Thursday, July 19, 2012

WATANZANIA WAENDELEA KUPOTEZA MAISHA KWA AJALI ZA MELI, HII TENA


WATU 60 wanahofiwa kufa maji na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya boti iliyokuwa imebeba abiria wanaokadiriwa kufikia 250 ikitokea Dar es Salaam kwenda Unguja, Zanzibar kuzama baharini.Hii ni ajali ya pili mbaya kutokea katika kipindi cha miezi 10 tangu ilipotokea nyingine ya Meli ya Mv Spice Islander ambayo inakadiriwa kuwa watu wapatao 200 walifariki dunia.Boti hiyo iliyoondoka jana Dar es Salaam majira ya saa 6:00 mchana na kutarajiwa kufika Bandari ya Malindi, Zanzibar saa 9:30 jioni, ilizama eneo la Pungume karibu kilomita 48 kutoka Bandari ya Zanzibar.
Inaelezwa kuwa, ilianza kuzama saa 7:30 mchana kutokana na kupigwa na mawimbi mazito ya bahari.

Hata hivyo, Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu wa Zanzibar, Hamad Masoud Hamad alithibitisha vifo vya watu 12 hadi vilivyoripotiwa ilipotimu saa 12:30 jioni jana wakati kazi ya uokoaji ikiwa inaendelea.

Baadaye saa 1:00 Ofisa Habari na Mawasiliano wa Wizara hiyo, Nafisa Madai aliwaambia waandishi wa habari kuwa idadi hiyo ilikuwa imeongezeka hadi kufikia 24 na majeruhi walikuwa 145.Madai alisema wakati boti hiyo inaondoka Dar es Salaam, ilikuwa na abiria 250 wakiwamo watoto 31 na wafanyakazi tisa.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Said Shaaban akizungumzia ajali ya boti hiyo ya Mv Skad, inayomilikiwa na Kampuni ya Meli Seagull alisema: “Vikosi vya uokoaji tayari vinaelekea katika eneo hilo ili kusaidia majeruhi na kufuatilia yaliyotokea.”

Maofisa kadhaa wa Serikali wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi walifika Bandari ya Malindi na Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu Zanzibar, Hamad Masoud Hamad aliongoza msafara wa viongozi wengine kwenda katika eneo la tukio.

Awali, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alisema kuwa, hadi alipopata taarifa, watu waliokuwa wamefariki dunia ni saba na 124 ndiyo waliokuwa wameokolewa. Alisema meli hiyo ina uwezo wa kubeba abiria 300 na waliosafiri siku ya tukio hawazidi 250.

Awali, taarifa zilieleza kuwa watu 10 waliokolewa na maiti zaidi ya 60 zimenasa katika boti hiyo na kuvifanya vikosi vya uokoaji vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi na KMKM kupata wakati mgumu kwenye zoezi la uokoaji.Kazi ya kuokoa maisha ya watu waliozama kwenye boti hiyo na kuopoa maiti ilifanywa kwa kutumia boti nne zikiwamo za Serikali na zile zinazomilikiwa na Kampuni ya Azam Marine.

Hata hivyo, ilielezwa kwamba boti za polisi zilichelewa kwenda katika eneo la tukio kutokana na kukosekana kwa mafuta.

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kufika bandarini, Balozi Seif aliwataka wananchi kutulia na kusubiri wakiwa nyumbani wakati Serikali ikifanya juhudi za uokoaji.

Shughuli nyingi za usafiri zilivurugika kutokana na tukio hilo na Meli ya Mv Sea Bus ililazimika kufuta safari zake kupisha kazi hiyo ya uokoaji.
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), imesema inafuatilia tukio hilo kwa karibu ili kubaini chanzo.
Ofisa Uhusiano wa Sumatra, David Mziray alisema jana muda mfupi baada ya ajali hiyo kuwa, wanawasiliana na Kituo cha Utafutaji na Uokoaji Majini (MRCC), ili kupata taarifa kamili kabla ya kuujulisha umma.


Baadhi ya abiria wakisubiri uokozi


Waokoaji wakiwa katika boti ya Kilimanjaro wakiopoa maiti ya mzungu


Muokoaji akiwa na maiti



Meli ya MV Skagit ikiwa imezama katika bahari ya Chumbe


Abiria akichomolewa baharini na kikosi cha uokoaji




Jopo la madaktari likitoa huduma ya kwanza kwa majeruhi wa ajali ya meli katika bahari ya Chumbi


Umati wa wananchi wakiwa katika bandari ya Malindi wakifuatilia tukio la ajali ya meli ya Mv Seagull(Skagit)







"Najuuuuta kuifahamu Tanzania".....Inaelekea ndivyo mzungu huyu anavyofikiria


Boti ya KMKM ikiwa katika uokozi


Maiti ikitolewa baharini


Majeruhi akiwa amebebwa tayari kwa kupatiwa huduma ya kwanza



No comments:

Post a Comment