Thursday, July 26, 2012

VIGOGO WAGAWANA VIWANJA DAR,WALALAHOI WACHINJIWA BAHARINI

MANISPAA ya Temeke imetoa orodha ya majina ya wananchi waliopewa viwanja katika manispaa hiyo, ambayo inaonyesha kuwamo kwa vigogo wanaojumuisha mawaziri, wabunge, watendaji wakuu wa Serikali pamoja na baadhi ya watoto wa vigogo hao.Katika orodha hiyo, jumla ya watu 1,800 walipatiwa viwanja hivyo, huku majina hayo ya vigogo yakiwa ni zaidi ya 50, ambao baadhi wamejiandikisha wenyewe, wengine wake zao, ndugu na watoto wao.
Orodha ya Vigogo hao iliyobandikwa katika ofisi za manispaa ya Temeke gazeti la Mwananchi 25 Julai 2012 limeyanyaka kama ifuatavyo;

Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama; Naibu Spika, Job Ndugai; Waziri wa Mawasiliano, Sanyansi na Teknolojia, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima.

Kwa upande wa Makatibu Wakuu wa Wizara wapo, Dk Florence Turuka (Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia), Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Ramadhan Kijjah; Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Omary Chambo na Dk Idris Rashid ambaye ni Gavana wa Zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Pia wamo Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi, Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Slaa; Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Suleinan Kova.

Wengine ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Haruna Masebu; Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh na Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili(MNH),Marina Njelekela.

Kwa upande wa wabunge wamo Dk Augustine Mrema (Vunjo - TLP), Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe; Mbunge wa Kibaha Mjini (CCM), Sylvester Koka; Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan; Mbunge wa Moshi Vijijini (CCM), Dk Cyril Chami na Mbunge wa Singida Kusini (CCM), Mohamed Misanga.
Wengine ni Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila; Mbunge wa Igunga (CCM), Dk Peter Kafumu na Mbunge wa Bukene (CCM), Seleman Zedi.

Wabunge wa Viti Maalumu (Chadema), Maulida Komu na Suzan Lyimo, Viti Maalumu CCM, Dk Mary Mwanjelwa na Zakhia Meghji ambaye ni mbunge wa kuteuliwa.

Orodha hiyo pia inaonyesha majina ya ukoo yanayofanana na majina ya baadhi ya viongozi ambao ni Miraji Kikwete, Khalfan Kikwete, Juanita Mramba, Suzan Mkapa, Zainab Mkomwa, George Rupia, Maimuna Mfutakamba, Mary Membe, Pharles Ngeleja, Judith Kahama na Wilfred Mwanri.

Mkurugenzi apepesa macho na kung'ata maneno ashindwa kutoa maelezo yaliyonyooka
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Magreth Nyalile alipoulizwa kuhusu orodha hiyo alisema kuwa, majina hayo hajayaona na kwamba waliobandika wamefanya uamuzi huo bila ya yeye kuupitia.

Majina yenyewe sijayaona, hivyo basi siwezi kujua ni kina nani waliopewa viwanja hivyo, kwa sababu wako zaidi ya 1,000, jambo ambalo litakuwa vigumu kwangu kubaini tatizo hilo,” alisema Nyalile.

Aliongeza kuwa, kutokana na hali hiyo hawezi kusema lolote kwa sababu yuko nje ya ofisi kwa ajili ya shughuli nyingine za ujenzi wa taifa.

Hata hivyo, Nyalile alisema mchakato wa ugawaji wa viwanja hivyo ulifuata taratibu za kisheria na kwamba hakuna mtu au kiongozi yeyote aliyependelewa, jambo ambalo linaweza kusababisha mgongano wa hapa na pale.

Nyalile alisema kuwa kama kuna viongozi walipewa kwa njia zisizo sahihi, au kwa rushwa wakati wa uwasilishaji wa majina hayo, walipaswa kutoa taarifa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

No comments:

Post a Comment