Wednesday, February 8, 2012

NUSU FAINALI KOMBELA MATAIFA YA AFRIKA NYASI KUCHIMBIKA LEO


GHANA "BLACK STARS"


Wachezaji wa Ghana wakishangilia katika moja ya mechi zao

IVORY Coast na Ghana zinapewa nafasi kubwa ya kukutana katika hatua ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika wakati zitakapopambana na Mali na Zambia leo katika mechi za hatua za nusu fainali za mashindano hayo zinazosubiriwa kwa hamu.
Ivory Coast mpaka sasa imeshinda mechi zote nne ilizocheza katika fainali hizo za Afrika bila ya kuruhusu hata bao moja, ambapo hivi sasa inataka kufika fainali na kutwaa ubingwa ambao haijaupata kwa miaka 20, huku Ghana ikitafuta ubingwa huo kwa mara ya tano baada ya miaka miwili iliyopita kushindwa kutwaa ubingwa huo baada ya kufungwa na Misri katika mechi ya fainali.

Kikosi cha Zambia

Lakini Ghana kama inataka kuingia fainali na kutwaa ubingwa huo inabidi iifunge kwanza Zambia katika mechi ya leo ya nusu fainali katika mechi inayotarajiwa kuwa kali kwa sababu Zambia pia imeonyesha soka la kuvutia ikitaka kucheza fainali mjini Libreville kwa ajili ya kumbukumbu ya wachezaji wenzao 25 na viongozi baada ya miaka 19.
Kwa upande wa Ivory Coast wapinzani wake ni Mali, ambao pia nao wanataka kucheza fainali baada ya kufanya kazi kubwa ya kuwatoa wenyeji Gabon katika hatua ya robo fainali.

Ingawa mpaka sasa Ivory Coast imefunga mabao nane bila kufungwa, lakini imeshindwa kuonyesha soka la kiwango cha juu kama ilivyotarajiwa kwa sababu ni timu inayoundwa na wachezaji bora wanaofanya vizuri katika ligi kubwa za Ulaya.
Ivory Coast ikiongozwa na nahodha wake Didier Drogba, Yaya Toure na Gervinho inapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika mechi ya leo, ingawa inatarajiwa itapata pia upinzani mkubwa kutoka kwa Mali.
"Jambo la msingi ni kutinga fainali kwa sababu tumeshindwa kufanya hivyo mara tatu katika fainali hizi za Afrika," alisema Yaya Toure akimaanisha kwamba walishindwa kufanya vizuri katika fainali za Afrika za mwaka 2006, 2008 na 2010.
Alisema: "Tuna wachezaji wazuri na washambuliaji, lakini tunatakiwa tupambane ili tuweze kushinda fainali hizi."

Kikosi cha Ivory Coast


Didier Drogba anatazamiwa kuongoza mashambulizi ya Ivory Coast dhidi ya Mali leo.

Naye kocha wa Mali, Alain Giresse alisema: "Wachezaji wote katika kikosi changu wana kiwango cha juu, tunawapenda na kuwaheshimu. Wote hawa wameshacheza fainali za Afrika zilizopita hivyo wana uzoefu."
Kwa upande wa mechi ya Ghana dhidi ya Zambia, kiungo wa Ghana, Anthony Annan ambaye mama yake alifariki alhamisi iliyopita aliamua kubaki kambini pamoja na wenzake ili kukisaidia kikosi cha Ghana kiweze kuibuka na ushindi kwa sababu mara ya mwisho Ghana ilitwaa ubingwa wa Afrika mwala 1982.

Kikosi cha Mali


Frederic Kanoute ataiongoza Mali dhidi ya Ivory Coast

Ghana waliingia hatua hiyo ya nusu fainali baada ya kuichapa Tunisia, huku Zambia wakiingia hatua ya nusu fainali baada ya kuichapa Sudan.
Zambia wana sababu ya kushinda mechi hiyo na kwenda Libreville itakapochezwa mechi ya fainali Jumapili ijayo, ambako kuna kumbukumbu ya wechezaji wenzao 18 na viongozi saba kufariki kwa ajali ya ndege mwaka 1993
"Hatuna wasiwasi wa kuifunga Ghana, tunataka kuifunga Ghana ili tucheze fainali, nina furaha timu yangu kucheza nusu fainali ya Fainali za Mataifa ya Afrika, tuna furaha na hatua tuliyofikia, naamini tutacheza kwa asilimia 100 kuhakikisha tunashinda, hatutaki kukata tamaa wala kujutia baadaye," alisema kocha wa Zambia, Herve Renard.


No comments:

Post a Comment