Friday, August 26, 2011

KIKOSI STARS CHATANGAZWA COSTA NDANI CANNAVARO OUT

Sosthenes Nyoni
BAADA ya takribani miaka minne, hatimaye beki wa kimataifa wa Tanzania na Simba,Victor Costa ameitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars, huku Nadir Haroub akiachwa kwa mara ya kwanza tangu 2006.

Kocha Jan Poulsen jana alitangaza kikosi chake cha wachezaji 22 kinachojiandaa na mechi ya kuwania kufuzu kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika 2012 dhidi ya Algeria hapo Septemba.

Akitangaza kikosi hicho jana kwa Wanahabari jijini Dar es Salaam, Poulsen kwa mara ya kwanza tangu alipokabidhiwa jukumu la kukinoa kikosi hicho amemwacha beki kisiki wa timu hiyo na Yanga, Haroub 'Canavaro' sambamba na kumrejesha kipa Juma Kaseja wa Simba.

Poulsen ambaye katika kikosi chake alichokiita kwa ajili ya mechi dhidi Sudan aliwaengua wachezaji wote, lakini jana aliwajumuisha wachezaji hao wa kulipwa Tanzania wanaocheza nje ya nchi.

Wachezaji hao sita wanaocheza soka ya kulipwa nje ya nchi ni Mbwana Samata (TP Mazembe, DRCongo) akiwamo Henry Joseph (Kosvinger, Norway), Nizar Khalfan (Whitecaps, Canada), Abdi Kasim 'Babi' na Dany Mrwanda (Long, Vietnam) na Athuman Machupa (Vasslander, Sweden).
Beki Costa ambaye hivi karibuni alirejea katika kikosi cha Simba akitokea klabu ya HCB Songo ya Msumbiji, mara ya mwisho aliichezea Taifa Stars kwenye mechi ya kuwania kufuzu kwa fainali za Afrika 2008 dhidi ya Msumbiji mwaka 2007, wakati huo Stars ikiwa chini ya kocha Mbrazil Marcio Maximo.

Poulsen alisema sababu iliyomsababisha kumwita Costa licha ya kumwona katika mechi moja tu ya Simba dhidi Yanga alisema alizingatia ushauri aliopewa na baadhi ya makocha wenzake waliomweleza kwamba mchezaji huyo ni mmoja kati ya mabeki bora nchini.

Poulsen akizunguzia pambano dhidi ya Algeria na nafasi ya Stars kufuzu kwa fainali hizo alisema Algeria ni kati ya timu imara Afrika, ikumbukwe kwamba mara kadhaa imebadili kocha kwa lengo la kuhakikisha wanafanya vizuri, kufungwa mabao 4 na Morocco haimaanishi wao ni legelege.

"Wakati mwingine ni vizuri tukawa wakweli na wawazi, nafasi yetu ya kufuzu ni finyu sana na hii ni kutokana na matokeo ya kundi letu lilivyo, lakini sisemi kwamba hatutakiwi kupambana hapana, tunaichukulia mechi hii kwa umuhimu mkubwa kwa vile pia itakuwa sehemu ya kujiweka sawa kabla ya kucheza na Chad mwezi Novemba."

Katika hatua nyingine Poulsen alilalamikia nidhamu mbovu kwa wachezaji uwanjani na kukosa moyo wa kujituma ndiyo sababu ya Tanzania na Afrika kwa ujumla kutofanya vizuri katika medani ya soka ulimwenguni ukilinganisha na nchi ya Ulaya.

"Mimi hapa nimeshawaita mara kadhaa wachezaji wanaocheza soka nje ya nchi, lakini utakuta hawaji wote, Abdi Kasim alifunga bao kule Algeria, lakini tangu hapo haji kuichezea nchi yake tena hivyo hivyo kwa Samata tulipocheza na Afrika Kusini hakuonekana, hili ni tatizo kubwa kwa Tanzania na Afrika," alisema Poulsen.

Kikosi kamili cha Poulsen ambacho kitakachoingia kambini jijini Dar es Salaam keshokutwa ni pamoja na makipa, Shaaban Dihile, Juma Kaseja na Shabani Kado, wakati mabeki wa pembeni ni Shadrack Nsajigwa, Idrisa Rajabu na Amir Maftah.
Mabeki wa kati ni Aggrey Morris, Juma Nyoso na Victor Costa, viungo ni Henry Joseph, Nurdin Bakar, Shaaban Nditi, Juma Seif 'Kijiko' na Jabir Aziz, Nizar Khalfan, Mrisho Ngasa na Salum Machaku.
Washambuliaji ni pamoja na Mbwana Samata, Abdi Kassim, 'Ramadhan Chombo, John Boko na Athuman Machupa.


No comments:

Post a Comment