Monday, April 16, 2012

MAZISHI YA MUTHARIKA KUIGHARIMU MALAWI MILIONI 600 KUAGWA SIKU 10


Aliyekuwa Rais wa Malawi marehemu Bingu wa Mutharika

Serikali ya Malawi imetenga siku kumi kwa ajili ya wananchi wa Taifa hilo kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Bingu wa Mutharika.

Mwili wa kiongozi huyo unatarajiwa kuwasili leo jijini Lilongwe ukitokea katika hosipitali ya jeshi mjini Pretoria, Afrika Kusini na baadaye utapelekwa Ikulu ambako waombolezaji watapata fursa ya kuanza kutoa heshima za mwisho.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi ya Mutharika, Henry Mussa alisema kesho Jumapili mwili wa kiongozi huyo utaendelea kuwapo Ikulu na milango itakuwa wazi kwa wanafamilia na marafiki wa karibu kutoa heshima zao za mwisho na Jumatatu utawekwa katika jengo jipya la Bunge mjini Lilongwe ambako wananchi watapata fursa ya kutoa heshima hizo kwa siku mbili.

Mussa ambaye pia ni Waziri wa Serikali za Mitaa, alisema Jumatano mwili wa Mutharika utapelekwa katika mji wa Mzuzu ambako wananchi wa Kanda ya Kaskazini mwa Malawi pia watamuaga kiongozi wao, na Alhamisi mwili huo utasafirishwa kwenda Blantyre ambako utahifadhiwa Ikulu ya ndogo ya Sanjika.


Marehemu Mutharika kulia akiteta jambo na Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe enzi za uhai wake

Katika Ikulu hiyo wananchi watatoa heshima zao za mwisho kwa siku tatu hadi Jumamosi, April 21 kisha mwili huo kupelekwa katika eneo la maziko, shamba la Ndata, ambako wakazi wa eneo hilo pia watatoa heshima zao za mwisho, Jumapili Aprili 22.

Mussa alisema siku ya mazishi ambayo ni Jumatatu Aprili 23, 2012 watakaoruhusiwa kutoa heshima zao za mwisho ni wakuu wa nchi, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa na wale wa Jumuiya za Kikanda kabla ya Ibada itakayoongozwa na Kanisa Katoliki ambalo Mutharika alikuwa muumini wake.

Juzi, Ikulu ya Lilongwe ilithibitisha kwamba Rais Jakaya Kikwete ni miongoni mwa wakuu wa nchi na Serikali ambao wamealikwa kushiriki mazishi ya kiongozi huyo ambaye alifariki Aprili 5, mwaka huu kutokana na ugonjwa wa moyo.

Mutharika atazikwa katika shamba la Ndata katika Wilaya ya Thyolo iliyoko umbali wa Kilometa 45 Kusini mwa Blantyre, uamuzi ambao Mussa alisema ulitokana na maelekezo yake aliyoyatoa kabla hajafariki dunia.

“Kwa wale ambao tumewahi kufika Ndata alipozikwa mke wake Ether, aliweka sehemu ambayo pia angependa azikwe yeye, kwahiyo sisi ni akina nani hadi tupinge uamuzi wake?” alisema Mussa.

Mazishi kugharimu Sh600 milioni
Katika hatua nyingine Mussa alisema Serikali ya Malawi imechukua hatua za kuhakikisha kwamba hakutakuwa na uhaba wa mafuta wakati wote wa taratibu za mazishi ya Mutharika, ambayo yataigharimu nchi hiyo Kwacha150 milioni (zaidi ya Sh600 milioni).

Waziri wa Fedha wa Malawi juzi aliwasilisha bajeti ya Kwacha400 milioni (zaidi ya Sh1.6 bilioni) mbele ya kikao cha Baraza la Mawaziri lakini kikao hicho kilichokutana na chini ya Uenyekiti wa Rais Joyce Banda kikaipunguza hadi kufikia kwacha150 milioni.

Mussa alisema mbali na msaada wa lita milioni tano za mafuta ambazo Malawi imepokea kutoka Serikali ya Zambia, kiasi kingine cha lita milioni 20 kinatarajiwa kuingia mapema iwezekanavyo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba shughuli za Serikali hazikwami.


Mwenyekiti wa kamati ya mazishi Henry Mussa ambaye pia ni Waziri wa serikali za mitaa

“Shehena ya mafuta inaingia sasa kupitia sehemu mbalimbali, katika Bandari ya Dar es Salaam (Tanzania) na Beira, pia kule Nakala na tunataraji kwamba mafuta haya yatatumika kuhakikisha shughuli za mazishi ya Rais wetu hazikwami,” alisema Mussa.

Jana Malawi ilipokea rasmi mafuta ya msaada yaliyotolewa na Zambia kupitia kwa Rais wa nchi hiyo Michael Satan yalikabidhiwa na Waziri mwenye dhamana ya Nishati nchi hiyo, Christopher Yalima kwa Rais Banda.

Uhaba wa mafuta nchini Malawi ulianza kujitokeza miaka mitatu iliyopita lakini hali inaelezwa kuwa mbaya zaidi yapata miezi miwili iliyopita, kiasi cha kusababisha bei za bidhaa kupanda hivyo kuongeza ugumu wa maisha kwa Wamalawi.
Maombolezo Ikulu
Wananchi wa Malawi wameendelea kuingia Ikulu ya Malawi kwa ajili ya maombolezo ya Mutharika pia kuwafariji wafiwa katika msiba huo.

Habari kutoka Blantyre pia zinasema maombolezo kama hayo yanaendelea katika shamba la Mutharika la Ndata ambalo pia lilifunguliwa kwa ajili ya kuwaruhusu wananchi kuhani msiba wa kiongozi wao.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais wa Malawi, Khumbo Kachali aliapishwa jana na Jaji Mkuu wa nchi hiyo, Lovemore Munlo katika hafla iliyohudhuriwa na Rais Banda na mamia ya wafuasi wa chama kipya cha Peoples Party (PP).

No comments:

Post a Comment