Friday, November 25, 2011

SIMBA Vs AZAM HAPATOSHI FAINALI YA VIJANA LEO KARUME

TIMU za Simba na Azam FC zote za jijini Dar es Salaam, leo zinakutana katika mechi ya fainali inayotarajia kubeba taswira kubwa ya ushindani ya michuno ya Kombe la Vijana chini ya umri wa miaka 20 kwenye Uwanja wa Karume.
Upinzani wa mechi hiyo uko wazi kutokana na ubora ulioonyeshwa na vikosi hivyo mpaka kufikia hatua ya kucheza fainali.
Michuano hiyo maalum kwa ajili ya kukuza vipaji, ilianza wiki mbili zilizopita na kupigwa kwenye viwanja vya Karume na Chamazi kilichopo nje kidogo ya jiji.
Simba ilikata tiketi ya kucheza fainali hizo baada ya kuifunga Toto African kwa mabao 4-1 katika mechi ya nusu fainali. Ushindi huo wa Simba ulikuwa kama kulipa kisasi kwani katika mechi ya kwanza baina ya timu hizo Toto waliifunga Simba bao 1-0.
Kwa upande wa Azam walitinga hatua ya fainali baada ya kuifundisha soka timu ya taifa ya vijana (U-17), Serengeti Boys kwa kuiangushia kipigo cha mabao 3-0.
Timu za Toto African na Serengeti Boys, zitatangulia kushuka dimbani kucheza mechi ya kusaka mshindi wa tatu, ambapo mshindi ataondoka na shilingi 500,000 na medali za Fedha.
Bingwa wa mashindano hayo ya kila mwaka, atajinyakulia shilingi 1.5milioni, Kombe na medali za Dhahabu, huku mshindi wa pili akipata medali za Shaba na kitita cha shilingi 1milioni.
Mbali na hizo pia, kutakuwa na zawadi za Mchezaji Bora atajipatia shilingi 400,000. Mfungaji Bora shilingi300,000, Kipa Bora shilingi 300,000, na timu yenye nidhamu itapata shilingi 300,000.
Makocha wa pande zote mbili Simba na Azam wametamba kila mmoja kwa upande wake kutwaa kombe hilo kulingana na kikosi chake kilivyojiandaa.
Vijana wangu wako kwenye hali nzuri ya pambano hilo na wamenihakikishia kucheza kufa na kupona kutwaa kombe hilo," alisema Seleman Matola kocha wa Simba kama ilivyo kocha wa Azam Iddy Cheche.
Msimu uliopita Ruvu Shooting ndiyo iliyotwaa kombe baada ya kuwafunga 'ndugu' zao JKT Ruvu kwa mabao 2-1 katika mechi ya fainali. Msimu huu mabingwa hao hawakuweza kufua dafu.

No comments:

Post a Comment