Poulsen alisema kikosi chake kilicheza vizuri, na anashukuru mfumo wake wa kushambulia mfululizo ulizaa matunda.
Stars iliyotua mjini N'djamena siku moja kabla ya pambano, walioonekana kuwa na hamu ya kupata ushindi wa ugenini, walianza mchezo kwa kasi, na ndani ya dakika ya kwanza tayari walikuwa wameshafika langoni mwa wapinzani wao.
Falsafa ya kocha wa Stars Jan Poulsen ya kushambulia mwanzo mwisho, ilionekana kuwa kasi tangu mwanzo, baada wachezaji wake kugongeana vizuri pasi bila wenyeji kugusa mpira na kulazimisha kona dakika ya kwanza lakini bila kuzaa matunda.
Taifa Stars ambayo kwa mara ya kwanza jana ilishuhudia Shomari Kapombe akianza kwenye kikosi cha kwanza Poulsen, iliandika bao la kuongoza dakika ya 12 kupitia kwa Mrisho Ngassa.Ngassa alifunga bao hilo tamu baada ya kutumia akili nyingi na maarifa kuvunja mtego wa kuotea na kumfunga kipa wa Chad Brie Mbaya, ikiwa ni pasi ya Nizar Halfan.
Baada ya bao hilo, wenyeji Chad walicharuka na iliwachukua dakika tatu baadaye kufunga bao la kusawazisha likiwekwa kimiani na mshambuliaji Labo Mahamat.Bao hilo lilianza kwa mpira wa adhabu ndogo kufuatia winga wa pembeni wa Stars, Mrisho Ngassa kumchezaji faulo staa wa Chad Ndousel Ezekiel.
Karim Yaya alipiga adhabu hiyo na kumkuta mfungaji aliyeunganisha wavuni. Ngassa alionyeshwa kadi ya njano kwa kosa hilo.Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu, huku Stars wakitawala nusu ya kwanza ya kipindi cha kwanza kupitia kuelewana vizuri kwa viungo wanaocheza soka la kulipwa, Abdi na Nizar.
Hata hivyo, wenyeji Chad waliokuwa wakiongozwa na nyota wao Mahamat na Ezekiel, walicharuka nusu ya mwisho ya kipindi hicho baada ya kuusoma mchezo wa Stars.Kikosi cha Stars kilikuwa, Kaseja, Kapombe, Idrisa, Morris, Nyosso, Henry, Nditi, Ngassa, Abdi, Samatta na Nizar.

Esperance yatwaa ubingwa wa AfrikaBEKI Harrison Afful aliifungia bao la ushindi, Esperance ya Tunisia katika mechi ya fainali ambayo Wydad Casablanca waliokuw 10 uwanjani walilala kwa bao 1-0 katika mchezo wa pili wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Afful alifumania nyavu katika dakika ya 21, aliingia ndani ya eneo la hatari na kuachia mkwaju uliopmpita kipa wa Wydad, Yassine Bouno—aliyesimama langoni kuchukua nafasi ya mkongwe Nadir Lamyaghri aliyeumia mazoezini.

Esperance iliyotwaa ubingwa mara ya mwisho 1994, wakati Wamorocco wa Wydad walitwaa ubingwa mwaka ’92.Timu hizop mbili kutoka Kaskazini mwa Afrika zilitoka suluhu katika mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye mji wa Casablanca wiki moja iliyopita.

Wydad ilipunguzwa kasi baada ya mchezaji wake, Mourad Lemsen kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea vibaya Yannick N’Djeng.Esperance iliyopigwa 6-1 na TP Mazembe ya DR Congo katika fainali ya mwaka jana. Esperance pia iliingia fainali mwaka 1999 na kufungwa na Raja Casablanca Morocco kwa penalti na mwaka uliofuata ilifungwa na Hearts of Oak.

Lakini safari hii ikicheza mbele ya mashabiki 50,000 waliojazana Stade 7 November mjini Rades walikuwa na kila sababu ya kushinda.Baada ya bao, Afful alitengeneza mipira mingi ikiwemo wa dakika ya 28 alipomtolea pande Oussama Darragi, akiwa ndani ya eneo la hatari, alipaisha mpira huo.

Wydad ilishindwa kusawazisha nafasi ya wazi katika dakika ya 32 wakati Fabrice Ondama lakini shuti lake liliokolewa na kipa wa Esperance, Moez Ben Cherifa.