Tuesday, August 14, 2012

MALIASILI KIMENUKA,MKURUGENZI WANYAMAPORI ATIMULIWA


Waziri wa Maliasili na Utalii Khamis Kagasheki

Mkurugenzi wa Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Obeid Mbangwa na wenzake wawili, wametimuliwa kazi kwa kashfa ya kutorosha wanyama hai 136 wa aina 14 tofauti kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia), usiku wa Novemba 26, 2010.


Mkurugenzi wa Wanyamapori alietimuliwa kazi Obeid Mbangwa

Hatua hiyo imefikiwa baada ya tume mbili zilizoundwa kuchunguza suala hilo bila kuhusisha wizara yenyewe, kumaliza kazi yake na kukabidhi ripoti kwa Waziri.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki alisema jana mjini Dodoma kuwa mbali na watuhumiwa hao, mtumishi mwingine wa wizara hiyo amevuliwa madaraka, wawili wamepewa onyo kali la maandishi na wawili uchunguzi dhidi yao unaendelea.

Mbangwa wakati wa kashfa hiyo ya kusafirisha wanyama hai wanaokadiriwa kuwa na thamani ya Sh170 milioni kwa ndege ya kijeshi ya Qatar, alikuwa Mkurugenzi Msaidizi Matumizi ya Wanyamapori.
Wengine waliotimuliwa kazi ni Simon Gwera na Frank Mremi waliokuwa Maofisa Uwindaji wa Kitalii, Cites na Utalii wa Picha mkoani Arusha.

Mkurugenzi Msaidizi, Uendelezaji Wanyamapori, Boneventura Midala amevuliwa madaraka kutokana na kutochukua hatua kikamilifu za ulinzi ambazo zingeweza kuzuia kutokea kwa utoroshaji wa wanyama. Wakati wa tukio hilo alikuwa Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Kuzuia Ujangili.

Katika hatua hizo, maofisa wanyamapori daraja la pili, wawili waliotekeleza maelekezo ya wakuu wao wa kazi yaliyo kinyume cha sheria wamepewa onyo kali la maandishi.

Kagasheki aliwataja maofisa hao kuwa ni Ofisa Leseni ya Uwindaji wa Kitalii, Cites na Utalii wa Picha Arusha, Martha Msemo na Ofisa Leseni Ofisi ya Uwindaji wa Kitalii, Cites na Utalii wa Picha Dar es Salaam, Anthonia Anthony.

Rungu la wizara hiyo pia limemwangukia Mkuu wa Kituo cha Uwindaji wa Kitalii, Cites na Utalii wa Picha Arusha, Silvanus Ukudo aliyepewa onyo kali la maandishi kwa kushindwa kufuatilia kupata maelekezo ya Mkurugenzi wa Wanyamapori kuhusu mtumishi wake aliyekiuka sheria katika utoaji wa vibali.

Ukudo pia ameonywa kwa kushindwa kupeleka kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, taarifa kuhusu mtumishi huyo ili achukuliwe hatua za kinidhamu.
Kagasheki alisema uchunguzi unaendelea dhidi ya watumishi wengine wawili, Ofisa Matumizi Endelevu ya Wanyamapori, Mohamed Madehele na Ofisa wa Kituo cha Uwindaji wa Kitalii, Cites na Utalii wa Picha Arusha, Mariam Nyallu.

Alisema kwa upande wa wafanyabiashara waliohusika katika kashfa hiyo, kesi inaendelea mahakamani na kwa upande wa Qatar, Serikali alisema: “Tumefanya kila jitihada. Tumewasiliana kupitia Makao Makuu ya Cites, Geneva, Uswisi, lakini Qatar pamoja na kukubali kupokea maombi yetu kutoka Cites, imekaa kimya.”

Kuhusu hatua zaidi dhidi ya watuhumiwa hao, Waziri Kagasheki alisema: “Kwa kuwa imebainika walihusika na vibali vilivyosababisha hao wafanyabiashara wakamatwe, suala hilo halijaishia hapo.”
Waziri huyo alisema atajitahidi kadri ya uwezo wake kusimamia wizara hiyo ili kuhakikisha sheria na taratibu zinafuatwa... “Sheria zipo nzuri, udhaifu mkubwa ni kwa watendaji wetu,” alisema.
Alipotakiwa kuzungumzia suala hilo Mbangwa alisema hajui chochote.

Alisema hadi jana alikuwa hana taarifa za kufukuzwa kazi hivyo hawezi kusema chochote hasa bila ushahidi.

Unasema wamenifukuza kazi, ndiyo wametangaza hivyo? Mimi sina taarifa hizo na hivyo siwezi kuelezea chochote,” aling'aka Mbangwa.

No comments:

Post a Comment