Monday, September 12, 2011

SIMBA YASHIKWA SHATI NA AZAM WAKATI IKIKWEA KILELENI

SIMBA wameshindwa kulipiza kisasi kwa Azam baada ya kulazimisha suluhu iliyowapeleka kileleni mwa Ligi Kuu, huku Shirikisho la Soka TFF ikizipeleka Yanga na Simba kucheza mechi zao kwenye Uwanja wa Azam Chamazi.

Matokeo hayo yanaifanya Simba kufikisha pointi kumi kileleni moja zaidi kwa JKT Ruvu huku Azam ikifikisha pointi tano katika michezo minne na Yanga wakiwa mkiani na pointi zao tatu.

Simba waliokuwa na deni la kulipiza kisasi cha mabao 3-0 na kuchezewa samba msimu uliopita na Azam kwenye Uwanja Taifa walizidiwa ujanja na matajiri hao wa Chamazi waliotawala sehemu kubwa ya mchezo huo, lakini walikosa umakini kwenye umaliziaji.

Azam walitengeneza nafasi nyingi za kufunga langoni kwa Simba na kuwafanya mashabiki wengi wa wekundu hao wa Msimbazi waliofurika uwanjani hapo kimya muda mrefu.

Viungo wa Simba, Gervais Kago na Haruna Moshi waliingia kwenye eneo la hatari la Azam dakika ya tisa kwa kugongea pasi, lakini kipa Mwadini Ally alikuwa makini kuokoa hatari hiyo.

Simba iliendeleza mashambulizi yake dakika 20, beki Juma Nyoso aliunganisha vizuri kona ya Ulimboka Mwakingwe, lakini uhodari wa kipa Mwadini ndiyo ulioinusuru Azam.

Krosi ya Mwakingwe ilitua mguuni mwa Kago aliyepiga shuti kali lililopaa juu ya goli na kuwaacha mashabiki waliofurika uwanjani hapo wakishika vichwa.

Tofauti na mechi ya Yanga na Ruvu Shooting iliyoingiza mashabiki 6,566, mchezo wa jana watazamaji walikuwa wengi kutokana na ushindani uliopo baina ya Simba na Azam.

Kiungo Jabir Aziz wa Azam alijaribu kumtungua kipa Juma Kaseja aliyekuwa ameacha goli kwa shuti la umbali wa mita 25 hata hivyo lilipaa juu kidogo ya lango la Simba.

Mshambuliaji John Boko alipoteza nafasi tatu ikiwemo ile ya dakika 45, alipopokea pasi ya Kipre Tchetche akiwa yeye na Kaseja, lakini akapiga nje.

Azam walitawala sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza katika kiungo wakiongozwa na Ibrahim Mwaipopo, huku Mrisho Ngassa na Tchetche walikuwa wakianzisha mashambulizi yao kutoka winga na kuifanya Simba kubaki nyuma muda mwingi.

Dakika 72, Mwaipopo nusura afunge goli baada ya mpira wake wa adhabu kugonga mwamba upande wa kulia na kurudi uwanjani.

Mwamuzi Isihaka Shirikisho alitoa kadi za njano kwa Haruna, Shija Mkina kwa Simba kwa upande wa Azam ni Ngasa, Mwaipopo na Morris.

Kocha wa Simba Moses Basena aliwashanga wengi pale alipoamua kumtoa Mkina aliyekuwa ameingia uwanjani baada ya Amri Kiemba kwa dakika kumi na nafasi yake kuchuliwa na Uhuru Selemani.

Naye Steward Hall alimpumzisha Kipre na kumwingiza Wahaba Yahya, pia Simba ilimtoa Kago na kuingia Shomari Kapombe.

SIMBA YANGA KUTUMIA UWANJA WA CHAMAZIHatimaye klabu za Yanga na Simba zimepata nafasi ya kuutumia uwanja wa Azam, Chamazi wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 2000 kwa ajili ya mechi zao za Ligi Kuu kuanzia wiki hii.

Taarifa ya Simba na Yanga kutumia uwanja wa Chamazi ilitolewa jana na Shirikisho la Soka nchini TFF ikiwa ni kutii maagizo ya Serikali ya kutaka Uwanja wa Taifa utumike kwa michezo miwili tu kwa wiki.

Uongozi wa Azam ambao awali ulikataa kuziruhusu klabu hizo kongwe nchini kutumia uwanja wake kutokana na kuhofia uhalibifu wa mali zake wamefanya mazungumzo na Simba na Yanga na kukubaliana.

Mechi zitakazochezwa Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam; mechi namba 35- Simba vs Polisi Dodoma (Septemba 14), mechi namba 29- African Lyon v Yanga (Septemba 15), mechi namba 45- Yanga vs Villa Squad (Septemba 21), mechi namba 66- Simba vs Ruvu Shooting (Oktoba 19) na mechi namba 71- Yanga vs Oljoro JKT (Oktoba 23).

Huku Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ukitumika kwa mechi namba 39- Azam vs Yanga (Septemba 18), mechi namba 50- Simba vs Mtibwa Sugar (Septemba 25), mechi namba 52- Yanga vs Coastal Union (Septemba 28) na mechi namba 58- Yanga vs Kagera Sugar (Oktoba 13).

Nyingine ni mechi namba 62- Simba vs African Lyon (Oktoba 16), mechi namba 65- Yanga vs Toto Africans (Oktoba 20), mechi namba 72- Simba vs JKT Ruvu (Oktoba 22), mechi namba 78- Yanga vs Simba (Oktoba 29) na mechi namba 86- Moro United vs Simba (Novemba 2).
Vikosi
Azam: Mwadini Ally, Erasto Nyoni, Waziri Omari, Said Morad, aggrey Morris, Ibrahimu Mwaipopo, Mrisho Ngasa, Jabir Aziz, John Boko, Kipre Tchetche na Ramadhan Chombo.Simba: Juma Kaseja, Nassoro Said, Amir Maftah, Juma Nyoso,Victor Costa, Partick Mafisango, Amri Kiemba(Shija Mkina/ Uhuru Seleman), Jerry Santo, Gervais Kago, Haruna Moshi, Ulimboka Mwakingwe.

No comments:

Post a Comment