Monday, January 30, 2012

Zambia yawaliza wenyeji kombe la mataifa ya Afrika

Wachezaji wa Zambia
Wachezaji wa Zambia wakishangilia bao

Zambia ilijitengea nafasi katika robo fainali za michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa kuwashinda wenyeji Equatorial Guinea bao 1-0 katika mechi ya kundi A, na kuongoza kundi hilo, ikiwa na pointi 7.
Nahodha Chris Katongo aliifungia Zambia bao hilo katika dakika ya 67.
Zambia 1-0 Guinea

Ushindi huo unamaanisha kwamba Zambia huenda wakaepuka kucheza na Ivory Coast katika robo fainali, nchi ambayo inatazamiwa kuongoza kundi B.
Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Equatorial Guinea kushindwa, na ambao wanashirikiana na Gabon kama wenyeji wa mashindano hayo.
Ilikuwa pia ni mara ya kwanza kwa kocha mpya Gilson Paulo akiitizama timu yake ikifungwa.
Equatorial Guinea imo katika nafasi ya pili katika kundi A, ikiwa na pointi 6, Libya ina nne, na Senegal ni ya mwisho ikiwa haina pointi zozote.
Wenyeji Equatorial Guinea tayari walikuwa wamefuzu, na Zambia walihitaji tu kuondoka sare kuingia robo fainali.
Ushindi wa Chipolopolo unamaanisha kwamba sasa watasafiri kuelekea hadi uwanja wa Bata, katika kujiandaa kwa mechi yao ya robo fainali siku ya Jumamosi, tarehe 4 Februari.
Kinyume na Senegal ambao wanarudi nyumbani bila hata pointi moja, Libya inaondoka mashindano hayo baada ya kupata ushindi wa magoli 2-1 katika mechi yake ya Jumapili dhidi ya Senegal.
Ihab Albusaifi alifunga katika kipindi cha kwanza, na vile vile katika kipindi cha pili.
Deme Ndiaye aliifungia Senegal, na kinyume cha matazamio ya wengi, timu hiyo sasa inarudi nyumbani baada ya kushindwa katika mechi tatu.
Hata hivyo bado ni fahari kwa timu ya Libya ya Mediterranean Knights kuondoka mashindano hayo kwa kupata ushindi katika mechi, ikiwa ni ushindi wao wa kwanza tangu mwaka 1982, wakati nchi yao ilikuwa mwenyeji wa mashindano hayo
Huu ni ushindi wao wa kwanza kwa mechi ya Kombe la Mataifa ya Afrika, nje ya nchi yao.
Watajipongeza kwa kufikia hatua hiyo, hasa wakikumbuka kwamba ni hivi majuzi tu nchi yao imeanza kupata kutulia baada ya matatizo mengi.

No comments:

Post a Comment