Wednesday, February 15, 2012

RAGE 'AWARUHUSU' MASHABIKI WA SIMBA KUISHANGILIA ZAMALEK
















Mwenyekiti wa Simba Ismail Aden Rage

WAKATI Zamalek wakichekelea kurejea juu kiwango cha mshambuliaji Amr Zaki, tayari kuivaa Yanga, Mwenyekiti wa Simba, Aden Rage amesema klabu yake hawezi kuwazuia mashabiki kushangilia timu wanayoipenda, kwani kinyume chake ni kuingilia uhuru mtu.
Simba na Yanga mwishoni mwa wiki hii zitakuwa kwenye michezo ya kimataifa, wakati mabingwa wa Tanzania watakuwa wenyeji wa Zamalek kwenye Uwanja wa Taifa katika Ligi ya Mabingwa, watani zao Simba inayocheza Kombe la Shirikisho itakuwa Rwanda kuivaa Kiyovu.
Akijibu malalamiko ya Yanga kuhusu baadhi ya mashabiki wa Simba kununua jezi za Zamalek kwa nia ya kuishangilia timu hiyo, Rage alisema si kitendo cha uungwana, lakini hawezi kuwazuia kufanya hivyo.
Viongozi wa Simba na Yanga mwaka jana walikubaliana kuzungumza na mashabiki wao ili timu hizo zinapocheza mechi za kimataifa wawe kitu kimoja jambo lililoshindakana.

"Unajua ni vigumu kuingilia uhuru wa mtu. Ni kweli nimeshuhudia mashabiki wa timu yangu wakianza kuvaa jezi za Zamalek, lakini na Yanga nao wakumbuke wakati sisi tukicheza na TP Mazembe hali ilikua kama hii.
"Sasa napenda kutoa tu wito kwamba pamoja na hili kushindikana, lakini kila mmoja atambue juhudi za wachezaji ndio pekee zitakazowainua kusonga mbele," alisema Rage.

Aidha kwa upande wa Yanga kupitia msemaji wao, Luis Sendeu alisema hawana shaka na hilo kwani wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanashinda na kuwataka mashabiki wao kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu yao ili iweze kufanya vizuri.
"Ni kweli wapinzani wetu wameanza kununua jezi zenye jina la Zamalek mahususi kuvaa katika pambano letu Jumamosi, lakini sisi tunasema hatutakata tamaa kwa hilo ingawa uongozi unalaani kitendo hicho," alisema Sendeu.
Wakati hali ikiwa hivyo hapa nyumbani mambo ni tofauti kwa Zamalek baada ya kocha msaidizi wa timu hiyo Ismail Youssef kusifu kiwango kilichoonyesha na wachezaji wake waliposhinda 4-1 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Itisalat.
"Tumefaidika sana na mchezo huu wa kirafiki kabla ya mechi yetu dhidi ya Yanga," alisema Youssef.
Mshambuliaji Zaki alifunga mabao mawili tangu aliporejea dimbani baada ya kumaliza matatizo yake ya kudai mishahara iliyomweka nje ya uwanja kuanzia mwezi Desemba.

Kumuona mshambuliaji huyo mwenye miaka 29 akiwa kwenye kiwango cha juu kimetoa faraja kwa Youssef kuwa sasa lengo la klabu hiyo kurudisha heshima yake Afrika litafanikiwa.
"Zaki amerudi kwa kiwango kizuri utakuwa msaada mkubwa kwetu dhidi ya Yanga," alisema kocha huyo.
Zamalek wanatarajiwa kutua nchini Ijumaa alfajiri na baadaye jioni kufanya mazoezi katika Uwanja wa Taifa kabla ya pambano lao siku inayofuata.

No comments:

Post a Comment