Thursday, September 8, 2011

SIMBA DOZI NZITO YANGA HOI BIN TAABAN

MABINGWA watetezi Yanga wameendelea kung'ang'ania mkiani mwa Ligi Kuu huku mahasimu wao Simba wakipata ushindi wa tatu mfululizo kwenye ligi hiyo katika mechi zilizofanyika jana kwenye viwanja vya Jamhuri, Morogoro na Mkwakwani, Tanga.

Yanga walishuka kwenye Uwanja wa Jamhuri wakiwa na matumaini ya kupata pointi tatu, lakini walijikuta wakilazimishwa suluhu na Mtibwa Sugar, wakati Gervas Kago alifunga bao lake la kwanza tangu aanze kuichezea Simba na kuiwezesha timu hiyo kuilaza Villa Squad bao 1-0, huku Polisi Dodoma wakitoka suluhu na Ruvu Shooting.

Kwa matokeo hayo Simba imefikisha pointi tisa na kupanda hadi nafasi ya pili nyuma ya kinara wa ligi JKT Ruvu kwa tofauti ya mabao.Mabingwa wa Kombe la Kagame Yanga waliokusanya pointi mbili katika michezo mitatu ya ligi waliyocheza mpaka sasa walilazimika kubaki ndani ya uwanja wa Jamhuri kwa dakika tano na kuondolewa na ulinzi mkali wa polisi FFU baada ya mashabiki wao wenye hasira kuanza kurushia mawe basi lililobeba wachezaji hao.

Kocha Sam Timbe akizungumzia pambano hilo alisema vijana wake walishindwa kutumia nafasi walizopata kwenye mchezo huo.

Mkenya Tom Olaba aliyeiwezesha Mtibwa Sugar kufikisha pointi nane mpaka sasa aliwapongeza wachezaji wake kwa kucheza vizuri na kutawala sehemu ya kiungo, lakini walipoteza nafasi chake walizopata.Mtibwa ilianza mchezo huo kwa kasi na katika dakika ya 17, kipa Yaw Berko alifanya kazi ya ziada kuokoa shuti la Said Mkopi.

Yanga ikicheza bila ya nahodha wake,  Shadrack Nsajigwa ilionekana kupwaya katika kiungo na kuruhusu mashambulizi mengi golini kwake shukrani kwa juhudi binafsi za kipa Berko.

Mshambuliaji Thomas Mourice wa Mtibwa Sugar alipoteza nafasi ya kufunga katika dakika ya 40 kwa kushindwa kuunganisha vema krosi ya upande wa kushoto iliyopigwa na Said Bahanunzi.

Washambuliaji wa Yanga, Davis Mwape na  Jerryson Tegete walikosa mabao katika dakika ya 29 na 42 waliposhindwa kutumia nafasi zilizotengenezwa na winga Julius Mrope.

Mshambuliaji wa Ghana, Kenneth Asamoah alishindwa kumalizia mpira wa kona uliopigwa na Rashid Gumbo na kutemwa na kipa Munishi katika dakika ya 70.

Tanga; Mabingwa wa Ngao ya Jamii, Simba wamedhamiria kurudia rekodi yao ya msimu wa 2009/10 waliotwaa ubingwa bila ya kupoteza mchezo wowote baada ya kuichapa Villa Squad bao 1-0.

Mshambuliaji wa kimataifa wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Kago alifunga bao lake la kwanza Ligi Kuu ya Tanzania katika dakika ya 7 akipokea krosi ya Haruna Moshi na kuipa Simba ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Villa Squad.

Katika mchezo huo beki Victor Costa alifanya kazi ya ziada kuokoa bao lililotaka kufungwa na Mohamed Kijuso katika dakika za mwisho kwa mpira wa kichwa uliompotea kipa Juma Kaseja.

Pia winga wa Simba, Ulimboka Mwakingwe alipewa kadi ya njano kwa kujiangusha kwenye eneo la penalti, huku Amri Ramadhan wa Villa Squad akipewa kadi ya njano kwa kuushika mpira kwa makusudi.

VIKOSI

Yanga: Yaw Berko, Godfrey Taita, Oscar Joshua, Bakari Mbegu, Chacha Marwa, Nurdin Bakari, Julius Mrope, Rashid Gumbo, Jerryson Tegete (Kenneth Asamoah), Davis Mwape, Kigi Makassi (Idrissa Rashid).
Mtibwa Sugar: Deogartius Munishi, Juma  Abdul, Issa Rashid, Salvatory Ntebe, Salum Sued, Shabaan Nditi, Said Mkopi, Masoud Ali, Said Bahanunzi, Thomas Mourice na Ali Mohamed.
Simba: Juma Kaseja, Nasoro Chollo, Amir Maftah, Juma Nyoso, Victor Costa, Jerry Santo, Shija Mkina, Amri Kiemba, Gervas Kago, Haruna Moshi na Ulimboka Mwakingwe.
Villa Squad: Abbas Nassoro, Haruna Shamte, Yassin Majota, Shai Mpala, Menard Mbugunza, Zuberi Dadi, Lameck Mbonde, Mussa Nampaka, Mohamed Kijuso, Mohamed Binslum na Nsa Job.

SITA WASHIKILIWA KWA MAUAJI YA SHABIKI WEMBLEY

Shabiki wa soka wa Wales aliyekufa kabla ya pambano dhidi ya England katika uwanja wa Wembley, ametajwa na mashabiki wenzake kuwa ni Mike Dye, na watu sita wanashikiliwa na polisi kutokana na kifo chake.
Polisi uwanja wa Wembley wakichunguza mauaji
Polisi uwanja wa Wembley wakichunguza mauaji


Dye mwenye umri wa miaka 44 alipelekwa hospitali akiwa na majeraha kichwani baada ya kupatwa na maradhi ya moyo nje ya uwanja.
Salamu za rambirambi kwa shabiki huyo wa soka wa klabu ya Cardiff City, aliyefariki dunia usiku wa saa tatu zilitolewa kupitia mtandao wa soka.
Watu hao sita waliokamatwa inaaminika ni mashabiki wa Wales na polisi hawaamini kama kuna shabiki yeyote wa England alihusika na kifo hicho.
Katika taarifa kupitia mtandao wake klabu ya Cardiff City imesema: "Usiku wa Jumanne taarifa zilitufikia kuhusiana na msiba huu ambapo shabiki wa Wales na Cardiff City amekufa katika mechi baina ya England na Wales.
Msemaji wa polisi amesema: "Maafisa wa polisi na wa Huduma za gari la Wagonjwa walimhudumia shabiki huyo. Mtu huyo anayeaminika kuwa na umri miaka 40 alipelekwa hospitalini kaskazini mwa London akiwa na majeraha kichwani. Alitangazwa amekufa saa mbili na dakika hamsini.
England katika mechi hiyo ya kuwania kufuzu katika Ubingwa wa Ulaya, ilishinda kwa bao 1-0.

NIGER YAKANA KUMPA HIFADHI GADAFFI

Serikali ya Niger imesema kuwa itaamua jinsi ya kumshughulikia Kanali Muamar Gaddafi iwapo ataingia nchini humo kuomba hifadhi ya kisiasa.
Kanali Gadaffi
Kanali Gadaffi

Ripoti kutoka eneo hilo zinasema kuwa maafisa wa vyeo vya juu katika Serikali iliyotimuliwa wamewasili nchini Niger na kuna habari kuwa huenda Kanali Gaddafi akajiunga nao.
Baraza la Kitaifa la Mpito la Libya limetoa wito kwa Serikali ya Niger isimpe hifadhi Kanali Gaddafi.
Mwandishi wa Habari wa BBC nchini Libya anasema kuwa ombi hilo limeweka Niger katika hali ya kutatanisha kwa sababu tayari imetambua serikali ya mpito lakini haiwezi kumfukuza Kanali Gaddafi kwa sababu ya uhusiano wa karibu waliokuwa nao viongozi hao wa Niger.
Kiongozi wa Baraza la mpito nchini Libya
Kiongozi wa Baraza la mpito nchini Libya

Wakati huo huo Kanali Gadafi amepuuza madai kwamba ametorokea nchi jirani ya Niger na kuyataja madai hayo kama uongo na vita vya kiakili.
Matamshi ya Gadaffi yamepeperushwa na kituo kimoja cha televisheni nchini Syria, kilichodai kuwa Gadaffi baado yuko nchini Libya.
Gadafi ameapa kuwashinda wapiganaji wa upinzani wanaoungwa mkono na majeshi ya muungano wa NATO.
Huu ndio ujumbe wake wa kwanza katika kipindi kirefu.
Ripoti zinasema katika muda wa siku 10 zilizopita, maafisa wakuu wa uliokuwa utawala wa gadaffi wamekuwa wakiwasili nchini Niger na kuibua fununu kuwa Kanali Gadaffi huenda akajaribu kujumuika nao.
Baraza la kitaifa la mpito nchini Libya limetoa wito kwa Niger kutompa hifadhi. Serikali ya Niger imesema kwamba itaamua jinsi itakavyomshughulikia Kanali muammar gadaffi ikiwa ataingia nchini humo na kuomba hifadhi.

Wednesday, September 7, 2011

LIGI KUU YA VODACOM KUTIMUA VUMBI LEO SIMBAvsVILLA,YANGAvsMTIBWA

Ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara itaendelea tena leo katika michezo kadhaa ambapo MABINGWA watetezi wanaoshikilia mkia katika Ligi Kuu hiyo watoto wa jangwani Yanga watakuwa na kibarua kigumu leo mbele ya Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Jamhuri Morogoro, huku Simba wakiwakaribisha Villa Squad kwenye Uwanja wa Mkwakwani katika muendelezo wa ligi hiyo.

Lakini wakati mikikimikiki ya Ligi Kuu ya Bara ikizidi kushika kasi kwenye viwanja mbalimbali nchini, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jana limeifanyia mabadiliko ratiba ya ligi hiyo kufuatia Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha kutakiwa kutumika kwa shughuli za dini na mashindano ya riadha ya Safari International Marathon.

Kutokana na mabadiliko hayo mechi kati ya JKT Oljoro na Azam imesogezwa mbele na sasa itachezwa keshokutwa Ijumaa mjini Arusha.

Baada ya mapumziko Yanga wanashuka dimbani wakiwa na kumbukumbu mbaya ndani ya uwanja wa Jamhuri kwa kufungwa na JKT Ruvu na Moro United iliyowapa pointi moja mkiani, huku nje ya uwanja uongozi wa klabu hiyo kongwe upo njia panda baada ya mahakama kutaka uondolewe.

Kocha wa Yanga, Sam Timbe na vijana wake wanajua ushindi wa leo dhidi ya Mtibwa Sugar utarudisha hali ya utulivu ndani ya klabu ya Yanga inayoshikilia mkia wa ligi pamoja na kuwa na kikosi kilichojaa nyota kutoka kona zote za Afrika.

Mganda Timbe anajua mara mbili alinusurika kipigo kutoka kwa mashabiki kwenye uwanja huo hivyo analazimika kupigana kurudisha heshima yake.

"Sina wasiwasi na mchezo huo tumeshafanya marekebisho matatizo madogo madogo yaliyojitokeza katika michezo ya nyuma, lakini hiyo ilitokana na kuwa na majeruhi wengi.

Naye kocha msaidizi wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime alisema wamejipanga vyema katika mchezo wao wa leo dhidi ya mabingwa hao na wanategemea matokeo mazuri ili waendelee kujitengenezea mazingira mazuri ndani ya msimamo wa ligi hiyo.

Mtibwa ina pointi saba wakiwa nafasi ya pili katika msimamo wa ligi na imepania kuendeleza rekodi ya ushindi katika mchezo wa leo baada ya kuifunga Toto African ya Mwanza mabao 3-2 katika mchezo wao uliopita ikiwa nyumbani.

Jijini Tanga mabingwa wa Ngao ya Jamii, Simba walioanza msimu kwa kishindo kikubwa watakuwa na kazi nyepesi dhidi ya Villa Squad timu yenye rekodi ya utovu wa nidhamu kwa kuwa na kadi 12, moja nyekundu na njano 11 katika msimu huu.

Mshambuliaji Mohamed Kijuso wa Villa atakuwa na kazi ya kumthibishia kocha Moses Basena wa Simba kwamba alifanya kosa kumtoa kwa mkopo msimu huu.

Kijuso mwenye mabao mawili hadi sasa akisaidiana na Nsa Job watakuwa na kazi nzito mbele ya ukuta imara wa Simba chini Victor Costa na Juma Nyoso pamoja na kipa Juma Kaseja mwenye nia ya kuendeleza rekodi yao ya kutoruhusu bao.

Safu ya ushambuliaji wa Simba itamkosa Felix Sunzu,mzambia huyo anayetumikia adhabu ya kutocheza mechi tatu na Salum Machaku majeruhi, huku Emmanuel Okwi akiitumikia timu yake ya taifa Uganda kwenye Michezo ya Afrika nchini Msumbiji.

Kocha Basena atalazimika kubadili mfumo wa ushambuliaji leo kwa kuwatumia  Ulimboka Mwakingwe, Gervais Kago wakiunganishwa na Haruna Moshi"Boban".

 TFF imefanya mabadiliko ya ratiba ya ligi hiyo kwa mara nyingine kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Hahari wa shirikisho hilo Boniface Wambura.

Mabadiliko ya ratiba yanahusisha mechi zifuatazo na tarehe mpya zikiwa katika mabano; Septemba 7 mwaka huu mechi namba 20- Oljoro JKT vs Azam (Septemba 9), Septemba 10 mwaka huu mechi namba 22- Azam vs Simba (Septemba 11), Septemba 11 mwaka huu mechi namba 26- Ruvu Shooting vs Yanga (Septemba 10).

Septemba 17 mwaka huu mechi namba 38- Oljoro JKT vs African Lyon (Septemba 19), Septemba 21 mwaka huu mechi namba 43- Kagera Sugar vs Oljoro JKT (Septemba 22), Septemba 21 mwaka huu mechi namba 49- Ruvu Shooting vs African Lyon (Septemba 20) na Septemba 24 mwaka huu mechi namba 54- Toto Africans vs Oljoro JKT (Septemba 25).


Vermaelen aumia tena Arsenal kumkosa kwa wiki 4

Mlinzi wa kati wa Arsenal Thomas Vermaelen hatacheza soka kwa muda unaokisiwa mwezi mmoja baada ya kufanyiwa upasuaji mdogo wa kifundo cha mguu wake wa kushoto.
Thomas Vermaelen
Thomas Vermaelen

Mlinzi huyo mwenye umri wa miaka 25 aliumia wakati wa mechi ya marudiano ya kufuzu kwa Ubingwa wa Ulaya dhidi ya Udinese.
Ni pigo jingine kwa Gunners, ambayo imeuanza msimu kwa kuchechemea na hivi karibuni mchezaji mwengine Jack Wilshere ameumia na hatacheza soka kwa miezi mitatu kutokana na matatizo ya kifundo cha mguu.
Vermaelen msimu mzima uliopita hakucheza kutokana na kuumia kifundo cha mguu mwengine, ambao pia ulifanyiwa upasuaji.
"Haya ni matibabu yanayofanana na aliyopata katika kifundo cha mguu wa kuume mwezi wa Januari mwaka huu na hayahusiani na kuumia kwake kwa msimu uliopita," taarifa ya Arsenal ilifahamisha zaidi.
"Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya mashauriano na daktari bingwa aliyeshauri afanyiwe upasuaji kuzuia tatizo lisiwe la kudumu."
Vermaelen aliumia wakati Arsenal ilipoishinda udinese mabao 2-1 tarehe 24 mwezi wa Agosti na klabu hiyo ilikuwa na matumaini asingehitajika kufanyiwa upasuaji.
Lakini alipasuliwa mjini Stockholm siku ya Jumatatu na sasa atakosa mechi dhidi ya Swansea, Borussia Dortmund, Blackburn, Shrewsbury, Bolton, Olympiakos na Tottenham.
Mlinzi huyo wa zamani wa Ajax hakucheza tarehe 28 mwezi wa Agosti siku Arsenal ilipoadhiriwa na Manchester United kwa kutandikwa mabao 8-2, lakini licha ya kukosa mechi hiyo msimu huu amecheza karibu mechi zote za Arsenal.
Per Mertesacker, aliyejisajili na Arsenal muda mfupi kabla ya kufungwa dirisha la usajili, huenda akaitwa haraka kuziba pengo la Vermaelen, wakati walinzi wengine wa kati Laurent Koscielny, Johan Djourou na Sebastien Squillaci huenda mmoja wao akawa matumaini ya Arsene Wenger kwenye safu ya ulinzi.
Arsenal msimu huu imeshafungwa mabao 11 na hadi sasa inashikilia nafasi ya 17 ya msimamo wa Ligi Kuu ya England ikiwa na pointi moja tu baada ya mechi tatu.

Tuesday, September 6, 2011

UEFA YAMKOMALIA WENGER KUKOSA MECHI MBILI

Meneja wa Arsenal Arsene Wenger rufaa yake ya kuzuiwa na Uefa kukaa katika benchi la ufundi la timu hiyo katika mechi za Ubingwa wa Ulaya imegonga mwamba.
Arsene Wenger
Arsene Wenger

Wenger aliadhibiwa baada ya kupatikana na hatia ya kuwasiliana na benchi la ufundi la Arsenal wakati akitumikia adhabu ya kukaa kwenye benchi la ufundi mwezi wa Agosti wakati timu yake ilipoilaza Udinese bao 1-0.
Arsenal pia imepigwa faini ya euro 10,000 sawa na paundi 8,700 kutokana na utovu wa nidhamu.
Wenger sasa ataiangalia timu yake akiwa jukwaa la watazamaji kwa mechi za makundi mwezi wa Septemba dhidi ya Borussia Dortmund na Olympiakos.
Meneja huyo wa The Gunners aliaamini hakufanya kosa baada ya klabu kumwambia anaweza kutuma ujumbe kwa msaidizi wake Pat Rice kupitia kwa kocha katika mechi ya mkondo wa kwanza ya Arsenal ya kufuzu dhidi ya Udinese katika uwanja wa Emirates. Wakati huo aliambiwa wakati wa mapumziko hakuwa ameruhusiwa kufanya hivyo.
Wenger baadae alisema inakera kwa vile klabu iliiuliza Uefa kabla ya mechi kwa ajili ya ufafanuzi wa kanuni na yeye alikuwa anazifuata.
Klabu ya Arsenal ilikata rufaa dhidi ya adhabu hiyo na Uefa ikaafiki kuweka kando uamuzi wake hadi baada ya mechi ya pili ya marudiano ambapo Arsenal ilifanikiwa kusonga mbele katika hatua ya makundi

SONG LA LEO