Monday, January 28, 2013

SIMBA, YANGA, AZAM ZAANZA VYEMA DURU LA PILI

MABINGWA watetezi, Simba jana walianza kwa kishindo duru la pili Ligi Kuu Bara kwa kuitungua African Lyon mabao 3-1, katika mechi ambayo kila upande ulikosa kufunga penalti katika kila kipindi.
Ushindi kama huo pia uliandikwa na Azam FC iliyotumia vizuri Uwanja wa Chamazi kuiogesha kipigo Kagera Sugar ya Kagera, kadhalika Coastal Union kule Mkwakwani Tanga dhidi ya Mgambo Shooting.

Wachezaji wa Simba wakimnyanyua Ngassa baada ya kufunga goli.

Simba imefikisha pointi 26, lakini ikiendelea kubaki nyuma ya Azam kwa tofauti ya pointi moja, na Yanga inayocheza leo haijaathiriwa na matokeo ya mechi za jana.
Katika mchezo huo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wachezaji Mrisho Ngassa wa Simba na
Shamte Ally wa Lyon walikosa penalti. Penalti ya Ngassa ingeweza kumpa ‘hat trick’ kama siyo kipa wa Lyon, Abdu Seif kuicheza dakika ya 66 kufuatia Ibrahim Issac kumkwatua Ramadhan ‘Redondo’ Chombo.

Ngassa akiwachachafya mabeki wa African Lyon

Shamte naye alishindwa kulenga lango baada ya penalti yake kwenda nje kufuatia madhambi ya Paul Ngalema dhidi ya Fred Lewis dakika ya 30.
Redondo alifunga bao la mapema zaidi mzunguko wa pili, baada ya kutumia dakika mbili tangu kuanza mpira kutikisa kamba za Lyon akimalizia pasi ya Mrisho Ngassa.
Lyon walijibu shambulizi dakika ya nne na ustadi wa Juma Kaseja ulimnyima bao Jacob Massawe baada ya shuti lake kuchezwa na kipa huyo namba moja Msimbazi.
Mashuti mawili ya Ngassa dakika ya 4 na 6 yangeweza kubadilisha matokeo kama siyo kukosa shabaha na kwenda moja kwa moja mikononi mwa kipa wa Lyon, Abdul Seif.
Ngassa alirekebisha makosa yake kwa kufanya matokeo kuwa 2-0 baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa Lyon akimalizia pasi ya Jonas Mkude.
Alikuwa Ngassa tena akipachika bao la tatu, la pili kwake kwenye mchezo huo shuti akimalizia mpira wa krosi uliopigwa na Haruna Chanongo dakika ya 35. Kipindi cha pili, Kocha Patrick Liewig aliwapumzisha Paul Ngalema na Mussa Mudde na kuingia Kigi Makasi na Komalibil Keita.

Mlinda mlango wa Afrikan Lyon akiondosha hatari langoni mwake.

Lyon walipunguza makali ya tofauti ya mabao ya kufungwa baada ya Bright Ike kumtungua Kaseja dakika ya 60 likiwa bao pekee kwao kwenye mchezo huo.
Pamoja na ushindi huo, Kocha Liewig alisema mchezo ulikuwa mgumu, ingawa pia hakusita kueleza hisia akiwalaumu wachezaji wake kucheza ovyo kipindi cha pili.
Mkwakwani Tanga, Union walifikisha pointi 25 na kupanda mpaka nafasi ya nne kwenye msimamo kwa mabao ya Philipo Mutasela, Danny Lihanga na Haroun Mahundi, huku bao la Mgambo likifungwa na Peter Mwaliyanzi.




Wachezaji wa Yanga wakimpongeza Tegete baada ya kutupia goli dhidi ya Prisons ambapo Yanga ilishinda 3-1.


Mabeki wa Prisons wakiondosha hatari langoni mwao

 

No comments:

Post a Comment