Tuesday, November 1, 2011

SIMBA S.C KULIPIZA KUMALIZA HASIRA KWA MORO UNITED KESHO?

Timu ya Simba inayoongoza ligi kuu Tanzania bara wana nafasi kubwa ya kupoza moto unaoendelea kufukuta kwenye jeraha la kichapo cha bao 1-0 toka kwa mtani Yanga Jumamosi iliyopita, lakini iwapo tu watatumia dakika 90 kupata ushindi katika mechi yao kesho ya kufunga duru la kwanza dhidi ya Moro United kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kocha wa Simba Mganda, Moses Basena alikitupia lawama kikosi chake, hasa safu ya ushambuliaji akilaumu kwa matumizi mabaya ya nafasi nyingi za kufunga walizopata bila kutumia kwenye mechi dhidi ya Yanga.

Lakini jana alisema kikosi chake kipo kwenye hali nzuri na tayari ameshafanya marekebisho kadhaa yaliyotokana na mapungufu ya mechi iliyotangulia."Kikubwa kwetu ni kushinda mchezo huo na kufikisha pointi 30 katika mzunguko huu wa kwanza wa Ligi Kuu," alisema Basena.

"Nafikiri tutakuwa tumejiweka kwenye nafasi nzuri ya mbio za kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu," aliongeza.Alisema haoni sababu ya kukumbuka kufungwa na Yanga isipokuwa akili yake kwa sasa ameiweka zaidi kwenye mbio za kutwaa ubingwa wa ligi.

"Nimewataka wachezaji kutulie na kusahau yaliyowapata Jumamosi iliyopita na kuweko akili na nguvu kwenye mchezo wa kesho dhidi ya Moro United," alisema Basena.Naye kocha wa Moro United, Hassan Banyai alisema wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaishinda Simba kwenye pambano na kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi hiyo.

"Nashukuru kurejea kwa beki wangu wa kati ambaye alikuwa anatumikia adhabu ya kadi, Tumba Sued," alisema Banyai."Naamini uwepo wake utaimarisha zaidi safu ya ulinzi ya timu yangu pia kuongeza imani kwa wachezaji wengine uwepo wake," aliongeza."Tumba ni mchezaji ambaye ana uzoefu mkubwa na ligi kuu ukizingatia aliwahi kuichezea Azam siku za nyuma," alisisitiza.

Kivutio kikubwa kwenye mchezo huo kitakuwa mshambuliaji wa Moro Utd, Gaudence Mwaikimba akisumbuana na mabeki wa Simba, Juma Nyosso. Simba inaongoza ligi ikiwa na pointi 27 baada ya kushuka dimbani mara 12 ikishinda michezo minane, kutoka sare mitatu na kufungwa mmoja dhidi ya mahasimu Yanga. Imefunga magoli 18 na kufungwa matano.

Wakati, Moro United inashika nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi kwa pointi zake 13 ikiwa imecheza mechi 12 ikishinda mitatu, kutoka sare minne na kupoteza mitano. Imefunga mabao 15 na kufungwa 20.

No comments:

Post a Comment