Wednesday, August 17, 2011

VUMBI LAHAMIA NOU CAMP LEO

LEO ni fainali ya Hispania Super Cup, ambapo Barcelona itakuwa ikikabiliana na Real Madrid katika mechi ya pili ya kuwania kombe hilo baada ya timi hizi kukutana kwa mara ya kwanza Jumapili iliyopita kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu na kutoka sare ya 2-2.

Katika mechi ya kwanza iliyozikutanisha Real Madrid na Barcelona ya kuwania Hispania Super Cup siku ya Jumapili, timu ya Real Madrid ilipiga mashuti mengi golini, lakini mabingwa wa Ulaya na mabingwa wa Ligi Kuu ya Hispania wao walipata faida ya magoli mawili ya ugenini.

Timu hizi mbili zimekutana kwa mara ya kwanza katika kuwania Hispania Super Cup, ambapo katika mechi ya leo ya marudiano kwenye uwanja wa Camp Nou, Barcelona inapewa nafasi kubwa ya kutwaa kombe hilo.

Katika mechi ya kwanza kipa wa Real Madrid, Iker Casillas alishindwa kuzuia mipira ya hatari golini mwake kwa sababu mipira miwili ya hatari iliyopigwa golini mwake yote ilitinga nyavuni kati ya mashuti manne waliyopiga Barcelona.

Hivyo uwezo walioonyesha Barcelona ni wazi timu ya Real Madrid iliyo chini ya kocha Jose Mourinho itabidi ibadilishe mikakati yake katika mechi ya leo, lakini tangu Mourinho alipojiunga na Real Madrid ameweza kutoa ushindani mkubwa kwa klabu ya Barcelona tangu 2010.

Real Madrid itaingia leo kwenye Nou Camp ikiwa inajiamini kwamba juhudi zao walizozionyesha katika mechi ya kwanza wataziendeleza katika mechi hii ya leo, Real Madrid katika mechi hiyo ya mwanzo walionekana kuwa imara na hawakusumbuliwa na mfumo wa pasi nyingi wa Barcelona.

Ingawa Karim Benzema hakufunga katika mechi ya kwanza, lakini aliweza kusaidia vizuri Mesut Ozil ambaye alikuwa mchezaji muhimu wa Real Madrid katika mechi hiyo.

Cristiano Ronaldo vilevile alikuwa katika kiwango chake cha kutandaza soka, pia kocha Mourinho alipanga safu imara ya ulinzi hata hivyo Barcelona waliweza kuipenya ngome hiyo na kufunga magoli.

Katika mechi ya kwanza, Barcelona haikumtumia beki wake Carles Puyol na pia katika mechi ya leo beki huyo hatacheza. Kukosekana kwa beki huyo wa kati kulionyesha wazi pengo hilo, ingawa mabeki Javier Mascherano na Eric Abidal walijitahidi sana kucheza katika mechi hiyo.

Swali kubwa linalomkabili kocha Pep Guardiola katika mechi ya leo ni kama atampanga kiungo wake mpya Cesc Fabregas na kama atampanga atamtumia kwa muda gani.

Tangu siku ya Jumatatu Cesc Fabregas alianza kufanya kazi na wachezaji wenzake wa Barcelona hata hivyo mchezaji huyo anayetokea Arsenal ya England kwa muda mrefu sasa amekuwa hachezi mechi za ushindani.

Kocha wa Barcelona, Pep Guardiola anakabiliwa na wachezaji wake mahiri kutokuwa fiti, ambapo katika mechi ya kwanza dhidi ya Real Madrid wachezaji wake Xavi Hernandez, Gerard Pique na Pedro walitokea benchi.

Katika mechi ya leo Je, Barcelona itanufaika na kikosi chake na kutwaa ubingwa wa Hispania Super Cup ? au Real Madrid itaondoka na kombe hilo katika uwanja wa Camp Nou unaomilikiwa na Barcelona?

No comments:

Post a Comment