Katibu mkuu wa CCM Wilson Mukama
Habari kwa hisani ya gazeti la Mwanachi,Amini Yasini, Rufiji na Ahmed Makongo, Kahama
HALI ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), si shwari na Katibu Mkuu wake, Wilson Mukama amekiri kwamba hivi sasa kina mpasuko mkubwa unaotokana na makundi yanayofanana na yale ya Umoja wa Kujihami wa Nchi za Magharibi (Nato) na Umoja wa Mataifa yenye nguvu kubwa kiuchumi duniani (G8).
Wakati mtendaji mkuu huyo wa chama tawala akitoa kauli hiyo, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige ameibuka na kumshambulia waziwazi, Katibu wa Taifa wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye akimtuhumu kukiharibu kwa utendaji mbovu, hivyo kutaka ang’olewe haraka akidai kuwa ni gamba.
Nchi zinazounda G8 ni Marekani, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Russia na Uingereza ambazo pia baadhi yao, ndizo zinazounda Nato, umoja wenye wanachama 28.
Mukama alitoa kauli hiyo juzi wilayani Rufiji wakati akizungumza na umati wa wananchi na wanachama wa chama hicho waliofurika katika Viwanja vya Corecu, Kata ya Kibiti.
Alisema baadhi ya wanachama wa CCM wamekuwa ni wasaka madaraka na wanapokosa huamua kuunda makundi ya uhasama ambayo hawataki kuyavunja pindi mchakato wa kutafuta mgombea unapomalizika.
“Makundi yaliyoundwa tangu 2005 na 2010 yanaendelea kukitafuna chama, wanachama wakinyimwa uongozi wanaanza uhasama, hatufiki malizeni makundi,” alisema.
Alisema makundi hayo pia yako katika Wilaya za Mkuranga na Rufiji, ambako katika ziara yake amebaini mpasuko mkubwa unaotokana na fitina na uhasama miongoni mwa wapenzi na makada wa CCM na kusisitiza kwamba hayafai na ni hatari kwa mustakabali wa chama hicho kikongwe barani Afrika.
“Nikiwa Mkuranga nilitaarifiwa kuwa kuna makundi ya Nato na G8 na sasa nimefika Rufiji nimeyakuta makundi hayo. Jamani makundi hayo ya nini?”
Mukama ambaye aliwahi kushika nafasi mbalimbali za kiutendaji zikiwemo za Ukuu wa Wilaya ya Mafia akimrithi mtangulizi wake Hemedi Mkali, alisema aliwahi kugombea ubunge wa viti vya Taifa kupitia Juwata (iliyokuwa Jumuiya ya Wafanyakazi Tanzania), na aliposhindwa alikubali matokeo.
Alisema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema bila CCM imara nchi yetu itayumba, akimaanisha kuwa hakuna chama mbadala cha kuongoza nchi zaidi yake.
Waziri mkuu wa kwanza na Raisi wa Kwanza wa TANZANIA hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Alitoa mfano wa Chama cha Democrat cha Marekani kwamba wanachama wake hawana kadi, bali mapenzi ya chama yako mioyoni mwao na wanapojiunga hawafanyi hivyo kwa lengo la kusaka madaraka... “Hii ni tofauti kubwa na nchi zetu ambako mtu akijiunga na chama kitu kwanza kufikiria ni kusaka madaraka,” alisema.
Alisema chama hicho kina mkakati madhubuti wa kupambana na watu wachache wanaotaka kukimiliki wakitumia nguvu ya fedha.
Alisema baadhi ya wanachama wa kawaida wamejiona kuwa hawana nafasi katika chama chao wakiamini kuwa kimetekwa na wenye fedha na kuongeza kwamba mwanachama wa kawaida hawezi kuongoza bila rushwa.
“Hapana! Chama chetu hakitakubali hali hiyo. Ni hatari sana kwa mustakabali wa chama chetu na nchi yetu,” alisema na kuongeza kuwa wanachama wa kawaida wanatakiwa kugombea hata kama hawana fedha.
Alisema chama kipo katika uchaguzi wake wa ndani na kuwataka wanachama kufanya uamuzi sahihi wa kuchagua viongozi waadilifu wasiotumia rushwa, kwani kufanya hivyo kunaweza kusababisha kuingia watu katika uongozi waliotoa rushwa.
Katika mikutano yake hiyo, Mukama alitamba kuwa chama chake hakitishwi na wapita njia akimaanisha wapinzani wanaodai kuwa hakijafanya kitu.
Alisema CCM ni chama makini na sikivu katika kusikiliza kero za wananchi akitamba kwamba kimejenga Daraja la Mkapa ambalo limekuwa kiunganishi kati ya Mikoa ya Lindi, Mtwara na Dar es Salaam na umeme wa gesi unaotoka kusini ambao wananchi wa Rufiji wananufaika nao kwa sasa.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rufiji, Mrisho Matimbwa alisema katika uchaguzi uliopita wa chama hicho kulikuwa na makundi mawili, ya Bush na Al Qaeda ambayo kwa sasa yamekufa na kubakia mpasuko katika halmashauri kuu ambako aliahidi kuutatua.
Maige na Nape
Katibu wa itikadi na uenezi wa CCM Nape Nnauye
Mbunge wa Msalala(CCM) Ezekiel Maige
Akizindua matawi mawili ya wakereketwa wajasiriamali wa CCM katika Kijiji cha Isaka, Kahama, Shinyanga, Maige ambaye ni Mbunge wa Msalala alimtaka Nape kuacha tabia yake ya kutoa kauli ambazo kwa namna moja au nyingine zinaelekea kukidhoofisha chama.
Alimtaka kupima utendaji wake tangu alipoishika nafasi hiyo ya Itikadi na Uenezi na kujiuliza ni wanachama wangapi wameingia ndani ya chama hicho.
Alisema sasa hivi kuna wimbi kubwa la wanachama wa chama hicho kuhama na kukimbilia upinzani na kusema ni wajibu wa Nape kupima na kuona kuwa kazi ya itikadi na uenezi haiwezi na kwani hajui wajibu wake akisema ni mtu wa kumhurumia.
Maige alisema mbali ya kushindwa kuzuia wimbi la wanachama kukihama CCM pia hapaswi kuvumiliwa kutokana na kauli yake kwamba hata kama wanachama watahama wote na akabaki yeye (Nape) peke yake, haitakufa. Alisema kauli hiyo haikijengi chama, bali kuchochea makundi ambayo yanaweza kukibomoa.
Alisema akiwa mwana CCM anaona kwamba sasa hivi Nape amekuwa hafanyi kazi ya uenezi na kukirejeshea haiba na mvuto ambao umepotea kwa wananchi na kwamba, kazi anayoifanya sasa ni kukuza makundi na kusema ovyo.
Aliendelea kumshambulia Nape kwa maneno akisema amejenga jeuri, kiburi, dharau na ulevi wa madaraka huku akidai kwamba kitendo cha CCM kupoteza wanachama zaidi ya 10,000 kwa wakati mmoja mkoani Arusha na sehemu nyingine wanachama 3,000 ni ishara ya hatari lakini, Nape amekuwa akiwaita wanaohama kwamba ni mzigo.
“Huyu Nape ni lazima atupishe. amekifanya chama kama mali yake, yeye ndiye mwenye jukumu la kueneza sera za chama na kutafuta wanachama wapya, lakini ndiyo kwanza anasema waachwe waondoke, Chadema wanatamba kila siku yeye hajali, huyu nasema ni gamba ni bora atupishe,” alisema.
Baada ya mashambulizi hayo, Maige alijitetea kwamba maneno yake dhidi ya Nape yasitafsiriwe kama ni kuulilia uwaziri: “Ni uchungu nilionao kwa chama changu kuona kila siku zinavyokwenda ndivyo tunavyopoteza idadi kubwa ya wanachama, tuliyemkabidhi jukumu la uenezi anasema hajali, sasa huyu si atupishe mapema kabla mambo hayajaharibika?”
“Nikuombe Mwenyekiti wa CCM Mkoa mzee wangu, Mgeja (Hamis), nafikiri ninyi wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec ya CCM) mnapaswa kuchukua hatua haraka juu ya Nape... huyu sasa ni tatizo. Chama kitawafia hivihivi mkiona, avuliwe gamba maana tukisubiri ajivue atatuchelewesha, CCM ni wanachama si Nape.”
Wakati Maige akitoa maneno hayo, Mgeja alikuwa ameinamisha kichwa chake chini huku mikono ikiwa kichwani, lakini wana CCM na wananchi wengine walikuwa wakishangilia.
Aidha, Maige aliwalaumu viongozi wa CCM katika ngazi ya wilaya na kata ambao wamekuwa na tabia ya kutowatembelea wananchi katika maeneo yao kusikiliza kero zao wakisubiri mpaka viongozi wa kitaifa ndipo na wao wajitokeze.
“Jamani inakuwaje kiongozi mwenezi wa CCM kata ama wilaya anakaa kimya kabisa hakuna kazi yoyote anayoifanya! Viongozi wa aina hii wasipewe nafasi kabisa katika uchaguzi ujao. Tupate safu ya viongozi wenye kukifia chama chetu.”
“Maana kama watu wanakuja na Operesheni Sangara hakuna anayesimama kujibu, Operesheni Vua Gamba Vaa Gwanda hakuna aliyewajibu wala CCM haijatafuta operesheni yoyote ile kukabiliana nao, sasa wameanza Operesheni Movement For Change (M4C), sisi na Nape wetu kimya tunawaangalia tu wanazoa wanachama. Tuwe makini chagueni viongozi wenye uchungu na chama,” alisema Maige.
Alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo za Maige, Nape alisema: “Nasubiri taarifa rasmi ya chama na nikiyakuta hayo nitajibu. CCM ina taratibu zake katika utendaji wake wa kazi. Katika taratibu hizo, ziara zote za viongozi wetu zinaandikiwa taarifa ambayo lazima zipite kwangu. Hayo unayosema yakinifikia, nitayajibu lakini siwezi kuzungumza bila hakika kwamba amesema.”
Mario Balotelli akiwa kwenye mazoezi na kikosi cha timu ya taifa ya Italia
Balotelli alipokuwa akitangaza azma ya kumtoa 'ngeu' mtu yeyote atakaemkebehi na kumdharau katika michuano ya Ulaya huko Poland na Ukraine
Mshambuliaji mtukutu wa Manchester City anayechezea timu ya taifa ya Italia, Mario Balotelli amesema kuwa ataondoka uwanjani endapo ataonyeshwa vitendo vya ubaguzi wa rangi wakati wa Fainali za Euro zinazoandaliwa kwa pamoja kati ya Poland na Ukraine.
Jarida ya Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC, lilisema kuwa wenyeji wa Fainali za Euro wamekuwa na tabia ya ubaguzi wa rangi na UEFA imesisitiza kuwa m chezo unawez akuvunjwa endapo itatokea hali hiyo.
Mshambuliaji huyo wa Italia, Balo, 21, alisema: “Endapo mtu atanipiga kwa ndizi mtaani, ni wazi nitakwenda jela kwa sababu nitamuua.“Ubaguzi wa rangi hauna nafasi kwangu, siwezi kuuendekeza. Naamini hakutakuwa na matatizo katika Fainali za Euro, na ikitokea nitarudi nyumbani.
“Lakini tuko katika michuano ya Euro 2012, najua haiwezi kutokea.”
Balotelli, 21, alikumbana na hali hiyo akiwa na City katika michuano ya Ligi ya Europa walipocheza na Porto mapema Februari.Lakini hakupata tabu sana na alipokuwa Inter Milan mwaka 2009 aliwahi kurushiwa ndizi.
Balotelli aliiambia France Football: “Najua wanaweza kunifuata askari kuja kunikama, kwa sababu naapa, nna ninaapa kweli nitampa mtu kipigo cha sawasawa. Nitawapiga kweli. “Lakini bado nina imani hilo haliwezi kutokea.”
Tukio lingine lililotokea Italia ni wakati Balotelli alipodhihakiwa na mashabiki wa Juventus.
Alisema: “Nakumbuka vizuri na hiyo ni kwa sababu nafunga mabao. Kimsingi, watakuwa watu wazuri na hawawezi kufikiria hilo la kukufanya ukasirike. Kikubwa wanachofanya ni kukuchanganya kwa kukukebehi. “
Nilijifanya sioni lolote lililotokea kwa sababu nilitaka kucheza mpira. Nilikuwa bado mdogo. Nilichokifanya ni kumwambia mwamuzi. Lakini kama ningemwambia mwamuzi asimamishe mchezo nisingefunga.”
Naibu waziri wa Habari Utamaduni Vijana na Michezo Amos Makalla akimkabidhi nahodha wa Stars Juma K Juma hapo jana tayari kwa safari ya leo alfajiri kwenda Ivory Coast
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Kim Poulsen amesema wanakwenda Abidjan, Ivory Coast na watawaduwaza Ivory Coast kwa mchezo wao wa kwanza kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia, 2014 zitakazofanyika Brazil.
Stars na Ivory Coast zilizopambana Mei 2010 kwenye Uwanja wa Taifa na Ivory Coast kushinda bao 1-0, zitacheza mechi yao Juni 2 ikiwa ni takribani miaka miwili, mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Houphouet Boighny ulioko katikati ya jiji la Abidjan.
Kocha wa Stars Kim Puelsen katikati, kushoto ni rais wa TFF Leodgar Tenga
Timu hiyo imeondoka leo alfajiri ikiwa na msafara wa watu 32 wakiwemo wachezaji 23 na viongozi tisa akiwemo mwandishi wa habari wa magazeti ya Mwananchi Communications Ltd.
Wachezaji hao na viongopzi waliagwa jana na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Amos Makalla na Kim aliwaambia wachezaji wake kwamba njia pekee ya kuweza kuaminiwa na Watanzania ni kuhakikisha wanashinda pambano hilo.
"Jana (juzi) jioni nilikaa na wachezaji nikawauliza mmoja mmoja unafahamu ni kwa nini umeitwa kwenye timu ya taifa, nashukuru kwamba walinijibu kwa usahihi kabisa.
"Ukweli ni kwamba niliwaambia wajiamini kwanza wenyewe kwa kuhakikisha ushindi unapatikana na baada ya hapo mashabiki na hata vyombo vya habari vitawaamini,"alisema Kim na kuongeza: "Lakini katika kufanikisha hili nimewasisitizia hakuna mafanikio pasipo nidhamu ya hali ya juu."
Naye Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo Amos Makalla aliwataka wachezaji wa Taifa Stars kutoweka mawazo kwamba Ivory Coast ni Chelsea kwa kuwa ina wachezaji maarufu kama Didier Drogba na Solomon Kalou ambao wanaichezea klabu hiyo.
Pia aliwataka waelekeze akili zao katika kupapambana dimbani badala ya kuhofia hujuma za nje ya uwanja za wapinzani wao.
Mkuu wa msafara huo ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, Crescentius Magori na pamoja na Makamu wa Rais wa Chama cha Soka Zanzibar, ZFA, Haji Ameir Haji.
Viongozi walioambatana na timu hiyo ni Kim Poulsen na msaidizi wake Sylvester Marsh na kocha wa makipa, Juma Pondamali 'Mensar'.
Wengine ni meneja wa timu hiyo, Leopord Tasso Mukebezi, daktari wa timu Mwanandi Mwankemwa, mtaalamu wa viungo Frank Mhonda na mtunza vifaa, Alfred Chimela.
Wachezaji wa Stars ni nahodha: Juma Kaseja, Aggrey Morris, Mwadini Ally, Deogratius Munishi, Nassor Masoud Cholo, Amir Maftah, Erasto Nyoni, Kelvin Yondan, Waziri Salum, Shomari Kapombe na Juma Nyoso.
Wengine ni Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Salum Aboubakar, Shaaban Nditi, Edward Christopher, Mrisho Ngassa, Frank Domayo, Mbwana Samata, Ramadhan Singano, Simon Msuva, Haruna Moshi 'Boban' na John Boko.