Thursday, January 26, 2012

Simba yapaa baada ya kuwasambaratisha wagosi wa kaya,Azam yaiadhibu Lyon

















Mpachikaji wa bao la kwanza la Simba Haruna Moshi"Boban"

Wekundu wa Msimbazi, Simba jana walianza vizuri hekaheka za duru la pili la ligi hiyo baada ya kuichapa mabao 2-1 Coastal Union na kujiimarisha kileleni mwa msimamo, huku Azam ikiwa bado na 'harufu' ya ubingwa wa Kombe la Mapinduzi ikitumia vizuri uwanja wao wa Chamazi na kuzoa pointi zote tatu kutoka kwa African Lyon kwa ushindi kama wa Simba.

Ushindi wa Simba kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, umeiwezesha kufikisha pointi 31 ikiwa na pointi tatu mbele ya mahasimu wao Yanga waliolazimishwa sare ya 2-2 na Moro United katika siku ya kwanza ya ufunguzi wa duru la pili.

Katika mechi hiyo ilioyopooza na kukosa ladha na changamoto ya ushindani hasa kipindi cha kwanza, ilishuhudia timu zote zikikosa nafasi chache za kufunga.Simba ilikosa nafasi mbili muhimu kupitia kwa Patrick Mafisango dakika ya 23 na Boban dakika ya 33.

Pamoja na ushindi huo, Kocha wa Simba, Milovan Cirkovic alikiri timu kushindwa kujiamini na hivyo kucheza chini ya kiwango, huku akimsifu kiungo Boban kwa kuonyesha kiwango kizuri.

"Nimefurahishwa na pointi tatu tulizopata ingawa timu haikucheza kwa kujiamini kama nilivyotarajia," alisema Cirkovic mara baada ya mchezo.

Coastal Union ilicheza vizuri zaidi kipindi cha pili na kufanya shambulizi moja kubwa dakika ya 29 kupitia Benard Mwalala aliyeshindwa kuusukumiza wavuni mpira akiwa kwenye nafasi nzuri.Kutokuwapo kwa mshambuliaji wa Simba wa kimataifa kutoka Uganda, Emmanuel Okwi na majeruhi Felix Sunzu kulileta udhaifu kwenye safu ya ushambualiaji ya Wekundu hao wa Msimbazi.

Sehemu ya kiungo ndiyo iliyoonekana kucheza kwa kuelewana, huku Mkude na Kapombe wakiilisha vizuri mipira iliyoshindwa kumaliziwa vizuri na washambuliaji wa Simba.

Dakika tano kabla ya mapumziko Simba walifungua kiu ya mabao baada kiungo mshambuliaji, Haruna Moshi 'Boban' kukwamisha mpira wavuni kwa shuti akimalizia krosi ya Shomari Kapombe na matokeo kuwa 1-0.

Kipindi cha pili Simba ilianza mchezo kwa kasi na nusura wafanye matokeo kuwa 2-0 kama siyo shuti kali la mshambuliaji Gervais Kago kupanguliwa na kipa wa Union katika dakika ya 49.

Coastal nao walijibu shambulizi hilo dakika ya 53 na nusura mshambuliaji Mohamed Ibrahim amtungue kipa Juma Kaseja kama asingekuwa makini langoni.

Ushirikiano mzuri kati ya Kago na Boban uliishia kwa Wekundu hao wa Msimbazi kufunga bao la ushindi dakika ya 77 likiwekwa wavuni na Kago.

Coastal walijitutumua dakika za lala salama na moja ya shambulizi lao lilizaa penalti dakika ya 88 baada ya beki Juma Nyosso kumuangusha Salum Gila na Hamis Shengo kufunga kiki hiyo ya penalti.

Kocha wa Coastal, Juma Mgunda aliwalaumu wachezaji wake kwa kushindwa kutumia vizuri nafasi za kufunga walizopata hasa kipindi cha pili.

Simba ilifanya mabadiliko kwa kipindi cha pili, ambapo alitoka Patrick Mafisango na kuingia Ramadhan Singano, Kago/ Edward Christopher na Mwinyi Kazimoto/Salum Machaku.

Katika mechi nyingine iliyochezwa kwenye Uwanja wa Chamazi nje kidogo ya jiji, wenyeji Azam walio kwenye kiwango kizuri waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya African Lyon.

Azam walikuwa wa kwanza kupata bao baada ya beki wa Lyon, Hassan Mwamba kujifunga mwenyewe katika harakati za kuokoa shuti la Aggrey Morris dakika ya 16.

Lyon ilijibu shambulizi hilo muda mfupi baadaye na kujipatia bao la kusawazisha likifungwa kwa shuti kali la Semmy Kessy na kumshinda kipa Mwadin Ally.
Bao la ushindi lililoifikishia Azam pointi 26 kwenye msimamo lilifungwa na John Bocco dakika ya 36.

Kocha wa Lyon, Jumanne Chale alisema ameridhishwa na kiwango walichoonyesha wachezaji wake, ingawa amesikitishwa na bao la kujifunga wenyewe na kusema limewanyima matokeo mazuri

No comments:

Post a Comment