Tuesday, December 11, 2012

TAIFA QUEENS BINGWA WA MABARA WAICHAKAZA MALAYSIA KATIKA FAINALI

wachezaji wa timu ya taifa ya Netiboli, wakiwasili kwenye uwanja wa kimataifa wa Julius Nyerere, wakitokea Singapore walikokuwa wakishiriki mashindano ya mabara na kuibuka mabingwa. Hakika wanastahili pongezi
Taifa Queens ilipowasili nchini

Timu ya netiboli ya Tanzania (TAIFA QUEENS) imeibuka kidedea na kushinda mchezo wa fainali dhidi ya Malaysia kwa kuibanjua mabao 45-38. Kwa matokeo hayo Taifa Queens imetawazwa kuwa bingwa wa mabara kwa mwaka huu wa 2012 (IFNA Inter-Continental netball title). 
Mashindano hayo yaliyofanyika Nchini Singapore  ambayo bingwa mtetezi alikuwa Australia yameshuhudia Taifa Queens ikimaliza mashindano bila kupoteza mchezo hata mmoja. Mwenyekiti wa Chaneta Anna Bayi amesema mpaka timu zinaenda mapumziko tayari Taifa Queens walikuwa mbele kwa mabao 25-16, Waliporudi kipindi cha pili ilikuwa kumalizia kazi nzuri waliyoianza.

Timu hiyo imewasili nchini jana na kombe la mabara na medali za dhahabu na kuleta heshima mpya kwa Tanzania katika anga ya michezo, Ikumbukwe Taifa Queens ilitembeza bakuli balaa mpaka kufikia kuelekea Singapore huku wadau wenye kuweza kudhamini michezo wameng'ng'ania kupanda mbegu zisizoota kwenye mpira wa miguu, Wakati umefika wadau kuigeukia michezo mingine na huenda mungu akatujaalia kama jinsi nyota inavyoanza kuonekana katika sekta ya michezo nchini.

Hongereni sana Taifa Queens kwani mmetutoa kimasomaso na sasa Tanzania itaanza kutamkwa bila kung'atang'ata maneno katika anga za michezo duniani.

Taifa Queens wakifanya vitu vyao..wacha weeee..kalieni soka tu halafu tuone tutafika wapi!!

Weyee, Chezea Taifa Queens weweeee!!!

Sisi ndio sisi bhanaaaaa mtausaka kwa tochi hamuupati ngodo!

HAKUNA KAMA LEONEL MESSI

LIONEL Messi amevunja rekodi ya miaka 40, iliyowekwa na gwiji wa Ujerumani, Gerd Mueller baada ya kufunga mabao 86 ndani ya mwaka mmoja kwa klabu na timu ya taifa.
Mshambuliaji huyo wa Argentina alifunga mabao mawili na kuiongoza Barcelona kushinda 2-1 dhidi ya Real Betis Jumapili kwenye mchezo wa Ligi ya Hispania.


Bao lake la kwanza ni juhudi binafsi, alilifunga katika dakika 16 na kumfikia Mueller aliyeweka rekodi ya kufunga mabao 85 mwaka 1972, zikiwa zimebaki dakika tisa, Messi alifunga bao lake 86 mwaka huu.


"Kama ninavyosema wakati wote, ni vizuri kuweka rekodi hii, lakini jambo muhimu zaidi ni kuisaidia timu kushinda," alisema Messi. "Kila wakati nasema kazi yangu ni kuona timu inatwaa ubingwa wa Ligi Kuu, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Copa del Rey."


Messi amefunga mabao 74 kwa Barcelona na 12 kwa timu yake ya taifa ya Argentina mwaka huu. Amebakiza michezo mitatu kabla ya kufunga mwaka huu na huenda akatengeneza rekodi mpya. Mueller alifunga mabao 85 akiwa na Bayern Munich na Ujerumani Magharibi.
Messi mwenye miaka 25 alivunja rekodi ya gwiji wa Brazil, Pele aliyeifungia Brazil na Santos mwaka 1958 mabao 75, lakini nyota huyo wa Argentina, Novemba 11 alivunja rekodi hiyo kwa kufunga bao la 75 na 76 na kuanza kuisaka rekodi ya Mueller.


Baada ya kuweka rekodi ya kufunga mabao 50, msimu uliopita, Messi ameiongoza Barcelona kuanza msimu huu kwa kishindo wakishinda mechi 14 na kutoka sare moja kati ya 15. Pia ameshafunga mabao 30 kwenye michuano yote aliyoichezea timu mpaka sasa.


"Hakuna mchezaji mwingine kama Messi," alisema kocha Barcelona, Tito Vilanova. "Siyo kwa sababu ya uwezo wake wa kufunga, lakini ni pamoja na ujuzi wake wa kutoa pasi, kuwatoka mabeki, na kuelewa mchezo kwa haraka."


Messi, ambaye Novemba 2 alikuwa baba wa mtoto wa kiume aitwaye Thiago, pia ametajwa kwenye wachezaji watatu wanaowania tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka wa FIFA akiwa pamoja na Andres Iniesta na mshambuliaji wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo.
Messi ametwaa tuzo wa Ballon d'Or mara tatu mfululizo na kuisaidia Barcelona kutwaa ubingwa wa La Liga mara tatu, Ligi ya Mabingwa mara mbili na mataji mengi 10.


Pia, anategemewa kuwa mchezaji wa kwanza kuchukua tuzo ya mwanasoka bora wa dunia kwa mara ya nne. Mshindi atatangazwa Januari 7.