Tuesday, May 22, 2012

BOBAN AANGUUKA NA KUZIMIA UWANJA WA NDEGE


Mgosi na Boban wakiwa katika msiba mjini Kinshasa

MICHAEL MOMBURI, KINSHASA
KIUNGO wa Simba, Haruna Moshi Boban, ameanguka katika Uwanja wa Ndege wa N`Djili mjini Kinshasa kutokana na mapigo ya moyo kushuka ghafla.

Tukio hilo lilitokea jana Jumatatu wakati Boban akiwa anajiandaa kurudi Dar es Salaam baada ya kuhudhuria mazishi ya Patrick Mafisango aliyefariki Alhamisi iliyopita kwa ajali ya gari iliyotokea jijini Dar es Salaam.

Hali ya Boban ilibadilika ghafla akiwa uwanjani hapo na akashindwa kuona mbele kabla ya kulegea na kuanguka.

Madaktari wa uwanja huo walitumia zaidi ya saa 1:30 kumtibu Boban kabla hajarejea katika hali ya kawaida huku bado akiwa na simanzi kubwa kutokana na kifo cha Mafisango.

"Nilimkumbuka sana Mafisango, wakati nikitafakari, nikaona ninalegea, nikashindwa kuona kitu chochote mbele na nikaanguka," Boban aliliambia Mwanaspoti katika uwanja huo wa ndege wa Kinshasa.

Daktari aliyemuhudumia Boban aliliambia Mwanaspoti kuwa: "Alikuwa na hali mbaya sana, mapigo ya moyo yalikuwa chini, yangeweza kuondoa maisha yake."

Licha ya kupata matibabu hayo, Boban pia alipewa kahawa kwa lengo la kuinua mapigo yake ya moyo.

Boban ambaye alikuwa rafiki mkubwa wa Mafisango ikiwa ni pamoja na kulala chumba kimoja wanapokuwa kambini Simba, aliwakilisha wachezaji wengine wa klabu hiyo katika msiba huo mjini Kinshasa.

Mwili wa Mafisango aliyekuwa akicheza nafasi ya kiungo enzi za uhai wake, ulizikwa katika makaburi ya Kinkole nje kidogo ya Kinshasa juzi Jumapili kuhitimisha safari yake ya miaka 32 ya uhai wake duniani.

No comments:

Post a Comment