Monday, February 6, 2012

WEBB aibeba Man United kutoa sare na Chelsea

Howard Webb refa alieibeba Man United

Meneja wa Chelsea, Andre Villas-Boas, amelalamika kuhusiana na uamuzi wa Howard Webb, baada ya timu yake ambayo ilikuwa ikiongoza magoli 3-0, hatimaye ilipotoka sare ya magoli 3-3 na Manchester United katika mechi ya Jumapili.
Chelsea, ikichezea uwanja wa nyumbani wa Stamford Bridge, ilionekana kuelekea kupata ushindi, lakini kufuatia uamuzi wa refa Webb, Wayne Rooney aliweza kufunga magoli mawili ya penalti, na mchezo kubadilika.
Chelsea 3-3 Man United

Sare hiyo imeiwezesha Manchester United kupunguza tofauti kati yake na majirani Manchester City, na ambao wanaongoza ligi, kuwa pointi mbili tu kati yao.
"Penalti ya kwanza ilikuwa ni wazi, na hakuna la kusema, lakini ya pili, ni ya kutiliwa shaka kabisa", alielezea Villas-Boas.
"Sijui kama Howard Webb alikuwa katika nafasi muwafaka ya kuweza kuona vyema na kufanya uamuzi, lakini ni jambo la kutoridhisha kwa yeye kutoa penalti hiyo", alilalamika meneja wa Chelsea.
Villas-Boas aliongezea: "Sijui kama Howard alikuwa analipizia jambo fulani ambalo hakulifanya katika nusu ya kwanza, lakini uamuzi wake haukufaa".
Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson alisisitiza kwamba penalti zote mbili zilikuwa halali, na akielezea kwamba hata walistahili penalti zaidi, baada ya Gary Cahill kugongana na Danny Wellbeck katika kipindi cha kwanza.
"Tungeliweza kupata jumla ya nafasi nne za penalti", alisema.
Katika mchezo wa awali wa Jumapili, Papiss Demba Cisse, aliyesajiliwa na Newcastle, na akicheza mechi yake ya kwanza, aliweza kuifungia timu yake bao, na wakapata ushindi wa magoli 2-1 dhidi ya Aston Villa.
Newcastle sasa imo katika nafasi ya tano katika ligi kuu ya Premier kufuatia ushindi huo.
Cisse alisajiliwa kwa pauni milioni 10.
Mapema mwenzake kutoka Senegal, Demba Ba, alikuwa ameiwezesha timu yake kupata bao la kwanza katika mechi hiyo, lakini Robbie Kean akaisawazishia Villa.

No comments:

Post a Comment