Monday, November 7, 2011

Bolton yafanya maangamizi,Tottenham yailowesha Fulham

Bolton yazinduka kutoka usingizini

Chris Eagles na Ivan Klasnic walipachika mabao mawili kila mmoja wakati Bolton ilipoisasambua Stoke City na kuweza kupata ushindi wao wa kwanza nyumbani msimu huu na kujiondoa katika mizizi ya msimamo wa ligi
Kevin Davies alifunga bao la kwanza lililoonekana ni la utata ndani ya sekunde 90 baada ya kupigwa free-kick ya haraka na Klasnic.

Bolton vs Stoke City
Eagles alipachika bao la pili kwa mkwaju maridadi baada ya Asmir Begovic kushindwa kuweka mpira wavuni.

Klasnic alifumua mkwaju mkali umbali wa yadi 18 na kuandika bao la tatu kabla ya Eagles kufunga bao la nne na Klasnic akapachika bao la tano kwa kichwa na kukamilisha kazi ya ushindi maridadi.

Matokeo hayo yalikuwa ni nafuu kwa Bolton ambayo imeanza msimu huu kwa kusuasua.

Wolves nayo ilimaliza ukame wa kukosa ushindi kwa mara ya nane mfululizo baada ya kuilaza Wigan mabao 3-1.

Walikuwa Wolves walioanza kuliona lango la wageni wao Wigan katika dakika ya 31 kwa bao la Jamie O'Hara baada ya kuunganisha pasi kutoka kwa Kevin Doyle.

Lakini Ben Watson aliisawazishia Wigan, baada ya kuunganisha mpira uliookolewa na mlinda mlango Wayne Hennessey ambaye awali aliokoa mkwaju wa penalti.

David Edwards aliihakikishia mwendo mzuri Wolves kwa kuandika bao la pili kwa mkwaju wa karibu na Stephen Ward akahitimisha mabao kwa kufunga bao la tatu.

Ushindi huo ni mzuri kwa Wolves ambao wananuia kujinasua kutoka eneo la kushuka daraja.

Lakini Wigan inaendelea kubakia mkiani mwa msimamo wa ligi na wamo katika matatizo makubwa baada ya kuweka rekodi mpya ya klabu hiyo ya kushindwa michezo minane mfululizo katika Ligi Kuu ya England. Hakuna timu ambayo ilikuwa na rekodi kama hiyo na ikaweza kuepuka kushuka daraja.


Tottenham imeweza kucheza mechi yao ya kwanza ya ligi bila ya meneja wao Harry Redknapp na kufanikiwa kupata ushindi murua katika uwanja wa Fulham kwa kuilaza mabao 3-1 ukiwa ni ushindi wao wa nane mfululizo wa ligi msimu huu.

Redknapp hakuwepo uwanjani wakati huu akiwa anaendelea kujiuguza nyumbani kwake baada ya kufanyiwa upasuaji mdogo wa moyo mapema wiki hii.

Gareth Bale alikuwa wa kwanza kuifungia Tottenham bao la kwanza baada ya kufumua mkwaju mkali uliomchanganya mlinzi wa Fulham Chris Baird kabla ya Aaron Lennon kufunga bao maridadi la pili baada ya kuipangua ngome ya Fulham.

Fulham walipata bao lao moja baada ya mlinzi wa Tottenham Younus Kaboul kujifunga mwenyewe, kabla Jermain Defoe kuithibitishia ushindi timu hiyo kwa kuandika bao la tatu.

No comments:

Post a Comment