Monday, April 23, 2012

NGORONGORO HEROES YAIADABISHA SUDAN


Thomas Ulimwengu

Timu ya taifa ya Tanzania chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes, imepata ushindi kwa kuwachabanga vijana wenzao kutoka Sudan jumla ya magoli 3 -1 katika mechi ya mkondo wa kwanza kufuzu fainali Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 20.

Mechi hiyo ilichezwa Jumamosi katika uwanja mkuu wa taifa mjini Dar es Salaam.

Thomas Ulimwengu, mchezaji anayechezea klabu ya TP Mazembe ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo ndiye aliyeanza kufunga goli la kwanza kwa upande wa Tanzania katika dakika ya 13 kipindi cha kwanza.

Iliwachukua timu ya Tanzania dakika tano ambapo katika dakika ya 18 Ramadhani Singano alipachika goli la pili na hivyo hadi mapumziko matokeo yalikuwa 2-0.

Katika kipindi cha pili timu ziliingia uwanjani kwa ari kubwa ya kupata magoli ambapo zilionekana kushambuliana kwa zamu.

Ni Tanzania tena waliobahatika kupata goli mwishoni mwa kipindi cha pili katika dakika ya 43 kupitia Simon Msuva.

Hata hivyo Sudan walionekana kutokata tamaa ambapo katika dakika ya 46 Ahmed Nas Eldin alipachika goli la kufuta machozi kwa upande wa Sudan, na mpira ukamalizika kwa matokeo ya 3-1.

Timu hizi zinatarajiwa kucheza mechi ya mkondo wa pili wiki mbili zijazo mjini Khartoum, Sudan, kati ya Mei 4, 5 au 6 mwaka huu.

Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 20 zinatarajiwa kuchezwa nchini Algeria mwaka 2013.

Bingwa mtetezi ni Nigeria.

No comments:

Post a Comment