Wednesday, September 7, 2011

Vermaelen aumia tena Arsenal kumkosa kwa wiki 4

Mlinzi wa kati wa Arsenal Thomas Vermaelen hatacheza soka kwa muda unaokisiwa mwezi mmoja baada ya kufanyiwa upasuaji mdogo wa kifundo cha mguu wake wa kushoto.
Thomas Vermaelen
Thomas Vermaelen

Mlinzi huyo mwenye umri wa miaka 25 aliumia wakati wa mechi ya marudiano ya kufuzu kwa Ubingwa wa Ulaya dhidi ya Udinese.
Ni pigo jingine kwa Gunners, ambayo imeuanza msimu kwa kuchechemea na hivi karibuni mchezaji mwengine Jack Wilshere ameumia na hatacheza soka kwa miezi mitatu kutokana na matatizo ya kifundo cha mguu.
Vermaelen msimu mzima uliopita hakucheza kutokana na kuumia kifundo cha mguu mwengine, ambao pia ulifanyiwa upasuaji.
"Haya ni matibabu yanayofanana na aliyopata katika kifundo cha mguu wa kuume mwezi wa Januari mwaka huu na hayahusiani na kuumia kwake kwa msimu uliopita," taarifa ya Arsenal ilifahamisha zaidi.
"Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya mashauriano na daktari bingwa aliyeshauri afanyiwe upasuaji kuzuia tatizo lisiwe la kudumu."
Vermaelen aliumia wakati Arsenal ilipoishinda udinese mabao 2-1 tarehe 24 mwezi wa Agosti na klabu hiyo ilikuwa na matumaini asingehitajika kufanyiwa upasuaji.
Lakini alipasuliwa mjini Stockholm siku ya Jumatatu na sasa atakosa mechi dhidi ya Swansea, Borussia Dortmund, Blackburn, Shrewsbury, Bolton, Olympiakos na Tottenham.
Mlinzi huyo wa zamani wa Ajax hakucheza tarehe 28 mwezi wa Agosti siku Arsenal ilipoadhiriwa na Manchester United kwa kutandikwa mabao 8-2, lakini licha ya kukosa mechi hiyo msimu huu amecheza karibu mechi zote za Arsenal.
Per Mertesacker, aliyejisajili na Arsenal muda mfupi kabla ya kufungwa dirisha la usajili, huenda akaitwa haraka kuziba pengo la Vermaelen, wakati walinzi wengine wa kati Laurent Koscielny, Johan Djourou na Sebastien Squillaci huenda mmoja wao akawa matumaini ya Arsene Wenger kwenye safu ya ulinzi.
Arsenal msimu huu imeshafungwa mabao 11 na hadi sasa inashikilia nafasi ya 17 ya msimamo wa Ligi Kuu ya England ikiwa na pointi moja tu baada ya mechi tatu.

No comments:

Post a Comment