Thursday, February 23, 2012

STARS KUIVAA DRC LEO


KOCHA wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Jan Poulsen leo anatarajia ushindi toka kikosi chake alichokijumuisha na wachezaji chipukizi, pale kitakapopambana na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo katika mechi ya kirafiki ya kimataifa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Poulsen aliwaita kwa mara ya kwanza wachezaji kadhaa chipukizi kuunda kikosi hiko, ambacho pia kitashuka dimbani kucheza mechi ya kwanza kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Msumbiji wikiendi ijayo.
Akizungumza jijini jana jijini Dar es Salaam, Poulsen alisema ameridhishwa kwa kiasi kikubwa na maandalizi ya muda mfupi aliyofanya kuelekea mechi hiyo ya leo.
Poulsen alisema amefurahishwa kuona kiwango kizuri toka kwa nyota hao wapya, na hiyo inampa tumaini kwamba hakufanya makosa kuwapa jukumu la kupeperusha bendera ya nchi kwenye mchezo huo.
"Nawategemea sana kwenye mechi ya kesho (leo) wameonyesha kiwango kizuri kwenye mazoezi naamini watalibeba jahazi langu na watakuwa chachu ya ushindi," alisema Poulsen.

Miongoni mwa sura mpya ni pamoja na Abubakar Salum, Jonas Mkude na Waziri Salum, ambapo Kocha Poulsen amesema kuitwa kwao Stars ni kutokana na kiwango kizuri walichoonyesha kwenye timu zao.
Tofauti na wakati mwingine nyuma, ambapo Poulsen alikuwa na falsafa ya kuwategemea zaidi nyota wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi, safari hii ameipotezea falsafa hiyo.

Wachezaji wa nje walioitwa lakini hawatacheza mechi ya leo, ni pamoja na Nizar Khalfan anayecheza soka la kulipwa na klabu ya Philadephia ya Marekani na Ally Badru wa Canal Suez ya Misri.
Wachezaji hao watakosa mechi hiyo kwa vile Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liliwaombea mechi dhidi ya Msumbiji, ambapo wanatarajia kuwasili wakati wowote wiki hii.
Mbali na wachezaji hao wa kulipwa, pia Poulsen atategemea uzoefu wa nahodha Shedrack Nsajigwa, Nassor Said, Aggrey Moris, Juma Nyoso na Kelvin Yondani.
Wengine ni Shabani Nditi, Shomari Kapombe, Mwinyi Kazimoto, Abdi Kasim 'Babi' Hussein Javu, John Bocco, Mrisho Ngasa, Uhuru Selemani, na magolikipa Shaban Kado, Juma Kaseja na Mwadini Ali.
Aidha, akiongea juu ya pambano hilo, Kocha Msaidizi wa wa Kongo Muntubile Santos alisema wamejiandaa vizuri kwa mechi hiyo na wana uhakika kushinda.
"Timu yangu ni nzuri tumeiandaa kuja kushinda hata Tanzania, nafahamu kwamba matokeo ndiyo yataamua timu gani ni nzuri," alisema Santos katika mkutano na waandishi wa habari.
Akiongea kuhusu wapinzani wao Taifa Stars, Santos alisema naamini wenyeji wana timu nzuri inayoweza kuwapa changamoto kuwa ya ushindani lakini bado anaamini watafanya vizuri.
Hata hivyo alisema watawakosa nyota wao wa kulipwa akiwemo mpachika mabao ya hatari akiwemo Alain Kaliyutika anayecheza soka Qatar, lakini kuwapo kwa Tresor Mputu ni tumaini kubwa la ushindi.
Mputu aliwahi kuwa mchezaji bora wa Afrika miaka ya nyuma na pia alishawahi kufanya majaribio timu ya Arsenal.
Alisema kikosi chake kinaundwa na wachezaji kutoka timu ya TP Mazembe, Vital Club na DC Motema pembe.