Monday, March 19, 2012

SIMBA S.C NI NOMAAAA YAILIZA MTIBWA 2-1


Siku ya jana ilikuwa mbaya kwa kiungo Patrick Mafisango jana alipiga penalti mara mbili akakosa, lakini bado Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo mkali wa Ligi Kuu ya Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa.
Mafisango alikosa penalti hiyo iliyotokana na mshambuliaji Emmanuel Okwi kuchezewa rafu katika eneo la hatari katika dakika ya 59. Alipiga mara ya kwanza akakosa lakini mwamuzi akaamuru irudiwe kwa madai ya kipa kuvuka mstari, hata hivyo alipopiga tena Deogratius Munishi ambaye ni kipa wa zamani wa Simba akadaka tena.
Katika mchezo huo, Simba walipata bao katika dakika ya 18 lililofungwa na Mafisango baada ya kuitumia vizuri krosi ya Okwi. Mtibwa Sugar walirejea kwa kasi katika kipindi cha pili na kufanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 52 kupitia kwa Hussein Javu aliyepiga shuti kali nje kidogo ya eneo la hatari.
Huku timu zote zikionekana kushambuliana kwa zamu, walikuwa ni Simba waliofanikiwa kutikisa nyavu za wapinzani wao baada ya mshambuliaji mrefu, Felix Sunzu kufunga kwa kichwa akipokea mpira wa faulo iliyopigwa na Okwi.
Mtibwa ndiyo waliowahi kulisakama lango la Simba katika dakika ya tatu. Mshambuliaji wa timu hiyo, Javu alibaki yeye na mlinda mlango Juma Kaseja lakini akashindwa kuutumbukiza mpira wavuni.
Beki wa Simba, Mkenya, Derrick Walulya, jana alicheza mechi yake ya kwanza ya ligi tangu asajiliwe na Wekundu wa Msimbazi, Januari, mwaka huu, ingawa alilaumiwa na wachezaji wenzake uwanjani kwa kuonekana kuwa uchochoro, alijitahidi kwa kiasi chake.
Baada ya mchezo huo, Kocha wa Simba, Milovan Cirkovic, aliwapongeza wachezaji wake kwa kucheza vizuri huku akiuponda Uwanja wa Jamhuri kwamba hauna ubora, wakati Kocha wa Mtibwa, Tom Olaba alimshutumu mwamuzi kwa kushindwa kuchezesha vizuri pambano hilo.
Katika michezo mingine iliyopigwa jana, Azam iliifunga Ruvu Shooting kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam, wakati Toto African ilifufua matumaini yake ya kubaki ligi kuu kwa kuibamiza Polisi kwa mabao 2-1 katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

No comments:

Post a Comment