Kocha mkuu wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ Charles Boniface Mkwasa (kushoto) akifafanua jambo leo wakati akitaja kikosi kipya tangu ateuliwe jana (kulia) kocha msaidizi Hemed Morocco
Kocha wa timu ya Taifa ‘Taifa
Stars’ Charles Boniface Mkwasa Jana ametangaza kikosi kipya cha timu hiyo
ambacho kitaingia kambini hivi karibuni kwa ajili ya kujiandaa na
mchezo wa marudiano wa kufuzu kucheza fainali za michuano ya Mataifa ya
Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN) utakaopigwa kwenye uwanja
wa Namboole, Kampala Uganda.
Mbali na kutangaza kikosi cha
wachezaji 26, Mkwasa ametaja vipaombele vyake kwenye timu hiyo ambavyo
amezingatia katika kuteua majina hayo. Amesema kitu pekee ambacho
wameangalia ni uwezo wa mchezaji na nidhamu ndani na nje ya uwanja ili
kuweza kujenga timu imara ambayo itakuwa na uwezo wa kupambana kwa
kuwawakilisha watanzania.
Ametaja pia benchi la ufundi
ambalo atashirikiana nalo katika kuhakikisha wanatekeleza majukumu ya
kuinoa Stars mpya, waliotajwa kwenye benchi la ufundi ni pamoja na kocha
msaidizi Hemed Morocco, kocha wa makipa Peter Manyika, madaktari wa
timu watakuwa wawili watatangazwa baada ya kuwasiliana na idara ya tiba,
mtunza vifaa Hussein Sued ‘Gaga’ Mshauri wa timu Abdallah Kibadeni
‘King Kibadeni Mputa’, mratibu wa timu Alhaj Ahmed Idd Mgoyi na meneja
wa timu ni Juma Mgunda.
Mkwasa pia ameomba ushirikiano
kutoka kwenye vilabu vyote vya Tanzania na pindi watakapoliona benchi la
ufundi la Stars kwenye vilabu vyao watoe ushirikiano kwani watakuwa
wakitembelea vilabuni ili kufuatilia kwa karibu maendeleo ya wachezaji
ili kuendelea kukiimarisha kikosi chao.
Ameishukuru kamati ya utendaji ya
TFF kwa kumuamini na kumpa majukumu ya kuifundisha timu ya Taifa huku
akikiri kuwa kazi hiyo siyo nyepesi kwasababu timu imeshapoteza mchezo
wake wa nyumbani kwa idadi kubwa ya magoli lakini akakiri kuwa kwenye
mpira chochote kinaweza kikatokea. Mbali na kuishukuru TFF, ameushukuru
pia uongozi wa klabu yake ya Yanga kwa kumruhusu kwenda kuifundisha timu
ya Taifa.
Lakini Mkwasa ameonya kuwa,
wachezaji ambao wameitwa kwenye kikosi cha Taifa wanatakiwa kuendelea
kufanya vizuri kwenye kikosi cha Stars na vilabu vyao. Mchezaji yeyote
ambaye hatopata nafasi ya kucheza kwenye klabu yake hatoitwa kwenye
kikosi cha Taifa hata kama anacheza nje ya nchi kama mchezaji nwa
kulipwa.
Kikosi kipya cha Stars ni;
Mudathir Khamis (KMKM), Mwadini Ali (Azam FC) na Ally Mustafa ‘Barthez’ (Yanga).
Mabeki ni Shomary Kapombe (Azam), Michael Aidan (Ruvu
Shooting), Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ (Simba SC), Mwinyi Hajji
Mngwali (KMKM), Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (Yanga SC), Kevin Yondan (Yanga
SC), Hassan Isihaka (Simba SC), Aggrey Morris (Azam FC).
Viungo ni Jonas Mkude (Simba SC),
Abdi Banda (Simba SC), Salum Telelea (Yanga SC), Frank Domayo (Azam
FC), Simon Msuva (Yanga SC), Said Ndemla (Simba SC), John Bocco (Azam
FC), Ramadhani Singano ‘Messi’ Simba SC na Deus Kaseke (Mbeya City).
Washambuliaji ni Atupele Green (Kagera Sugar), Rashid Mandawa
(Kagera Sugar), Ame Ali (Mtibwa Sugar), wakati wengine ambao wamewekwa
akiba ni Juma Abdul wa Yanga SC, Mudathir Yahya wa Azam FC na Samuel
Kamuntu wa JKT Ruvu.
Leo benchi la Ufundi la Stars litakutana na wachezaji wote
walioteuliwa katika hoteli ya Tansoma, eneo la Gerezani, Dar es Salaam
ili kuzungumza nao juu ya uzalendo na Mkwasa amesema Jumamosi timu
itaenda kuweka kambi nje ya mji.
Mwisho, amewaomba wapenzi na
mashabiki wa Stars wasahau yote yaliyopita kwasababu timu ipo mikononi
mwao nao wanaamini watafanya vizuri. Amewaomba watanzania kuiunga mkono
timu yao kama ilivyokuwa zamani na kuacha vitendo vya kuwadhihaki
wachezaji ikiwa ni pamoja na kuwapiga mawe