Wednesday, November 23, 2011

Tsvangirai aoa mfanyabiashara,Mahari zaidi ya milioni 60 za kitanzania (USD 36,000) na Ng'ombe 10


Tsvangirai na mkewe mtarajiwa Bi Tembo

Waziri Mkuu wa Zimbabwe Morgan Tsvangirai amevunja mwiko kwa kufunga ndoa mwezi Novemba.
Kitamaduni inahofiwa kuwa kufunga ndoa mwezi Novemba kutaletea wanandoa bahati mbaya.

Lakini waziri huyo mkuu amefanya harusi na Locadia Tembo katika sherehe za kikabila siku ya Jumatatu, baada ya kutoa mahari ya dola elfu 36 na ng'ombe 10.

Mke wake wa kwanza, Susan, alifariki katika ajali ya gari muda mfupi baada ya Bw Tsvangirai kuingia katika serikali ya umoja wa kitaifa na Rais Robert Mugabe mwaka 2009.

Viongozi hao wawili walitia saini makubaliano ya kuunda serikali ya pamoja, kufuatia uchaguzi wenye utata ulioghubikwa na ghasia.

Dalili za mwanzo kuwa Bw Tsvangirai anafikiria kufunga ndoa zilikuja wakati wa mkutano wa hadhara wa chama chake cha MDC mwishoni mwa wiki, katika eneo la Chitugwiza, nje kidogo ya jiji la Harare.

Kiongozi huyo wa MDC,59, alifanya mzaha kwa watu waliokusanyika kwa kusema waandishi wa habari wamekuwa wakiandika kuhusu yeye kuwa na marafiki wa kike. "Lakini kwani kapera anakatazwa kufanya hivyo?" alioluza mashabiki wake na kujibiwa kwa kicheko na kupigiwa kofi.

Bi Tembo, 39, ni mfanyabiashara wa bidhaa za rejareja na pia ni dada wa mbunge aliye katika chama cha Mugabe cha Zanu-PF - jambo ambalo limeleta utata kwa baadhi ya wafuasi wa MDC.

Lakini wafuasi wa MDC wanaonekana kufurahishwa na hatua ya kiongozi wao, wakisema kuwa uchaguzi ukiwa umekaribia mwakani, mgombea urais atanufaika kwa kupata msaada kutoka kwa mke wake na mshauri katika kampeni.

Katika mitaa ya Harare kulikuwa na maoni tofauti, hata hivyo wengine wakiwa na wasiwasi kuhusu harusi hiyo ya mwezi Novemba.

"Kama mzee anatakiwa kuongoza kwa mfano - wao ndio wanatuambia tusioe mwezi Novemba," mtu mmoja aliiambia BBC.

Baada ya kutoa mahari, maarufu kama lobola, kwa ndugu wa Bi Tembo katika sherehe ya kitamaduni huko Criston Bank, takriba kilomita 25 kaskazini mwa Harare, Bw Tsvangirai imeripotiwa alitaka ifanyike harusi 'nyeupe' katia kufuata utamaduni.

Ni katika sherehe hizi zinazoegemea zaidi katika utamaduni wa Kizimbabwe, zinatoa dalili kuwa zitafanyika wakati wa mapumziko ya Krismasi.

Jameson Timba, waziri wa nchi katika ofisi ya waziri mkuu, ameiambia BBC kuwa Bw Tsvangirai "atatoa tangazo rasmi kuhusu mipango ya harusi yake wakati utakapowadia".

No comments:

Post a Comment