Wednesday, February 1, 2012

Simba kuichezesha kwata Oljoro leo?



NYASI za Uwanja wa Taifa ulio kusini mwa jiji la Dar es Salaam leo zitakuwa katika msuguano mkali wakati vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba SC watakapokabiliana uso kwa uso na maafande wa JKT Oljoro.

Mbali ya vita hiyo kati ya Simba na JKT Oljoro inayofananishwa na ile 'takatifu' pia zitashuhudiwa harakati nyingine za ligi hiyo zikiendelea kwenye dimba la Uwanja wa Azam Complex ambapo African Lyon itakuwa ikipepetana na Polisi Dodoma.

Hata hivyo shughuli pevu inaonekana kusalia kwenye Uwanja wa Taifa, ambapo Simba yenye pointi 31 itakuwa inaukabili mtihani wa kusaka pointi tatu kutoka kwa Oljoro ambayo ipo Ligi Kuu kwa mara ya kwanza na ilianza msimu wa kwanza vizuri.

Simba inahitaji zaidi ushindi iwakimbie watani wao wa jadi Yanga waliofungana kwa pointi kileleni huku wakitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga timu ya Simba ipo kambini katika hoteli ya Lamada tangu juzi na maamuzi hayo yalitokana na maombi ya wachezaji na benchi la ufundi kwa uongozi wa Simba.

Kimsingi mtanange huu unaonekana kuwa mzito kwa Simba hasa kwa kuzingatia wapinzani wao JKT Oljoro walio nafasi ya nne na pointi zao 26 nyuma ya Azam FC inayokamata nafasi ya tatu na pointi zake 29, pia watakuwa wakihaha kusaka pointi tatu kwa lengo la kupunguza pengo kati yake na walio juu.

Ukiondoa nia, sababu na uwezo wa kila timu wakati huu, kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-0 ilioupata Simba ikiwa ugenini katika pambano la mzunguko wa kwanza inaweza kuwa faida nyingine kwa kikosi hicho cha kocha Milovan Cirkovic kuondoka na pointi tatu.

Pia, kurejea kwa mshambuliaji wao Emmanuel Okwi ambaye ilielezwa alikuwa 'amejificha' nyumbani kwao Uganda kunaweza kuongeza morali katika kikosi cha Simba ambacho katika mechi kadhaa zilizopita kilionekana kumtegemea zaidi Felix Sunzu ambaye sasa ni majeruhi ambapo hali hiyo ilisababisha Cirkovic awatumie zaidi viungo wake Haruna Moshi'Boban' na Uhuru Selemani katika kupachika mabao.

Nayo African Lyon ikiwa katika nafasi ya 10 na pointi zake 14 na ambayo hivi karibuni imekumbwa na wasiwasi baada ya Mkurugenzi wake, Rahim Zamunda kutishia kuiondoa kwenye ligi, kocha wake Jumanne Chale ameweka wazi kuwa kikosi chake kitaendelea kupigana hadi tone la mwisho ili kuhakikisha kinaondoka katika hatari ya kushuka daraja na leo kinatarajia kuibuka na ushindi kitakapokwa kikipambana na JKT Ruvu.

"Pamoja na hali ya wasiwasi iliyowakumba wachezaji wangu bado tutaendelea kupambana hadi tone la mwisho, nimewaambia vijana wangu waelekeze akili zao uwanjani kwani ndio kazi yao hivyo sina shaka katika kutekeleza wajibu wao kesho(leo),"alisema Chale.

Kwenye kambi ya kikosi cha Polisi Dodoma kinachokamata nafasi ya 13 mbele ya Villa Squad inayokamata mkia kwa pointi 10 kocha wa timu hiyo, Rashid Chama amesema ushindi walioupata katika mechi yao ya mwisho dhidi ya JKT Ruvu umewaongezea nguvu na sasa watahakikisha wanaitwanga Lyon.

"Sitaki masikhara tena kwa sababu nafasi tuliyopo sio nzuri, tumelitumia dirisha dogo kwa umakini, tuna watu kama Aman George atashirikiana na wengine kuipa timu pointi tatu na hili litathibitika kesho(leo) tutakapowanyuka African Lyon," alisema Chama

No comments:

Post a Comment