Tuesday, December 11, 2012

HAKUNA KAMA LEONEL MESSI

LIONEL Messi amevunja rekodi ya miaka 40, iliyowekwa na gwiji wa Ujerumani, Gerd Mueller baada ya kufunga mabao 86 ndani ya mwaka mmoja kwa klabu na timu ya taifa.
Mshambuliaji huyo wa Argentina alifunga mabao mawili na kuiongoza Barcelona kushinda 2-1 dhidi ya Real Betis Jumapili kwenye mchezo wa Ligi ya Hispania.






Bao lake la kwanza ni juhudi binafsi, alilifunga katika dakika 16 na kumfikia Mueller aliyeweka rekodi ya kufunga mabao 85 mwaka 1972, zikiwa zimebaki dakika tisa, Messi alifunga bao lake 86 mwaka huu.


"Kama ninavyosema wakati wote, ni vizuri kuweka rekodi hii, lakini jambo muhimu zaidi ni kuisaidia timu kushinda," alisema Messi. "Kila wakati nasema kazi yangu ni kuona timu inatwaa ubingwa wa Ligi Kuu, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Copa del Rey."


Messi amefunga mabao 74 kwa Barcelona na 12 kwa timu yake ya taifa ya Argentina mwaka huu. Amebakiza michezo mitatu kabla ya kufunga mwaka huu na huenda akatengeneza rekodi mpya. Mueller alifunga mabao 85 akiwa na Bayern Munich na Ujerumani Magharibi.
Messi mwenye miaka 25 alivunja rekodi ya gwiji wa Brazil, Pele aliyeifungia Brazil na Santos mwaka 1958 mabao 75, lakini nyota huyo wa Argentina, Novemba 11 alivunja rekodi hiyo kwa kufunga bao la 75 na 76 na kuanza kuisaka rekodi ya Mueller.


Baada ya kuweka rekodi ya kufunga mabao 50, msimu uliopita, Messi ameiongoza Barcelona kuanza msimu huu kwa kishindo wakishinda mechi 14 na kutoka sare moja kati ya 15. Pia ameshafunga mabao 30 kwenye michuano yote aliyoichezea timu mpaka sasa.


"Hakuna mchezaji mwingine kama Messi," alisema kocha Barcelona, Tito Vilanova. "Siyo kwa sababu ya uwezo wake wa kufunga, lakini ni pamoja na ujuzi wake wa kutoa pasi, kuwatoka mabeki, na kuelewa mchezo kwa haraka."


Messi, ambaye Novemba 2 alikuwa baba wa mtoto wa kiume aitwaye Thiago, pia ametajwa kwenye wachezaji watatu wanaowania tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka wa FIFA akiwa pamoja na Andres Iniesta na mshambuliaji wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo.
Messi ametwaa tuzo wa Ballon d'Or mara tatu mfululizo na kuisaidia Barcelona kutwaa ubingwa wa La Liga mara tatu, Ligi ya Mabingwa mara mbili na mataji mengi 10.


Pia, anategemewa kuwa mchezaji wa kwanza kuchukua tuzo ya mwanasoka bora wa dunia kwa mara ya nne. Mshindi atatangazwa Januari 7.

No comments:

Post a Comment