Wednesday, October 19, 2011

Bondia David Haye atangaza kustaafu kuzichapa

David Haye, bondia wa Uingereza aliyekuwa bingwa wa zamani wa mkanda wa WBA, ametangaza kustaafu kutoka masumbwi.
Vladimir Klitschko na David Haye
Wladimir Klitschko na David Haye (kulia)
Haye, ambaye Alhamisi ametimia umri wa miaka 31, mara nyingi alinukuliwa akisema kwamba asingelipenda kupigana mara tu atakapotimia umri wa miaka 30.
Pambano la mwisho la Haye lilikuwa ni dhidi ya mpinzani Wladimir Klitschko wa Ukraine, tarehe 2 Julai, alipopoteza ubingwa wa mkanda wa WBA mjini Hamburg.
Awali kulikuwa na gumzo kuhusu matazamio ya Haye kurudi ulingoni na kupigana na Vitali, ambaye ni kakake Wladimir, mwaka 2012, licha ya habari za Jumanne kwamba bondia huyo wa London kamwe hakuwa na nia ya kuomba leseni mpya ya kuendelea na ndondi, leseni ambayo itakwisha mwezi Desemba.
Haye, ambaye alifanikiwa kusonga kutoka uzani wa cruiser hadi ule wa heavy, alipoteza ubingwa wake katika pambano la kujaribu kuwa bingwa wa kumiliki mikanda yote, baada ya kupigwa na Wladimir, ambaye alimshinda kwa pointi, na kutwaa ubingwa wa WBO, IBF na IBO.
Baadaye, Haye alidai alipigwa kutokana na maumivu ya kidole cha mguu ambacho kilikuwa kimevunjika.
Muingereza Haye alipata mkanda wa WBA baada ya kumshinda bondia wa Urusi, Nikolay Valuev kwa pointi nchini Ujerumani, mwezi Novemba, mwaka 2009.
Haye, ambaye alishindwa mara mbili tu katika mapambano 27 ya kulipwa, kisha aliweza kuutetea ubingwa wake kwa kumpiga Mmarekani John Ruiz katika ulingo wa mjini Manchester, Uingereza, mwezi Aprili, mwaka 2010.

No comments:

Post a Comment