Monday, August 6, 2012

SIMBA KUTEMBELEA YATIMA NA WAGONJWA KUELEKEA SIMBA DAY

Simba Sports Club
KIKOSI kizima cha wachezaji wa Simba SC, leo kinatarajiwa kutembelea kituo cha watoto yatima cha Maungu Orphanage Center, kilichopo Kinondoni Mkwajuni, Dar es Salaam katika mfululizo wa Wiki ya Simba na Jamii, kuelekea tamasha la kuazimisha kuzaliwa kwa klabu hiyo, Simba Day, Agosti 8, mwaka huu.

Wachezaji wa Simba, wanatarajiwa kujumuika na watoto hao, wanaoishi katika mazingira magumu na kuwafariji sambamba na kuwapa zawadi mbalimbali.

Ratiba inaonyesha kesho Simba watatembelea wagonjwa katika hospitali ya Mwananyamala mjini Dar es Salaam na keshokutwa ndipo litafanyika Tamasha la Simba Day, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika tamasha hilo, litakalotanguliwa na burudani mbalimbali, litafuatiwa na utambulisho wa wachezaji wote wa kikosi cha msimu ujao cha Simba SC wakiwemo Mrisho Khalfan Ngassa aliyesajiliwa kutoka Azam FC, Mbuyu Twite kutoka APR ya Rwanda na wengineo.

Baada ya utambulisho, Simba itacheza mechi ya kirafiki na timu ambayo hadi sasa haijatajwa ingawa wachunguzi wa mambo wamefunguka kuwa klabu ya Simba ipo kwenye mawasiliano na Nairobi City Stars ya Kenya.

Siku inayofuata, yaani Agosti 9, Simba watatembelea shule ya msingi Mgulani,ili kuhamasisha michezo mashuleni na Agosti 10, mabingwa hao wa Tanzania, watahitimisha wiki ya Simba na Jamii, kwa kutembelea kiwanda cha Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kilichopo Ilala, Dar es Salaam.

TBL ndio wadhamini wakuu wa Simba SC, kupitia bia yao ya Kilimanjaro Premium Lager, ambayo pia ndio imedhamini Wiki nzima ya Simba na Jamii, kuanzia kwenye Mkutano Mkuu wa mwaka wa klabu hiyo, jana Bwalo la Maofisa wa jeshi la Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam,



RATIBA YA WIKI YA SIMBA KWA JAMII:

Agosti 5, 2012: Mkutano Mkuu wa mwaka Simba SC (Polisi Oystrebay)

Agosti 6, 2012: Kutembelea watoto yatima Maungu Orphanage Center, K’ndoni Mkwajuni

Agosti 7, 2012: Kutembelea wagonjwa Mwananyamala hospitali

Agosti 8, 2012: Simba Day (Uwanja wa Taifa, burudani na mechi)

Agosti 9, 2012: Kutembelea shule ya msingi Mgulani kuhamasisha michezo mashuleni

Agosti 10, 2012: Kutembelea kiwanda cha TBL Ilala

No comments:

Post a Comment