Thursday, December 6, 2012

NI KITIMTIM NUSU FAINALI TUSKER LEO, TANZANIA MACHO KWA USO NA UGANDA,ZANZIBAR USO KWA MACHO NA KENYA


MABINGWA watetezi, Uganda na jirani zao Kenya watakuwa na kibarua kizito mbele ya Tanzania Bara na Zanzibar kwenye nusu fainali itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Nambolee, Kampala.

Uganda 'The Cranes' ilikata tiketi hiyo baada ya kuwafunga Ethiopia mabao 2-0, huku Harambee Stars ikiwalaza Malawi kwa bao 1-0.

Awali katika mechi ya robo fainali iliyochezwa mwanzoni, kiungo wa zamani ya Yanga na Simba, Mike Baraza aliiyeingia akitokea benchi aliifungia Kenya 'Harambee Stars' bao pekee katika dakika ya 57 baada ya kuunganisha kwa kichwa shuti la mbali mita 25 la Abdalla Juma na kumpoteza kipa wa Malawi, Charles Swini.

Kwa ushindi huo sasa Harambee Stars watakuwa na kibarua kigumu mbele ya Zanzibar Heroes inayosaka ubingwa wa pili wa michuano hiyo tangu walipofanya hivyo mwaka 1995 hapo Uganda.

Wakati huo huo;Kocha wa Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen amemsifia kiungo wake Mwinyi Kazimoto kwa kusema ni mchezaji mwenye akili nyingi na mchezeshaji bora kabisa.

Kauli hiyo ya Poulsen imekuja baada ya Mwinyi kutoa pasi zote mbili zilizozaa mabao mawili yaliyoipa Stars ushindi wa mabao 2-0 katika pambano la robo fainali dhidi ya Rwanda.

Kim alisema kuwa Kazimoto ni kiungo kikuu cha matokeo mazuri ya timu yake kutokana na aina ya uchezaji wake aliodai ni wa kutumia akili zaidi.

No comments:

Post a Comment