Friday, May 11, 2012

MASIKINI SAJUKI!! ZIMESALIA SIKU 2 KUELEKEA INDIA HALI YAZIDI KUWA MBAYA, WOLPER ATOA MIL 15


Sajuki akiwa kitandani na wasanii wenzake waliokwenda kumjulia hali

Masikini SAJUKI! Siku mbili kabla ya kwenda katika Hospitali ya Apollo nchini India kwa matibabu, afya ya stadi wa filamu za Kibongo, Sadick Juma Kilowoko ‘Sajuki’ ni ya kusikitisha ile mbaya.
Kadiri siku zinavyoyeyuka, hali ya Sajuki inazidi kuwatoa watu machozi baada ya kuzidiwa na kushindwa kunyanyuka kitandani. Laiti kama utamuona na ukashindwa kububujikwa na machozi basi utakuwa huna utu.



Wasanii wa Bongo movie wakiwa wamemzunguka Sajuki kitandani(Chini ya picha Wolper aliyetoa mil 15)

Tukio la kusikitisha lililowatoa machozi wasanii wenzake ni lile la Jumanne wiki hii nyumbani kwake Tabata Barakuda, Dar es Salaam ambapo msanii na prodyuza huyo wa filamu alishindwa kuamka kitandani kupokea dola elfu kumi (takribani Sh. milioni 15) alizozitoa mwigizaji mwenzake, Jacqueline Wolper kwa ajili ya matibabu huku akisindikizwa na mastaa wengine wa Bongo Movie.
Sajuki akiugulia maumivu huku akilalamika kujisikia vibaya, hivyo kuwaomba wasanii wenzake kwa heshima waingie chumbani kwake ili apokee fedha hizo.



Msanii wa Bongo movie akiwa ameshindwa kujizuia na kujikuta akimwaga chozi

Kitendo hicho ndicho kilichowafanya baadhi ya wasanii wenzake kushindwa kujizuia na kujikuta wakiangua vilio huku Sajuki akiwatuliza na kuwaomba wasilie wala wasihuzunike kwani kila kitu ni mapenzi ya Mungu.
“Msihuzunike ndugu zangu, naamini kila kitu ni mapenzi ya Mungu na si vinginevyo, jipeni moyo,” alisema Sajuki kwa tabu akiwa amelala kitandani akiwa amezungukwa na mastaa hao.

WOLPER Kwa upande wake Wolper aliyekuwa akimwaga machozi mithili ya bomba la mvua, alisema kuwa siyo kwamba ana fedha nyingi, ila ni namna alivyoguswa na mateso ya Sajuki.
“Siyo kwamba sina shida bali ni moyo wa kusaidia kuokoa uhai wa mwenzetu. Tulizoea kuwa naye location (sehemu ya kurekodia filamu) na kwenye tasnia yetu, anaumwa na hajiwezi, niliumia sana,” alisema Wolper aliyekuwa akifutwa machozi na wenzake.

WASTARA Naye mke wa Sajuki, Wastara Juma, huku akilia muda wote, alitoa shukurani zake za dhati kwa Wolper na kueleza jinsi alivyoguswa na kuona umuhimu wa kumsaidia mumewe
Habari kwa hisani ya Global Publishers.

No comments:

Post a Comment