Tuesday, December 17, 2013

LIVERPOOL WAMPONZA ''AVB'', ATIMULIWA TOTTENHAM

 
Andre Villa-Boas maarufu kama AVB
 
Klabu Tottenham imemtimua kocha wake Andre Villas Boas siku moja baada ya Tottenham kupata kichapo cha magoli 5- 0 kutoka Liverpool
Kipigo hicho cha magoli 5 - 0 ni moja kati ya matokeo mabaya kutokea katika uwanja wao wa nyumbani wa Tottenham wa White Hart Lane kwa takriban miaka 16 iliyopita.
 
Wakati Tottenham wakitimua kocha kwa upande wake Meneja wa Liverpool Brenden Rodgers amesema hatua ya timu yake kuisambaratisha Tottenham kwa magoli 5 - 0 katika uwanja wao wa nyumbani wa White Hart Lane ni moja kati ya mechi ya viwango vya juu vilivyoonyeshwa na Liverpool katika kipindi cha uongozi wake.
Rodgers alishika hatamu ya kuinoa Liverpool mwaka 2012 ambapo kwa sasa timu hiyo ipo nafasi ya pili ikiwa nyuma ya Arsenal katika msimamo wa ligi kuu ya England.
"Ni matokeo mazuri na viwango vya hali ya juu," amesema Rodgers.
"Tumepata magoli matano na inawezekana tungepata mengi hata saba au nane. Huo ndio uzuri wa timu ambapo inapata magoli."
Mshambuliaji wa timu hiyo Luis Suarez alifunga magoli mawili wakati Jordan Henderson, John Flanagan na Raheem Sterling wakifunga kila mmoja.
Wakati wa mchezo huo Tottenham alishindwa kulenga hata mara moja kwenye goli la Liverpoool ambayo imefunga timu hiyo katika mechi nane za ligi kuu ya England ziliyochezwa kwenye kiwanja hicho.