Wednesday, October 19, 2011

Kisa cha Muisraeli aliebadilishwa na wapalestina 1000



Tangu kutekwa kwake mapema Juni 25, 2006, Gilad Shalit aligeuka kuwa ndio turufu kubwa ya kundi la Hamas katika makabiliano yake na Israel.

Kijana huyo aliyekuwa na umri wa miaka 19 alivushwa hadi Gaza baada ya shambulio la Hamas. Israel iliapa kumkomboa bila ridhaa na kuanzisha mashambulio ya kijeshi dhidi ya Gaza.

Lakini hawakufanikiwa kumkomboa. Hamas siku zote ilikua na sharti moja tu - kwamba wafungwa takriban 1500 wa Kipalestinina waachiliwe kutoka jela - wengi wakiwemo waliohusika na mashambulizi mabaya ya mauaji dhidi ya raia wa kawaida.

Na akizungumza mwaka 2007 baba yake Gilad Noam Shalit alikiri kwamba hilo lingekuwa vigumu kwa Israeli kulikubali.

Juhudi za upatanishi ziliongozwa na maafisa wa Ujerumani na Misri.

Masharti ya kimsingi yakabainika wazi na hayatofautiani na mpango huu unaotekelezwa sasa wa kubadilishana wafungwa. Lakini juhudi hizi hazikufua dafu.

Na sababu moja ilikua waziri mkuu wa Israel wakati huo Ehud Olmert alikuwa dhaifu kisiasa hadi kwamba hakuwa na ubavu wa kulazimisha makubaliano.

Lakini kampeni ya kushinikiza Gilad aachiliwe huru ikiongozwa na wazazi wake ilizidi kupata msukumo.

Mapema mwaka 2009 Israeli ilianzisha mashambulio makubwa katika Gaza kwa lengo la kumkomboa Gilad Shalit lakini haikufanikiwa.

Baadae makubaliano yalifikiwa kwa kuachiliwa wafungwa 20 wanawake wa Kipalestina kwa kubadilishana na video ya Gilad ambayo ilithibitisha kuwa yuko hai.

Gilad alionekana amekonda sana ingawa alikuwa na hali nzuri ya afya.

Picha hizo zilisaidia kumfanya awe nembo kubwa zaidi nchini Israel ambayo siku zote imefanya juhudi kubwa za kuhakikisha kwamba inawarudisha wanajeshi wake waliotekwa, hata kama wamerejea maiti.

Lakini msemaji wa waziri mkuu mpya , Benjamin Netanyahu, bado hakutaka kufikiria wazo lolote la kutoa ridhaa kwa kundi la Hamas.

Familia ya Gilad iliimarisha kampeni yake ya kufikiwa makubaliano ya kubadilishana wafungwa wakiungwa mkono na vyombo vya habari vya Israeli na kuendeleza shinikizo kwa kuandamana kutoka nyumbani kwao hadi makao ya Bw Netanyahu.

Hamas nayo haikuonyesha ishara yoyote ya kubadili msimamo wake.

Hatimae ni wazi kabisa kwamba kitu kilichoshawishi serikali ya Israeli na Hamas kwamba makubaliano yangezinufaisha pande zote mbili ni mageuzi makubwa ya kisiasa yaliyotokea Mashariki ya kati mwaka huu.

Pande zote mbili zilikabiliwa na changamoto mpya na zilihitaji angalau kwa sasa kuimarisha umaarufu wao ambao wangeupata kwa kubadilishana wafungwa.

No comments:

Post a Comment