Saturday, June 16, 2012

MWANAMAMA FATOU ARITHI MIKOBA YA OCAMPO MAHAKAMA YA KIMATAIFA YA UHALIFU WA KIVITA


Bi Fatou Bensouda

Luis Moreno Ocampo(kushoto) mwendesha mashtaka anaemaliza muda wake na Bi Fatou Bensouda (kulia)

Mwendesha Mashtaka Mkuu mpya wa Mahakama ya Kimataifa ya kukabiliana na Uhalifu wa Kivita ameapishwa mjini Hague hii leo.

Bi Fatou Bensouda, aliyekuwa Waziri wa Haki nchini Gambia,ndiye Mwafrika na pia mwanamke wa kwanza kushikilia wadhifa huo wa kuendesha mashtaka ya uhalifu wa kivita.
Mtihani wa kwanza kwa mwanamama Fatou ni kumleta Hague mtoto wa aliyekuwa kiongozi wa Libya, Kanali Muamar Gaddafi, Saif al-Islam Gadaffi, ambaye ameshtakiwa kwa makosa dhidi ya binadamu na wakati huohuo kuongoza mashtaka yanayomkabili aliyekuwa kiongozi wa Ivory Coast, Laurant Gbagbo.


Bi Bensouda akila kiapo kuitumikia mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita

Fatou Bensouda amechukua nafasi ya Luis Moreno Ocampo"Jembe", ambaye ameongoza mahakama hiyo kwa zaidi ya mwongo mmoja.

Kesi ya rais wa zamani wa Liberia, Charles Taylor, ilisikilizwa na mahakama ya Umoja wa mataifa inayosikiliza kesi za waliohusika na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini
Sierra Leone.


Bi Bensouda amekuwa akifanya kazi kama naibu wa Luis Moreno-Ocampo anayemaliza muda wake katika mahakama ya ICC huko The Hague.

Mwandishi wa BBC anasema kuwa licha ya kwamba Bi Bensouda sio mgeni kwa mambo ya Hague, uteuzi wake unakuja wakati mfumo wa sheria ya kimataifa unahojiwa sana.

Pia anachukua jukumu hilo wakati kuna mtafaruku katika mahakama hiyo huku maafisa wanne wa mahakama hiyo wakiwa wanazuiliwa nchini Libya.

Mwandishi wa BBC anasema kuwa Bi Bensouda anasifika kwa kuwa mtulivu kitu ambacho huenda kimemsaidia katika kazi yake.
Ikizingatiwa kuwa washukiwa wengi ambao kesi zao ziko katika mahakama ya ICC ni waafrika na hili limekosolewa huku ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu  ikisadikiwa kuwalenga zaidi waafrika.


Bi Bensouda akifuatilia jambo mahakamani huko The Hague

Bi Bensouda katika "swagga"

Inatarajiwa kwamba kwa kuwa Bi Bensouda mwenyewe ni Mwafrika tena wakili, huenda akasaidiwa na hili kunyamazisha wakosoaji wake, kulingana na wadadisi wa mambo.

Mwezi Machi mbabe wa kivita kutoka DRC, Thomas Lubanga alipokea hukumu ya kwanza ya kesi yake ikiwa hukumu ya kwanza kuwahi kutolewa na mahakama hiyo tangu kuundwa kwake miaka kumi iliyopita.

Kikosi cha viongozi wa mashtaka wanataka Lubanga atundikwe miaka 30 jela kwa makosa ya kutumia watoto kama wanajeshi wakati wa vita mashariki mwa DRC  kati ya mwaka 2002 na 2003.

No comments:

Post a Comment