Friday, May 11, 2012

NYOSSO KUTIMKIA SAUZ


Juma Nyosso wa pili kulia waliosimama akiwa na kikosi cha Simba

Beki mashuhuri Juma Nyosso wa Simba, amepata soko baada ya Klabu ya Platinum Stars ya Afrika Kusini kutangaza kuwa inataka kumnunua kwa ajili ya msimu ujao.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba zimeeleza kuwa uongozi wa timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL), umeonyesha nia ya kumsajili Nyosso na ulifanya mazungumzo na Simba.
“Kweli jamaa wa Platinum Stars walikuja na kufanya mazungumzo. Wameonyesha wanamhitaji Nyosso,” kilieleza chanzo cha uhakika na kuongeza “ Mazungumzo yalifikia katika hatua nzuri kabisa lakini kuna mambo kadhaa ya kuangalia ndipo hilo likamilishwe.”
Mjumbe mwingine wa kamati ya usajili ya Simba aliliambia gazeti hili kuwa suala hilo lazima liidhinishwe na kamati ya usajili.
“Kamati ya usajili itamaliza kila kitu lakini itafanya hivyo baada ya kukutana na kocha Milovan ambaye ataeleza anachokitaka, pia ni wachezaji gani anataka wabaki, waondoke au waongezwe.

“Baada ya hapo tutaanza kufanya utaratibu, sasa inategemea huenda na Nyosso akaruhusiwa kuondoka,” alisema mjumbe huyo.
Platinum Stars inayofundishwa na Owen Da Gama ipo katika nafasi ya 10 katika PSL na kikosi chake kina wachezaji wote raia wa Afrika Kusini isipokuwa watatu, kipa Etame Soppo (Cameroon), Henrico Boates (Namibia) na Mohammed Chikoto (Niger).

Timu hiyo iliwahi kuripotiwa kumtaka Nyosso mwishoni mwa mwaka jana lakini baadaye viongozi wake walisita kuendelea na mazungumzo na Simba.

No comments:

Post a Comment