Tuesday, August 14, 2012

HANS POPE AIFUNGUKIA YANGA, MZAZI WA TWITE AHOFIA USALAMA WA MWANAE

Sakata la usajili wa Mbuyu Twite aliyejiunga Yanga, huku Simba nayo ikiingia naye mkataba, umeendelea kuwa 'kivutio', ambapo sasa Wekundu hao wa Msimbazi wameibuka na madai mapya.
Mwenyekiti wa Kamati ya usajili klabu ya Simba, Zacharia Hans Pope ameilaumu Yanga kwa kuuingiza mchezo wa soka kwenye machafuko.

Pope amesema kitendo cha wenzao kuwazunguka na kumshawishi Twite kurejesha fedha walizompa ili asajili Simba, kinaweza kuleta uhasama usio na ulazima."Tumepata taarifa kuwa baba mzazi wa Mbuyu (Twite) amemkataza mwanaye kuja kuichezea Yanga kwa hofu maisha yake."
"Mzee Twite anataka Simba na Yanga zikutane kufanya mazungumzo kwa lengo la kuweka mambo sawa kisha ndipo amruhusu kuja Tanzania," alisema Pope.
"Unadhani kwa kitendo walichofanya Yanga, mashabiki wa Simba watafurahi? Baba yake mzazi (Twite) amechukizwa na hali hiyo, anahofia usalama wa kijana wake," alisema Pope.
"Vita ya soka haina tofauti na ile ya siasa au dini. Kwa hiyo baba mzazi wa Mbuyu ameomba Yanga na Simba kumaliza suala hili mwanaye aweze kucheza soka kama ilivyo kazi yake."

Katika kusisitiza ukweli wa madai yao, Pope alisema tayari uongozi wa Yanga umeomba kukutana nao ili kuzunguza na kumaliza suala hilo.
"Ukweli ni kamba, hatuna tatizo na Yanga. Nafikiri siyo mara yao ya kwanza wala mwisho kutufanyia mchezo huu mchafu. Ni kawaida yao."

"Wameomba [Yanga] tukutane ili kumaliza utata wa suala hili, vinginevyo Twite hatakuja siyo kujiunga na Yanga au Simba, bali haji kabisa."
Aliongeza: "Tulianza mazungumzo na Bahanuzi (Said)wakatuzunguka na kumsainisha, ikawa hivyo tena kwa Kavumbagu (Didier) na sasa wametuma viongozi Kenya kutaka kumsainisha Pascal Ochien ambaye yupo na timu Arusha."

"Nafikiri Yanga kama wanataka kulipa kisasi cha mabao matano tuliyowafunga, wacheze mpira na siyo kutuzunguka na kusajili wachezaji wetu."
"Hata sisi tunaweza mchezo huo mchafu---ni kweli tunaweza kuwafanyia, lakini hatuoni sababu ya kufanya hivyo," alisema zaidi Pope.

Alipoulizwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Yanga, aliyefanikisha usajili wa Twite, Abdallah Bin Kleb, alikana kuwapo na makubaliano ya kukutana na Simba kuzungumza suala la mchezaji huyo.
Bin Kleb aliibeza kauli ya Pope na kusema inalenga kuwaziba mdomo mashabiki wa Simba ili wasahau kuzungumza suala la usajili wa Twite.

"Hakuna makubaliano ya sisi [Yanga] kukutana na Simba ili kuzungumza suala la Twite. Kwanza kwa nini tufanye hivyo wakati mchezaji tumemsajili kwa kufuata taratibu," alihoji Bin Kleb.
"Kama Simba wana matatizo na mchezaji ni wao, sisi hatuna matatizo na Twite wala mzazi wake, sasa iweje leo ashindwe kuja kujiunga na timu aliyopenda kuichezea?," alisema.

Alisema, Twite anatarajia kuja nchini wiki ijayo akitoka Kongo alikokwenda kuwasalimia wazazi wake ambao hakuonana nao muda mrefu.
Wakati huohuo, mshambuliaji mpya wa Simba George Ochan kutoka Kenya tayari ameshajiunga na wenzake, Arusha, huku Sihaune Abdulaziz kutoka Ghana akitarajia kutua leo.

No comments:

Post a Comment