Wednesday, February 1, 2012

Botswana na Mali kufa na kupona leo kombe la mataifa ya Afrika


KOCHA wa Botswana, Stanley Tshosane amesisitiza timu yake haitaibeba Mali watakapokutana leo kwenye mchezo wa mwisho wa Kundi D. Baada ya kuitoa jasho Ghana kabla ya kufungwa bao mmoja, Pundamilia hao kutoka Gaborone walisambaratishwa 6-1 na Guinea katika mchezo wao wa pili.

Botswana walioweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kufuzu kucheza fainali za mataifa ya Afrika mwaka huu, watasubiri miujiza pekee kuweza kufuzu kuingia robo fainali. Kilichokuwa cha muhimu kwenye mchezo wa leo dhidi ya Mali huu ndio utakaoamua timu mbili za mwisho zitakazofuzu kushiriki nane bora.

Hakutakuwa na kuwabeba. Tulifanya kazi kufika hapa, hivyo Mali nao wanapaswa wafanye kazi kubaki kwenye mashindano, alisisitiza Tshosane, ambaye mkataba wake unamalizika mwezi huu.

Tutacheza kama tulivyopanga. Tutaingia kwenye mchezo huo kwa umakini mkubwa kwa sababu tunataka kuondoka Gabon na ushindi.

Nao mabingwa mara nne wa michuano hiyo Ghana wanaopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, leo wanashuka dimbani kukamilisha mechi za makundi kwa kuumana na Guinea mjini, Franceville.Ghana ambayo inahitaji sare tu kujihakikishia nafasi ya kucheza hatua ya robo fainali, inaongoza Kundi D kwa kuwa na pointi sita kabla ya mechi ya leo.

Iwapo itashinda mechi ya leo itafikisha pointi tisa na hivyo kumaliza kundi lao bila kupoteza mchezo, lakini hata sare tu inaweza kuifanya kubaki kileleni mwa kundi .

Hata hivyo mechi hiyo inatarajiwa kuwa ngumu, kwani Guinea watashuka uwanjani kusaka pointi za kuwawezesha kucheza hatua ya robo.Guinea wanahitaji kushinda au sare iwapo Mali itafungwa na Botswana au timu hizo zikigawana pointi.

Hatua ya robo fainali ya michuano hiyo inatarajiwa kufanyika Jumamosi na Jumapili wiki hii, huku Zambia ikiwavaa Sudan na wenyeji Equatorial Guinea wakiwa na kibarua kizito mbele Ivory Coast.


No comments:

Post a Comment