Wednesday, February 8, 2012

Yanga kulipa kisasi kwa Mtibwa leo?



MABINGWA wa soka nchini, Yanga leo wanaweza kuwakaba vizuri kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara, mahasimu wao wakubwa Simba lakini hilo likiwezekana tu, iwapo watazoa pointi zote tatu mbele ya Mtibwa Sugar katika mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Vinara Simba, mwishoni mwa wiki iliyopita walishindwa kuvuna pointi zaidi kufuatia kushitushwa na kipigo wasichokitarajia cha bao 1-0 toka timu iliyokuwa ikiburuza mkia, Villa Squad ya Dar es Salaam.
Kama Yanga watatumia vizuri fursa ya kutereza huko kwa mahasimu wao na kushinda mechi dhidi ya Mtibwa, itapanda mpaka nafasi ya pili na kufikisha pointi 34, ambazo ndizo zinazoipa jeuri ya kukaa kileleni Simba.
Kinyume na matokeo hayo, Yanga itajikuta ikiiruhusu Simba kujikandamiza zaidi kileleni, huku pia ikitoa mwanya kwa Azam FC kukoleza mbio za kupanda kileleni.
Yanga itashuka dimbani kusaka ushindi utakaosindikizwa na sababu kuu mbili, kwanza kulipa kisasi cha kufungwa bao 1-0 katika mchezo wao wa kwanza, na pili kuhakikisha inapata pointi tatu za kupunguza kasi ya Simba.
Matokeo mazuri kwa Yanga yanahitajika ili kuwajenga vizuri kisaikolojia wachezaji wake kabla ya mechi ngumu ya Ligi ya Mabingwa Soka Afrika dhidi ya Zamalek ya Misri Februali 18 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kocha wa Yanga, Kostadin Papic huenda akamuanzisha kipa namba moja wa timu hiyo, Yaw Berko ambaye taarifa za furaha zinadai kuwa ameshapona baada ya kuwa majeruhi tangu kumalizika michuano ya Kombe la Mapinduzi.
"Wachezaji wote akiwemo Yaw Berko wako katika hali nzuri, isipokuwa Nurdin Bakar ambaye anatarajia kuondolewa bandeji ngumu (POP) baada ya wiki mbili zijazo," alisema Louis Sendeu, Afisa habari wa Yanga.
Kazi ngumu itakuwa kwa Mtibwa itakayokuwa ikicheza mechi ya kwanza ugenini baada ya kufungwa mechi mbili mfululizo kwenye uwanja wao wa nyumbani dhidi ya JKT Oljoro ya Arusha na Coastal Union ya Tanga.
Ikiwa na pointi 22 katika nafasi ya tano kwenye msimamo, Mtibwa itakuwa na kila sababu ya kushinda mechi ya leo ili 'kuganga' majeraha hayo ya vipigo na pia kurejesha imani kwa mashabiki wake.
Vichapo hivyo vilipelekea kutimuliwa kwa kocha msaidizi wa muda mrefu wa timu hiyo, Mecky Mexime aliyedaiwa kuwa kiini cha kufanya vibaya katika mechi hizo mbili za vipigo.
Msemaji wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru alitamba timu yake kuiduwaza Yanga na kuondoka na pointi zote tatu katika mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka.
"Kikosi kiko shwari, wachezaji wana ari na moyo wa ushindani dhidi ya Yanga. Tumejipanga kushinda mechi hii pamoja na kufahamu kwamba tunacheza na timu ngumu," alisema Kifaru.

No comments:

Post a Comment